Serikali yatenga Bilioni 3/- kufadhili wanafunzi wenye alama za juu masomo ya sayansi nchini

NA GODFREY NNKO 

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda amesema kuwa, Serikali imetenga shilingi Bilioni 3 kwa mwaka huu kwa ajili ya kuwezesha ufadhili kwa wanafunzi ambao wamepata ufaulu mkubwa katika elimu ya juu kupitia masomo ya sayansi.
Prof.Mkenda ameyasema hayo leo Julai 29,2022 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza katika mkutano maalumu wa kikazi kati ya Wizara ya Elimu na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini.

"Kigezo cha atakayepatiwa ufadhili huo ambao wengi wanataka uitwe Samia Scholar ni kufaulu vizuri katika masomo ya sayansi na upo tayari kuendelea na kusoma masomo ya uhandisi,elimu tiba.Kwa sasa tunatoa udhamini huo kwa vyuo vya ndani tu,"amesema Prof.Mkenda

Mheshimiwa Profesa Mkenda amesema, utaratibu huo ni wa kudumu na huenda mwakani wakaongeza zaidi kiasi hicho cha fedha ili kuweza kuwapa fursa wanafunzi wengi zaidi.

"Pia tutaweka dirisha kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu ili nao waweze kunufaika na ufadhili huo ambao utakuwa unatolewa bila kujali huyu katoka wapi au familia gani, ilimradi awe amefaulu vizuri sayansi na afahamu kuwa, anasoma kwa kodi ya Watanzania, hivyo anapaswa kuonesha bidii ili aje kuwahudumia kupitia taaluma yake,"amesema.

Amesema kuwa, wametoa ufadhili wa sayansi kwa sababu Dunia ya sasa,sayansi na teknolojia imeshika kasi, hivyo kila mmoja anatamani kuwekeza sana katika sayansi.

"Tunapenda kuwekeza kwenye sanyasi ili tusonge mbele. Kwa hiyo tutaendelea kuwekeza katika sayansi, teknolojia na elimu tiba ili iweze kuwa na manufaa kwa jamii yetu na Taifa kwa ujumla,"amesema Waziri.

Wakati huo huo, amesema ushirikiano kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) umekuwa na mafanikio makubwa katika juhudi za kuimarisha utoaji na upatikanaji wa elimu bora nchini.

"Mwenye sera ni Wizara ya Elimu, mtekelezaji ni TAMISEMI, hivyo tunashukuru kwa kuwa kupitia TAMISEMI tunafanya kazi vizuri sana.

"Tusiporuhusu kuwepo kwa mfumo ambao unapeleka madaraka chini, hatuwezi kufika mahali. Hivyo, mfumo wetu tulionao ni mzuri na tunafanya kazi vizuri na TAMISEMI, jambo la msingi tutaendelea kuimarisha ushirikiano wetu kati ya wizara na TAMISEMI ili kuhakikisha tunatoa elimu bora na huduma bora kwa watoto wetu nchini,"amesema Prof.Mkenda.

Pia amesema, Serikali itaendelea kuhakikisha inatoa elimu katika maeneo yanayofika kwa ajili ya wananfunzi wote na pale ambapo kuna ugumu kuangalia namna ambavyo itajenga shule za mabweni ili kuwapa nafuu wanafunzi.

Waziri Prof.Mkenda amesema, huko mbeleni wanatarajia kuona elimu ujuzi inashika nafasi kubwa ili kuhakikisha kila mwanafunzi anatumia ujuzi wake kwa manufaa ya jamii na Taifa.

Amesema, elimu ujuzi ni miongoni mwa hatua na mikakati muhimu ambayo Serikali inaiendea kwa kuwa inatambua licha ya elimu ujuzi kuwa na manufaa pia ni njia rahisi ya kila mtu kuwa na uwezo wa kujiajiri au kuajiri.

Kwa mwaka huu wanakusanya maoni kuhusu mfumo uliopo wa elimu kwa upande wa sera na mitaala ili mwishoni mwa mwaka waweze kuingia katika vikao vya mchakato wa maamuzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news