Elimu juu ya madhara ya vitendo vya ukatili, Sensa yashika kasi Serengeti

NA FRESHA KINASA

SHIRIKA la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia lenye makao makuu yake Mugumu Wilaya ya Serengeti Mkoa wa wa Mara kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Wilaya ya Serengeti wameendelea na kampeni ya utoaji wa elimu kwa njia ya mikuano ya hadhara kuhusiana na madhara ya vitendo vya ukatili wa kijinsia katika kata za Rung'abure, Nyamoko na Geita Samo zilizopo wilayani humo. 
Akizungumza na wananchi wa kata hizo kwa nyakati tofauti wakati wa utoaji wa elimu hiyo Julai 15, 2022, Afisa Mwelimishaji Jamii kutoka Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Emmanuel Goodluck amesema, elimu hiyo itazifikia kata 22 za Wilaya ya Serengeti ambapo wananchi watapewa elimu hiyo katika mikutano ya hadhara. 

Goodluck amewaomba wananchi waliopata elimu hiyo wawe mabalozi wa kutoa elimu hiyo kwa watu wengine. Huku akiwaomba wananchi kutowakeketa mabinti wakati wa likizo bali wawalinde sambamba na kushiriki kuhesabiwa Siku ya Sensa Agosti 23, mwaka huu.

"Niwaombe pia wazee wa kimila msaidie kumaliza ukeketaji, tumieni nafasi yenu kutokomeza ukeketaji. Mila ya ukeketaji haifai ina madhara makubwa kiafya, tuwalindeni watoto wa kike badala ya kuufanya ukejetaji kama njia ya kujipatia kipato zipo fursa nyingine nyingi ambazo zinaweza kusaidia kuingiza kipato kama vile kilimo, ufugaji, biashara, ujasiriamali na pia kutumia fursa ya kuunda vikundi kupata mikopo kutoka halmashauri hizi ni njia halali za kupata kipato na sio fedha ambazo zinatokana na malipo baada ya binti kukeketwa,"amesema Goodluck. 
Akizungumzia madhara ya ukeketaji, SSGT Titus Mufuluki kutoka Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Serengeti amesema, ukeketaji una madhara ikiwemo maumivu makali wakati wa kukeketwa, kutokwa damu nyingi wakati wa kukeketwa.

Sambamba na hatari ya kupata magonjwa ya kuambukiza kama UKIMWI kutokana na kutumia kifaa kimoja wakati wa kuketa, kuchangia ndoa za utotoni kwani binti anapokeketwa huandaliwa kuozeshwa, madhara ya kisaikolojia, kupoteza maisha kutokana na kutokwa damu nyingi pamoja na kutojiamini katika jamii. 

Ameongeza kuwa, njia za kumaliza ukeketaji ni pamoja na kutekeleza sheria za ukeketaji kifungu namba 169( A ) kanuni ya adhabu iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019 ambayo inatoa adhabu kuanzia miaka 5-15 pamoja na kulipa fidia kwa mhanga milioni moja hadi milioni tano.

 

Pia kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara ya ukatili wa kijinsia, viongozi wa dini na vyama vya siasa kutoa elimu, kuwawezesha kiuchumi wanawake, kutoa elimu kwa umma kuhusiana na madhara ya ukatili wa kijinsia ukiwemo ukeketaji, mashahidi kufika mahakamani kutoa ushahidi ili waliokamatwa wakifanya vitendo hivyo wapewe adhabu kwa mujibu wa sheria.

Pia, SSGT Mufuluki amewaomba wananchi hao, kutoa taarifa mapema kabla binti hajakeketwa wanapoona maandalizi na viashilia mapema ili kuwaokoa kabla hawajafanyiwa vitendo hivyo huku akisema kila mmoja awe mstari wa mbele kupinga ukeketaji na aina mbalimbali za ukatili wa Kijinsia kwani ni kikwazo cha usawa katika Jamii na ustawi bora kwa maendeleo kuanzia ngazi ya familia. 
Paul Paresso ni Afisa wa Polisi kutoka Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Serengeti akizungumza na wananchi wa kata hizo kwa nyakati tofauti kwa niaba ya OCD Wilaya ya Serengeti amesema kuwa, Serikali itawachukulia hatua kali za kisheria wananchi watakaojihusisha na vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji kwani ni kosa kisheria na kwamba wamejipanga vyema kudhibiti vitendo hivyo kabla havijafanyika. 

Katika hatua nyingine, amewaomba wananchi hao kusisimamia maadili mema na malezi bora kwa watoto wao na kuwafundisha tabia njema sambamba na kufuatilia maendeleo yao ya kitaaluma katika kuandaa kizazi bora kitakacholeta mabadiliko chanya katika jamii na taifa kwa ujumla. 
Akizungumzia kuhusu Dawati la Jinsia na Watoto,CPL Sijali Nyambuche kutoka Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Serengeti amewaambia wananchi hao kuwa, ni sehemu maalumu katika Kituo cha Polisi inayoshughulikia walioathirika na ukatili na unyanyasaji na kingono na kutoa taarifa kituo cha polisi.
Sijali amesema, lengo la kuanzishwa kwa Dawati la Jinsia ni kusikiliza malalamiko katika hali ya usiri mkubwa, kumpa ushauri muathirika wa ukatili kutegemeana na malalamiko aliyowathirisha, kumpa huduma ya kwanza iwapo inahitajika ikiwa ni pamoja na kuandaa PF3 na kumpeleka hospitali, ambapo amesema huduma ya Dawati hutolewa na maofisa wa polisi wa kike na wakiume kutegemeana na jinsia ya muathirika ambaye ameshahudhuria mafunzo maalumu kwa ajili hiyo. 

Ameongeza kuwa, wajibu wa muathirika wa ukatili wa Kijinsia ni pamoja na kwenda kutoa ushahidi mahakamani na pengine kumtambua mtenda makosa, kujua jina, anwani, na namba ya simu ya mpelelezi wake pamoja na maendeleo ya upelelezi wa Jambo alilolitolea taarifa, kutoa maelezo yake yote kwa Ofisa wa dawati la Jinsia na watoto bila kuficha Jambo lolote kwani atahakikishiwa usiri wa taarifa yake. 

Pia CPL Sijali amesema, huduma ya Dawati kwa upande wa Watoto ni kuhakikisha watoto wanapata haki ya kulindwa dhidi ya aina zote za ukatili na unyanyasaji na kwamba endapo haki ya mtoto itavunjwa kosa hilo linatakiwa kutolewa taarifa haraka kwenye dawati la Jinsia na Watoto mara moja, na kwamba kila dawati linalenga kutoa mazingira rafiki kwa mtoto. Ambapo maafisa wa dawati watafanya kazi pamoja na Maafisa wa Ustawi wa Jamii ili kufuatilia kesi zinazohusu Watoto sambamba na kuwasaidia watoto wakati wa mahojiano na wakati wote wa hatua za mfumo wa haki kutokana na wao kuwa katika hatua za kutishika kurahisi.
Nao wananchi wa kata hizo wamelipongeza Jeshi la Polisi Wilaya ya Serengeti na Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania ( HGWT) kwa kutoa elimu hiyo kwa wananchi kwani itasaidia kuleta ufanisi katika kutokomeza vitendo vya ukeketaji hasa mwaka huu ambao unagawanyika kwa mbili ambapo koo nyingi za kabila la kikurya zimejipanga kukeketa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news