LATRA yapigilia msumari agizo la RC Kafulila, yasema michomoko marufuku nchini

NA DIRAMAKINI

BARAZA la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini (LATRA) limetoa tamko kali kuunga mkono maamuzi magumu aliyochukua Mkuu wa Mkoa Simiyu, David Kafulila ya kupiga marufuku gari ndogo zinazotumika kusafirisha abiria maarufu kama michomoko kuanzia Julai 13, 2022. 
Mheshimiwa Kafulila alipiga marufuku gari hizo kuendelea kutumika kutokana na kuwa sababu kuu ya ajali mkoani Simiyu kufuatia gari hizo kutumika kubeba abiria wengi na kukaidi agizo lake la muda mrefu kutaka zitumike kama teksi badala ya kujigeuza daladala kwa kubeba abiria wengi zaidi ya uwezo. 

"Kwa kuwa kutokana na mwenendo usioridhisha gari hizi zimekuwa chanzo kikubwa cha ajali, na kwa kuwa gari hizi zimekaidi maelekezo ya Serikali kutaka zifuate taratibu za kujiendesha kama teksi kwa kisingizio kuwa mfumo huo haulipi kibiashara, basi kuanzia leo Julai 13, 2022, nasitisha usafiri wa MICHOMOKO mpaka hapo itakapoamuliwa vinginevyo,"alisisitiza RC Kafulila.

Katika tamko lao, LATRA wamesisitiza wakuu wa mikoa mingine kufuata mfano huo ili kukabili tatizo la ajali nchini kwani gari hizo sio salama, ni hatari kwa usalama wa wananchi kwani zimekuwa chanzo cha ajali maeneo mengi nchini na kuahidi kushirikiana na vyombo vingine ikiwemo jeshi la polisi kuhakikisha inafanyika operesheni nchi nzima.

Post a Comment

0 Comments