Mheshimiwa Mene kufungua Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara (DITF) leo

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amesema, Katibu Mtendaji wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AFCFTA), Mheshimiwa Wamkele Mene anatarajiwa kufungua Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara (DITF) leo Julai 3,2022 katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Waziri amebainisha hayo Julai 2, 2022 jijini Dar es Salaam alipotembelea katika viwanja vya maonesho hayo maarufu kama Sabasaba yaliyoanza Juni 28 hadi Julai 13, 2022 na kutembelea majengo ya taasisi na kampuni mbalimbali zilizoshiriki maonesho hayo. 
Akiongea na vyombo vya habari, Waziri Kijaji amesema Septemba mwaka jana Bunge lilipitisha Mkataba wa Eneo Huru la Biashara, Afrika na Januari mwaka huu lilipelekewa taarifa ya kuonesha utayari wa Tanzania kuingia katika eneo hilo la biashara.

"Kawaida wananchi walizoea maonesho yanazinduliwa na kiongozi wa nchi lakini mwaka huu itakuwa ni tofauti, Rais wetu Samia Suluhu Hassan alitoa fursa kwa sisi Watanzania kumkaribisha Katibu Mtendaji huyu na haya ni matokeo ya sisi kuingia huko katika ushirikiano,"amesema Dkt.Kijaji.
Aidha, Waziri Kijaji amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi katika ufunguzi wa maonesho hayo ambayo kwa kipindi hiki yameweza kuboreshwa kwa kiasi kikubwa na kuweza kuvutia wageni wengi kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi ya Tanzania.

"Tujitokeze kwa wingi kuja kumsikiliza mgeni wetu rasmi ambaye atatueleza fursa mbalimbali zilizopo katika soko hilo ili tuweze kuzitumia kikamilifu," aliongeza.

Hata hivyo Waziri Kijaji amewataka wafanyabiashara kuanza kuzalisha bidhaa zenye bora kwa ajili ya soko la Afrika na sio Tanzania pekee ili kuweza kujitangaza kwa nchi mbalimbali na duniani kote.

"Tunakoelekea ni kwamba Afrika inataka kuwa soko huru ambapo biashara zitatoka nchi moja kwenda nyingine bila vikwazo vyovyote. Tulichokubaliana katika Mkataba huo ni kwamba kila nchi iangalie sifa zipi za kipekee ambazo zikiweza kuchukuliwa na kutumiwa vizuri ndani ya Taifa hilo tunaweza kuzalisha kwa gharama nafuu na kuweza kuuza bidhaa zetu nje ya nchi,"ameeleza Dkt.Kijaji.
Aidha, Waziri Kijaji alifafanua kuwa wawekezaji wengi wanakuja nchini kwetu na hata Katibu Mtendaji huyu anakuja kuwaambia Watanzania Afrika tunakwenda kuwa soko moja, bidhaa zinazozalishwa Tanzania ziuzwe Afrika nzima.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news