Makamu wa Rais:Serikali itahakikisha dawa muhimu zinapatikana vituo vya afya

NA FRED KIBANO

SERIKALI imesema imejipanga kuhakikisha dawa muhimu zinapatikana katika vituo vya afya na hospitali mbalimbali ili kusogeza huduma karibu na wananchi.
Akiongea baada ya kuweka jiwe la msingi katika Kituo cha Afya Nsemulwa Mpanda Manispaa jana Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe.Dkt. Philip Mpango amesema suala la dawa linaendelea kupatiwa ufumbuzi ambapo mpaka upatikanaji wake ni asilimia 90 katika vituo vya afya na hospitali.

“Serikali imejipanga kusogeza miundombinu ya huduma mbalimbali ya afya,elimu, maji kwa wananchi tunaendelea kuhakikisha jitihada ya dawa muhimu zinapatikana katika vituo vyetu vya afya na hosptali mbalimbali na hivi sasa upatikanaji wa dawa ni asilimia 90,”alisema Dkt. Mpango.
Dkt. Philip Mpango amesema kukamilika kwa kituo hicho kwa mapato ya ndani ya Halmashauri kutasaidia kupunguza msongamano katika hospitali ya wilaya na ile ya rufaa kwa kuwa huduma zote za msingi zitatolewa katika kituo cha afya Nsemulwa. 

Amewaasa wazazi kuzingatia masuala ya lishe bora kwa watoto kwani lishe duni inasababisha kuzaliwa kwa watoto ambao hawana uwezo mkubwa wa kufikiri na hili litaepukika kwa kuzingatia lishe bora kwa kuwa mkoa wa Katavi unazalisha chakula kingi mpaka ziada ya kuuza nje ya mkoa na nje ya nchi ya Tanzania.
Katika hatua nyingine Dkt. Philip Mpango amewaagiza  Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuacha kuwatoza wananchi ushuru wa mazao chini ya tani moja kwa kuwa Serikali ilikwishatoa agizo hilo la kuacha kuwatoza wakulima ikiwa ni pamoja na kujenga barabara ya lami kutoka katikati ya Mji wa Mpanda hadi kituo cha Afya Nsemulwa ambayo ni umbali wa zaidi ya kilomita moja ili kuondoa adha kwa wagonjwa.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Dkt. Festo Dugange amesema katika kuboresha Sekta ya Afya mkoani Katavi magari mawili ya wagonjwa yaliletwa, mashine nne za mionzi zimeletwa ambapo moja itakuwa Manispaa ya Mpanda lakini pia Serikali imeondoa ada kidato cha tano na sita ili kuwapa nafuu wananchi. 

Akisoma taarifa ya Kituo cha Afya cha Nsemulwa Dkt. Paul Swakala Mganga Mkuu wa Manispaa ya Mpanda amesema kuwa fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri kiasi cha shilingi milioni 336 yalipokelewa na kutumika ambapo mpaka sasa maabara, vyoo na jengo la wagonjwa wa nje limekamilika na majengo mengine yapo katika hatua mbalimbali.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe.Mwanamvua Mlindoko amesema jumla ya vituo vitatu vinajengwa kwa fedha za mapato ya ndani ambavyo ni pamoja na Kituo cha Afya Nsemulwa Mpanda Manispaa, Halamashauri za Mpimbwe na Tanganyika ambavyo kila kimoja kitagharimu shilingi milioni 500 na ujenzi wake upo katika hatua mbalimbali.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Mhe. Jamillah Yusuph amesema Wilaya yake ilipokea jumla ya shilingi Bilioni 33.03 kwa ajili ya kutekeleza miradi yote ya maendeleo kwenye Wilaya yake lakini pia fedha zilizojenga kituo cha Afya Nsemulwa zimetokana na mapato ya ndani na sio fedha za Serikali Kuu hivyo hii ni dalili ya kuanza kujitegemea.

Post a Comment

0 Comments