Sensa ya Watu na Makazi ilivyobeba majibu ya ustawi bora wa maisha yetu

NA GODFREY NNKO

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepanga kufanya Sensa ya Watu na Makazi ifikapo mwezi Agosti 2022.

Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS), ipo kwenye maandalizi ya kufanya sensa hiyo.

Sensa ya Watu na Makazi ni zoezi la kitaifa linalofanyika kila baada ya miaka 10 ambapo Sensa ya mwisho kufanyika nchini ni ile ya mwaka 2012.

Uzinduzi rasmi

Septemba 14, 2021 jijini Dodoma Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alizindua rasmi Mkakati wa Uelimishaji na Uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Rais Samia alisema, lengo la mkakati huo ni kupata taarifa sahihi za idadi ya watu waliopo nchini ikiwemo jinsia, elimu, afya na hali za ajira ili kuwa na takwimu sahihi zitakazoiwezesha Serikali kupanga mipango ya maendeleo kwa ajili ya watu wake.

“Taarifa za Sensa zitatusaidia kujua idadi ya watu wapi walipo, elimu zao, afya zao, hali ya ajira zao pamoja na makazi yao, pia zitatusaidia kujua ongezeko la watu wetu ili tuandae Sera ya Taifa na kujua mgawanyo wa rasilimali kwa uwiano sawa kwa wananchi wetu,”alisisitiza Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amesema, haiwezekani kupeleka huduma kwa wananchi wa eneo fulani kama haijulikani idadi ya watu katika eneo husika ambapo amewataka wananchi wote watakaolala ndani ya mipaka ya Tanzania usiku wa kuamkia siku ya sensa kushiriki zoezi hilo.

Pia, Rais Samia amesema,taarifa za sensa hutumika pia kwa watafiti wengi wa ndani na nje ya nchi katika shughuli zao mbalimbali kwa lengo la kuleta maendeleo ya kijami, kisiasa na kiuchumi.

Kufuatia hatua hiyo, Rais Samia alitoa wito kwa viongozi mbalimbali nchini wakiwemo viongozi wa dini, kuhakikisha wanawahamasisha wananchi ili washiriki kikamilifu katika zoezi la sensa litakalofanyika Agosti, 2022.

Waziri Mkuu

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amesema jukumu la kusimamia zoezi la sensa lipo chini ya ofisi yake pamoja na ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambapo amemuhakikishia Rais Samia kwamba watu wote watakaolala ndani ya mipaka ya Tanzania kuamkia siku ya sensa watahesabiwa.

“Sina shaka na nikuhakikishie Mheshimiwa Rais kwamba, maagizo yako yote uliyoyatoa tutayafanya kama ulivyoelekeza na nikuahidi kwamba watu wote watakaolala ndani ya mipaka ya Tanzania kuamkia siku ya sensa watahesabiwa,”alisema Majaliwa.

Sensa ya Sita

Hivyo Sensa ya mwaka 2022 itakuwa ni sensa ya sita kufanyika nchini baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012.

Umuhimu wa kipekee wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ni pamoja na kuisadia Serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025, mageuzi ya masuala ya afya na jamii, pamoja na ufuatiliaji wa ajenda za maendeleo za kimataifa.

Pia, taarifa za idadi ya watu husaidia katika mamlaka za wilaya katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ambayo huakisi matakwa ya watu katika ngazi husika na kusaidia kwenye uwiano wa mgawanyo wa rasilimali.

Aidha, taarifa za msingi za hali ya kidemografia, kijamii na kiuchumi za idadi ya watu na makazi za mipango katika ngazi zote huwa zinasaidia kigawio katika kukokotoa viashiria vingine mfano pato la mtu mmoja mmoja, Pato la Taifa, ajira na ukosefu wa ajira na kiwango cha uandikishaji wa wanafunzi.

Kwa mujibu wa NBS, taarifa hizo zitawezesha serikali kujua ongezeko la idadi ya watu, kwa mgawanyo na viashiria vingine, ambavyo ni muhimu kwa usimamizi wa mazingira na msingi wa utawala bora na ujumuishaji wa demokrasia.

Wakati huo huo, takwimu sahihi za sensa zinahitajika kwa ajili ya ugawaji wa majimbo ya uchaguzi kwa ufanisi na kurekebisha mipaka ya kiutawala katika serikali za mitaa.

Sensa ya 2022

Mtakwimu Mkuu wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dkt. Albina Chuwa anasema, sensa ya mwaka huu inatarajiwa kuwa na vitu vipya ikiwemo kutenga maeneo ya kijiografia ya kuhesabia watu katika ngazi za kitongoji au mtaa.

Sambamba na upatikanaji wa taarifa za kitakwimu katika ngazi za kitongoji au mtaa pamoja na kuwa na mipaka ya kudumu katika ngazi hizo.

Dkt.Chuwa anasema,vishikwambi (tablets) vitatumika katika hatua zote za utekelezaji wa sensa kwa lengo la kupunguza gharama.

"Na kutakuwa na nyongeza ya maswali yatakayowezesha upatikanaji wa taarifa zaidi za kitakwimu ikilinganishwa na Sensa ya Mwaka 2012 ikiwemo taarifa za kidemografia (umri wakati wa ndoa ya kwanza) na maswali yanayohusu ulemavu (kichwa kikubwa, mgongo wazi, kifafa, mbalanga na usonji).

"Maswali ya uhamaji kulingana na mapendekezo ya Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (International Organization of Migration-IOM), maswali kuhusu umiliki wa nyaraka za kitaifa (vitambulisho NIDA, vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo wadogo, Mzanzibari mkazi, hati ya kusafiria, na leseni ya udereva.

"Pia kuna maboresho ya maswali ya shughuli za kiuchumi ikiwa ni pamoja na idadi ya kaya ziliko kwenye sekta isiyo rasmi, umiliki wa ardhi na taarifa za TEHAMA, takwimu za nyumba (orodha, hali ya umiliki na aina ya nyumba), maswali ya kilimo na mifugo,"amefafanua Dkt.Chuwa.

Rais Dkt.Mwinyi

Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameeleza matumaini yake makubwa kwamba zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka huu litakwenda vizuri kutokana na matayarisho mazuri yaliyofanyika ikiwa ni pamoja na kufanikiwa kwa Sensa ya Majaribio.

Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo Machi 2, 2022 wakati alipokutana na Kamisaa wa Sensa Zanzibar, Balozi Mohamed Haji Hamza akiwa na ujumbe wake Ikulu jijini Zanzibar wakati alipofika kwa ajili ya kutoa taarifa juu ya Sensa ya Majaribio iliyofanyika pamoja na muendelezo wa matayarisho ya zoezi hilo linalotarajiwa kufanyika mwezi Agosti, mwaka huu.

Katika maelezo yake Rais Dkt.Mwinyi amesema kwamba, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo tayari kuendelea kuunga mkono jitihada hizo na kusisitiza kwamba zoezi hilo kwa vile lina maslahi mapana ya Taifa na wananchi wake, Serikali itaendelea kuliunga mkono wakati wote.

Rais Dkt.Mwinyi amepongeza utaratibu uliwekwa wa ajira kwa watendaji wa zoezi hilo kwani mfumo huo utaondosha malalamiko yaliyowahi kutokea hapo siku za nyuma sambamba na kuweza kupata ufanisi mkubwa kutokana na watendaji ambao watatoka katika maeneo husika.

Amesema kwamba, kutokana na utaratibu huo ana matumaini makubwa kuwa hakutokuwa na eneo ambalo watapatikana watu ambao hawatokuwa na sifa za kufanya kazi hiyo ambayo ina umuhimu mkubwa katika maendeleo ya nchi.

Kamisaa wa Sensa

Naye Kamisaa wa Sensa Zanzibar, Balozi Mohamed Haji Hamza alitoa pongezi kwa Rais Dkt.Mwinyi kwa miongozo na maelekezo anayotoa juu ya matayarisho ya Sensa ya Watu na Makazi ya Agosti mwaka huu 2022, na kueleza kwamba sensa ya majaribio imefanyika kwa ustadi mkubwa na kuleta matokeo mazuri.

Amesema kuwa, matokeo ya Sensa ya Majaribio ni mazuri kwani zoezi hilo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika maeneo yote yaliyochaguliwa kufanyika na kuwashukuru wananchi kwa ushirikiano makubwa waliyoonesha katika maeneo yote ya majaribio Unguja na Pemba.

Amesema kuwa, matokeo ya Sensa ya Majaribio hutumika kwa matumizi ya ndani ambayo huwa ni kigezo kinachotumika kupima nyenzo zote za utekelezaji wa zoezi la Sensa pamoja na kuzifanya kazi changamoto zilizoonekana ili kuhakikisha zoezi hilo ifikapo Agosti 2022 linafanikiwa.

Balozi Hamza alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa Rais Dkt.Mwinyi pamoja na viongozi wengine wote wakuu wa Serikali kwa kufanya uhamasishaji mkubwa wa zoezi la Sensa ikiwa ni pamoja na kuzitumia hotuba zao wanazozitoa kwa wananchi.

Amesema kuwa, tayari wameshakutana na mawaziri wa wizara zote Zanzibar kuwapa mukhtasari wa zoezi hilo na kuwaomba watumie nafasi zao katika kila mikutano wanayoifanya kwa azma ya kuwafikishia ujumbe wananchi.

Ameeleza kwamba taasisi zote za Serikali zikiwemo mikoa na wilaya zimeshakabidhiwa majukumu ya utendaji kuhusu kuhamasiha zoezi hilo la Sensa huku akipongeza ushirikiano wanaopata kutoka ngazi ya Taifa hadi katika uongozi wa masheha.

Kaimu Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mashavu Khamis Omar alieleza namna ya zoezi hilo litakavyofanyika siku itakapofika, kwani kila mwananchi atahesabiwa katika eneo husika alilolala na hapatatokea mtu kuhesabiwa mara mbili hiyo ni kutokana na teknolojia itakayotumika.

Kamisaa Makinda

Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Mhe.Anne Makinda, amewasihi wananchi siku hiyo ya zoezi la Sensa ya Watu na Makazi kuhesabiwa na kushiriki kikamilifu ili Serikali ipate idadi ya watu wake kamili kwa kila eneo kuanzia ngazi ya chini.

"Tunaendesha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ili tujue Tanzania tuko watu wangapi, na itaisaidia Serikali katika upangaji wa mipango ya maendeleo kwa wananchi wote kulingana na idadi yao.

"Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akitafuta fedha za maendeleo kwa wananachi wake, na anataka kujua ni maeneo gani ambayo wananchi bado hawana maendeleo kwa uwiano sawa na idadi yao, hivyo nawasihi jitokezeni kuhesabiwa katika Sensa ya Watu na Makazi,"ameongeza.

Aidha, amewataka pia wananchi watoe ushirikiano kwa makarani wakati wa sensa pamoja na kutoa taarifa za kweli na usahihi na siyo kudanganya ili siku huduma zikianza kutolewa na Serikali katika eneo husika kusiwepo na mapungufu.

"Kama wewe una ng'ombe 100 wataje wote usiseme una ng'ombe 10, ili siku madawa yakija kulingana na idadi ya mifugo mlioitaja msianze kugombania na kulalamika madawa hayatoshi na wakati awali nyie ndiyo mlitoa taarifa siyo sahihi,"amesema Makinda.

Diwani

Diwani wa Kata ya Majengo jijini Dodoma, Shifaa Ibrahim naye amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa katika Sensa ya Watu na Makazi itakajayofanyika Agosti 23, 2022 ili kuiwezesha Serikali kuwaletea maendeleo.

"Mimi nipo tayari kuhesabiwa wewe je? Napenda kuwakumbusha ndugu zangu wote tarehe kuwa tarehe 23 Agosti, 2022 tuwe tayari kuhesabiwa. Naomba mwambie mwenzio mimi nipo tayari kuhesabiwa, mwenzangu je?. Tujitokeze kwa wingi tusifiche umri wetu, tuhesabiwe ili serikali yetu iweze kutusaidia kimaisha, kimapato na kimaendeleo.”

Kwa upande wake mfanyabiashara katika Soko la Majengo, Safina Kessy alisema kuwa yupo tayari kwa zoezi la sensa kutokana na hamasa aliyoipata.

Naibu Spika

Azan Zungu ambaye ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Ilala amewaasa Watanzania kushiriki kikamilifu Sensa ili kutimiza lengo la Serikali kupata takwimu za msingi za watu na hali za makazi ambazo zitasaidia kutunga sera, kupanga na kufuatilia mipango ya maendeleo.

“Tunapaswa kushiriki Sensa kikamilifu kwani litaisaidia taifa kupata takwimu za msingi zitakazotumika kuleta maendeleo nchini,”amesema.

Naye Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mchikichini wilayani Ilala, Hellen Madanganya amesema kuwa,Sensa ya Watu na Makazi ni moja ya zoezi linalokusanya taarifa za kila mtu aliyelala ndani ya mipaka ya nchi usiku wa kuamkia siku ya sensa.

Katibu huyo amesema kuwa, Sensa ya mwaka 2022 kama zilivyo sensa zilizopita itahusisha makarani wa sensa ambao watatembelea kaya zote nchini na kufanya mahojiano ya ana kwa ana baina ya Karani wa Sensa na Mkuu wa kaya.

Amesema, ikiwa mkuu wa kaya hatakuwepo, karani wa sensa atafanya mahojiano na mtu mzima yeyote katika kaya ambaye ana taarifa za kutosha kuhusu kaya na wanakaya wenzake waliolala katika kaya husika usiku wa kuamkia siku ya sensa.

Madanganya amesema kuwa, lengo la sensa ya watu na makazi ni kupata taarifa sahihi za kidemografia, kijamii, kiuchumi na hali mazingira kwa lengo la kupata takwimu sahihi zitakazoiwezesha serikali na wadau wengine kupanga kwa usahihi mipango ya maendeleo ya watu wake katika sekta mbalimbali za elimu, afya, hali ya ajira,miundombinu kama barabara,nishati na maji safi.

"Kwa msingi huo, sensa ni zoezi muhimu ambalo kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kushiriki na kutimiza wajibu wake ili kuhakikisha inakuwa ya mafanikio makubwa.

“Hii itasaidia serikali kutimiza wajibu wake kwa wananchi kulingana na idadi ya watu ya eneo husika ikiwa kama msingi mkubwa wa ugawaji ya keki ya Taifa kwa kila eneo la utawala hapa nchini,”amesema Madanganya.

Mbunge

Prof.Sospeter Muhongo ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara amewataka wananchi wote kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa.

"Na mimi mwenyewe tarehe 23, 2022 kwa kuwa ni raia mwema najipenda, napenda jimbo langu la Musoma Vijijini, napenda taifa langu Tanzania itabidi nitulie nyumbani nisubiri kuhesabiwa, ndugu zangu nawaomba sana tuhesabiwe wote kwa asilimia 100,"amesema Prof. Muhongo.

Wito

Katika hatua nyingine, Serikali imewataka viongozi wa dini nchini kuwaelimisha waumini wake umuhimu wa kuhesabiwa katka Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti, mwaka huu.

Aidha, imewataka viongozi wa dini kuendelea kusaidia katika suala zima la malezi ya kiroho ili kujenga jamii yenye kumcha Mungu, uadilifu na ubinadamu.

Akizungumza Machi 20, 2022 kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati wa Kutabaruku Kanisa la Bikira Maria wa Fatima mkoani Geita, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula alisema, Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi ambazo bila ya kuwa na takwimu sahihi haitaweza kupanga mipango thabiti ya matumizi endelevu ya rasilimali hizo.

‘’Viongozi wa dini mnao waumini wengi tumieni fursa hiyo kuwaelimisha waumini wenu umuhimu wa kuhesabiwa,’’ ilieleza hotuba ya Waziri Mkuu.

Alisema, zoezi la sensa ya watu na makazi ni muhimu kwa kuwa linaipatia nchi takwimu za msingi zinazotumika kutunga sera, kupanga mipango na program za maendeleo pamoja na kufuatilia utekelezaji wake.

Kupitia hotuba hiyo, Dkt.Mabula alieleza kuwa, takwimu rasmi zitawezesha serikali na wadau wengine kufuatilia na kutathmini malengo yaliyofikiwa katika kutekeleza mipango ya maendeleo iliyokusudiwa sambamba na changamoto mbalimbali zitakazojitokeza katika sekta zote na hatimaye kuweka malengo na mikakati ya kukuza uchumi pamoja na kupunguza umasikini miongoni mwa watanzania.

Kwa upande wake Askofu wa Jimbo Katoliki Geita, Mhashamu Baba Askofu Flavian Kasala ambaye ni Padre wa kwanza wa Parokia hiyo ya Bikira Maria wa Fatima tangu kuanzishwa kwake alisema, viongozi wa dni wataendelea kuiunga mkono serikali katika suala zima la sensa ya watu na makazi kwa kuwa suala hilo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.

‘’Sisi tutaendelea kuinga mkono serikali na uwepo tofauti ndogo ndogo ndizo zimewapeleka baadhi ya watu kwenye matatizo makubwa na tusiruhusu jambo hilo linaloweza kututofautisha kwenye imani zetu za kidini,’’alisema Askofu Flavian Kasala.

Askofu Ouma

Wakati huo huo, Askofu Mkuu wa Kanisa la New Life Gospel Community Church-Tanzania (Bonde la Baraka) nchini lenye makao makuu yake Kigera Bondeni Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara, Daniel Ouma amewataka Watanzania wajitokeze kushiriki kikamifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ili kuiwezesha Serikali kupanga mipango ya maendeleo.

Askofu Ouma amesema kuwa, zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi na wananchi wote. Hivyo amesisitiza Watanzania washiriki kikamilifu katika zoezi hilo muhimu. Huku akisema viongozi wa dini zote washiriki kuhamasisha jambo hilo ili lifanikiwe kwa ufanisi.

"Niwaase Watanzania wote, tushiriki kwa kwa ufanisi, sensa ya mwaka huu itakuwa ya sita kufanyika baada ya Tanganyika na Zanzibar kuungana. Hakuna sababu ya mtu kuzuia watu wasihesabiwe, bali tuhimize watu wahesabiwe. Sensa hata makanisa zinafanyika wachungaji wanahesabu idadi ya mahudhurio ya washirika, nakazia lazima zoezi hili lifanyike vizuri sana bila kukwamishwa.

"Sensa ina faida kubwa sana kwa nchi, Serikali itatambua hali za maendeleo ya wananchi, hali ya ajira, hali ya utoaji wa huduma za jamii, kupata takwimu sahihi na mambo mengine mengi ya muhimu kila kitu cha thamani kinahesabiwa na ndio maana fedha zinahesabiwa sembuse na binadamu ambaye thamani yake ni kubwa kuliko chochote,"amesema Askofu Ouma.

Ameendelea kufafanua kuwa, "Zipo sababu za Sensa, kwani kila nambari ina thamani kubwa kwa Mungu, kuhesabu kunapatikana katika Biblia, tunasoma Yesu alilisha watu 5,000 hiyo tayari ni hesabu, mjane alihesabu sarafu, na katika Biblia kuna kitabu kinachoitwa Hesabu kwa hiyo wanaopotosha Sensa waache na wapuuzwe kwani nia yao si nzuri.

"Na katika michezo tunaona takwimu hutolewa zikionesha idadi ya mashuti yaliyolenga lango, umililiki wa mpira, idadi ya kona zilizochezwa, hizo zote ni hesabu. Na ndio maana Taifa lina mipango yake ya maendeleo,"amesema Askofu Ouma.

Waumini EAGT

Dkt.Brown Abel Mwakipesile ambaye ni Askofu Mkuu wa Kanisa la EAGT nchini naye anatoa wito kwa waumini wa kanisa hilo na Watanzania wote kujitokeza kuhesabiwa katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi.

Askofu Dkt.Mwakipesile amesema ni jukumu la kila muumini kuwa kielelezo kizuri katika jamii kwa kuwa tayari na kuonesha ushirikiano kwa makarani wa sensa ili kufanikisha zoezi hilo.

“Kila aliyeokoka awe mfano kwenda kuhesabiwa, popote alipo mwana EAGT ahakikishe anakuwa mstari wa mbele kushiriki zoezi la sensa,”amesema Dkt.Mwakipesile.

Ameongezea kuwa, sensa ni jambo muhimu kwa kuzingatia idadi ya watu inahitajika kila eneo ikiwemo katika kanisa ili kufanishi mipango ya maendeleo.

Mashehe

Kwa upande wao viongozi wa dini ya Kiislamu nchini wametakiwa kuwahimiza waumini wa dini hiyo kujiandaa kuhesabiwa kwenye Sensa ya Watu na Makazi.

Sheikh wa Mkoa Mwanza, Hassan Kabeke anasema, zoezi hilo ni muhimu kwa mustakabali mwema wa Taifa na dini hiyo kwa ujumla katika kupanga mipango ya maendeleo na kuitekekeza kikamilifu.

Amesema, viongozi wa dini wakiwemo maimamu na wakuu wa taasisi za dini ya kiislamu wanao wajibu wa kuwaelimisha waumini wao kuhusu umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi ambapo pia Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Abubakar Zubeir akiwa ziarani mkoani Kagera hivi karibuni aliwaelekeza mashehe wote wa mikoa nchini kuhakikisha elimu hiyo inatolewa kwa waumini.

"Sisi Baraza Kuu la Waisilamu wa Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza kwa ushirikiano wa pamoja na viongozi wote tumepokea maagizo ya Mufti na tumeanza kuyatekeleza kwa kutoa mwongozo wa namna ya kufikisha elimu ya Sensa kwa waumini kupitia nyumba zetu za ibada," alisema Sheikh Kabeke.

Sheikh Kabeke alisema waumini wa dini ya kiislamu na wananchi kwa ujumla wanapaswa kuhesabiwa kwenye zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ili kupata takwimu sahihi zitakazosaidia Serikali kupanga mipango ya maendeleo kwa ufanisi.

ITAENDELEA

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news