Tanzania, Cuba zaangazia uwekezaji kwa maslahi mapana

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe Dkt.Ashatu Kijaji (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba, Mhe. Bruno Rodriguez Parrilla kuhusu uwezekano wa kupanua zaidi kiwanda cha kuzalisha viwatilifu ili kuzalisha bidhaa ya mbolea pamoja na bidhaa zingine za afya.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri Kijaji amesema moja ya bidhaa ambayo wanataka kuzalisha kwennye kiwanda cha Labiofam kilichopo Kibaha mkoani Pwani ni mbolea ambayo itakayowezesha kuwa na utoshelevu wa mbolea ndani ya Taifa letu.
"Kilimo ni sekta ambayo inachangia kwa kiwango kikubwa kwenye uchumi wa Taifa letu hivyo mbolea ni moja ya ya malighafi muhimu kuhakikisha kilimo kinakuwa na mchango mkubwa kwenye uchhumi wa Taifa letu, sisi kama Wizara tuko tayari kuhakikisha kiwanda chetu kinaendelea na uuzalishaji wa bidhaa hizi muhimu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu,"amesema Waziri Kijaji.
Aidha, Waziri Kijaji amesema majadiliano kati ya Serikali ya Tanzania na Cuba yanatarajiwa kuanza hivi karibuni na timu za wataalamu kwa nchi zote mbili zimeundwa na zipo tayari kuanza majadiliano mara baada ya wataalamu kutoka cuba kuingia nchini kuanzia Julai 8 hadi 10, mwaka huu.
Naye, Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Mhe. Valentino Mlowola amesema manufaa ya ugeni kutoka nchini Cuba utasaidia kupanua ushirikiano kati ya nchi hizo hasa katika sekta ya afya, elimu, viwanda na kilimo ambazo zitaongeza ajira kutokana na uwekezaji utakaofanywa baina ya nchi hizo. 
"Uhusiano wetu na Cuba ni mzuri na unaendelea kuimarika siku hadi siku na tutaendelea kushirikiana kwenye sekta mbalimbali hususani kwenye sekta yya afya,Elimu pamoja na Viwanda,"amesema Balozi Mlowola.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news