Makamu wa Rais Dkt.Mpango, mkewe waungana na wanakijiji Kasumo kushiriki ibada ya katikati ya wiki

NA MWANDISHI WETU

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiambatana na mkewe Mama Mbonimpaye Mpango wameungana na waumini wa Kijiji cha Kasumo mkoani Kigoma katika kushiriki Ibada ya kawaida ya katikati ya wiki katika Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani iliopo Kijiji hapo. 

Ibada hiyo imefanyika leo tarehe 29 Julai 2022 na kuongozwa na Paroko wa Parokia hiyo Padre Joseph Mashaka akishirikiana na Padre Francis Laswai.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango na mkewe Mama Mbonimpaye Mpango wakiongozana na Paroko wa Parokia ya Kasumo Padre Joseph Mashaka (wa pili kushoto) pamoja na Padre Francis Laswai ( wa Kwanza kushoto) mara baada ya kumalizika kwa Ibada ya kawaida ya Asubuhi katika Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani iliopo Kijiji cha Kasumo mkoani Kigoma leo tarehe 29 Julai 2022. 

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa ibada hiyo, Padre Francis Laswai ameiomba serikali kuusaidia mkoa wa Kigoma katika sekta ya kilimo ili waweze kuzalisha mazao mengi zaidi kutokana na uwepo wa mvua za kutosha katika mkoa huo. 

Padre Laswai ameongeza kwamba mkoa huo unahitaji kilimo cha kisasa hivyo wataalamu wa kilimo wenye uzoefu ni muhimu wakatembelea maeneo ya vijijini na kushauri vema wakulima ili kuongeza uzalishaji.

Aidha, Padre huyo ameomba kuongezwa vitendea kazi ikiwemo matrekta yatakayowezesha wakulima kufanya kilimo cha kisasa. 

Kuhusu mazingira Padre Laswai amesema mkoa huo unakabiliwa na imani potofu za uchomaji misitu kwa kudhani anaechoma anaweza kuishi muda mrefu hali inayopelekea kuharibu mazingira pamoja na miundombinu ya umeme.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akizungumza na waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani iliopo Kijiji cha Kasumo mkoani Kigoma leo tarehe 29 Julai 2022 baada ya kumaliza kushiriki Ibada ya kawaida ya asubuhi kijiji hapo. 

Makamu wa Rais amewataka wananchi wa kijiji hicho kuwalea watoto wao kwa maadili na nidhamu ili kupata taifa lililobora kwa sasa na baadae. 

Amesema wananchi wa Kijiji hicho wanapaswa kuiga mfano wa maisha ya hapo awali ambayo yalikuwa ni kufanya kazi kwa bidii pamoja na kuzingatia suala la elimu kwa watoto.

Halikadhalika Makamu wa Rais amewaasa waumini hao kubadilika mara moja na kuacha tabia za kuharibu misitu kwa kuichoma moto kwa imani zisizofaa. 

Ameiagiza halmashauri ya wilaya ya Buhigwe kusimamia kikamilifu sheria ndogo za kudhibiti uharibifu wa mazingira kwa kushirikiana na vyombo vya dola kuhakikisha wote wanaoharibu mazingira wanachukuliwa hatua.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango na mkewe Mama Mbonimpaye Mpango wakishiriki Ibada ya kawaida ya asubuhi katika Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani iliopo Kijiji cha Kasumo mkoani Kigoma leo tarehe 29 Julai 2022.

Makamu wa Rais amewasihi wananchi wa Kasumo kujitolea kwa hali na mali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kijijini hapo pamoja na kuwaasa viongozi serikali ya kijiji kuendelea kutoa ardhi kwaajili ya ujenzi huduma za kijamii kama vile shule na zahanati.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news