MFAHAMU STEPHEN WASSIRA:Kiongozi msomi na mkongwe aliyeitumikia Tanzania kwa muda mrefu

NA CHARLES REGASIAN 

MHESHIMIWA Stephen Wassira, alizaliwa mwaka 1945 Wilaya ya Bunda mkoani Mara, na katika maisha yake ya siasa ameshika nyadhifa mbalimbali serikalini. 

Kutoka mwaka 1970 hadi 1975 alikuwa Mbunge wa Jimbo la Mwibara akiwa na miaka 25 tu,ambapo akiwa katika nafasi hiyo ya Ubunge aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Kilimo kati ya mwaka 1872 hadi mwaka 1975.
Mwalimu Nyerere alimteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara mwaka 1975 hadi mwaka 1982 na baadae mwaka 1982 hadi 1985 aliteuliwa kuwa ofisa mwandamizi kwenye Ubalozi wa Tanzania jijini Washington DC, Marekani.

Mwaka 1985 hadi mwaka 1990, alichaguliwa kuwa Mbunge wa jimbo la Bunda mkoani Mara, ambapo katika kipindi hicho aliteuliwa kushika wadhifa wa Naibu Waziri wa Serikali za mitaa, na mwaka 1989 hadi 1990 aliteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo.

Waziri wa Maji toka Januari 2006 hadi Oktoba 2006, Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Oktoba 2006 hadi Februari 2008, Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu toka Februari 2008 hadi Mei 2008 na Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Mei 2008 hadi Novemba 2014.

Amewahi kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo 1972 hadi 1975 chini ya Rais Julius Nyerere,Naibu Waziri Serikali za Mitaa 1987 hadi 1989 chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi. Pia amekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara 1975 hadi 1982 na Mkuu wa Mkoa wa Pwani 1990 hadi mwaka 1991.

Mwaka 1992 alishiriki kuasisi chama cha CHADEMA na kuhamia NCCR-Mageuzi huko ni baada ya Wassira kukatwa jina lake kwenye kura za maoni, akiwakilisha Jimbo la Bunda kabla ya matokeo ya uchaguzi huo kubatilishwa.

Kwenye uchaguzi huo ambao alimshinda ndugu Joseph Sinde Warioba wa CCM katika uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi wa Tanzania mwaka 1995, ushindi wake huo haukudumu kwa muda mrefu mara baada Warioba kukimbilia mahakamani na ushindi huo kubatilishwa na Mahakama mwaka 1996 kwa tuhuma mbalimbali za ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi.

Mwaka 2005 aligombea tena Ubunge jimbo la Bunda na kufanikiwa kushinda, baada ya kushinda Ubunge mwaka 2005,Januari 2006 aliteuliwa kuwa Waziri wa Maji, Oktoba 2006 hadi Februari 2008 aliteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo,Chakula na Ushirika.

Februari 2008 hadi Mei 2008 alichaguliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri wa Mkuu ( Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) ambapo mwaka 2008 hadi 2010 aliteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.

Novemba 2010,aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), ndani ya CCM ni mjumbe wa NEC miongoni mwa wajumbe 370 ambacho ni chombo cha juu cha maamuzi kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho. amekuwa mjumbe wa NEC tangu mwaka 2007 ambapo pia alichaguliwa kuwa mjumbe kwa miaka mitano kabla ya hapo, mwaka 2011 alichaguliwa kuwa mjumbe wa kamati kuu inayoundwa na wajumbe 28 akiwemo Mzee Jakaya Kikwete.

Wassira ana historia ndefu katika siasa za Tanzania,kwa sasa anatajwa kuwa miongoni mwa wanasiasa ambao walikubalika ndani ya chama chake kutokana na sababu mbalimbali,jambo ambalo limethibitika bila kuwapo shaka yoyote ile kutokana na matokeo ya chaguzi hizo muhimu kwa mustakabali wa siasa za Tanzania.

Kada huyu ni miongoni mwa makada wasio na kashfa kwa kutokuwa na kashfa na ufisadi au matumizi mabaya ya madaraka,Wassira alijikuta akiwa mwenye kujiamini hasa linapokuja suala la kuomba kura mbele ya wenzake wa chama chao. 

Ni miongoni mwa wanasiasa ambao walibahatika kufanya kazi chini ya Serikali ya Awamu ya Kwanza ,iliyokuwa ikiongozwa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.

Katika Serikali ya Awamu ya Kwanza,Wassira alifanya kazi kama Naibu Waziri, Mkuu wa Mkoa na baadae alipelekwa katika ubalozi wa Tanzania nchini Marekani, nafasi ambazo zilimfanya ajifunze mengi na kupata uzoefu wa uongozi na maadili kutoka kwa Baba wa taifa Julius Nyerere kutokana na ukaribu wao kiutendaji.

Tofauti nyingine aliyokuwanayo ndani ya chama tawala ambayo kwake ni turufu kubwa ya mafanikio ,ni kutokuwa na makundi ya kisiasa, makundi ambayo yamegeuka na kuwa mwiba mchungu kwa wakongwe wengine wa siasa, hilo liliwahi kupelekea Rais awamu ya nne Jakaya Kikwete kumteua baada ya kuunda Wizara mpya chini ya Ofisi yake kwa ajili ya kuratibu na kusimamia mahusiano ya makundi mbalimbali ya kijamii yakiwamo ya kidini na kisiasa.

Wassira ambaye ni mhitimu wa shahada ya uchumi (BA in Economics ) Chuo Kikuu cha Washington DC, Marekani, Shahada ya Sayansi ya Siasa ( Chuo Kikuu cha Washington DC, Marekani,) na Shahada ya Uzamili katika Utawala ( Masters in Public Administration) kutoka Chuo Kikuu cha Washington DC, Marekani.

Ameshika madaraka katika awamu zote tatu za utawala wa Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia wakati wa Rais Julius Nyerere, Rais Ali Hassan Mwinyi na Rais Jakaya Kikwete.

Jina la Tyson lilianza kutumika rasmi mwaka 1996 hasa baada ya mpambano wa wanamasumbwi Mike Tyson na Bruce Seldon, mpambano ambao Mike Tyson alimshinda kwa TKO Bondia nguli Bruce Seldon,utani ukaanza hapo na kumfananisha Wassira na Tyson kwa kumshinda mwanasiasa nguli ndugu Joseph Sinde Warioba aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais.

Minong'ono mingine iliibuka na kusema kuwa, eti, aliwahi kumpiga masumbwi mwandishi wa habari fulani hivi, kwamba toka hapo akapewa jina hilo la Tyson ambalo hakupendelea aitwe na mtu mwingine zaidi ya Rais Jakaya Kikwete.

Pamoja na hayo, aliyekuwa muasisi wa chama cha CHADEMA Wakili msomi George Bokore Masato Wassira ni kaka yake na Wakili Msomi aliyetokea Loyola Esther Wassira ni ndugu yake pia.

Miaka ya karibuni Wassira alikuja kushindwa kwenye uchaguzi jimbo la Bunda Mjini na mgombea kutoka CHADEMA Esther Bulaya ambaye alikuwa CCM na baadaye kutimkia CHADEMA. Baada ya matokeo kutangazwa Wassira alibwagwa chini na Bulaya, akakata rufaa, na ndipo zikaanza sarakasi za Mahakamani ambako Wassira alishtaki na kushindwa tena.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news