Msemaji Mkuu wa Serikali agusia maboresho Bodi ya Ithibati

NA DIRAMAKINI

MKURUGENZI wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali,Gerson Msigwa amesema,Bodi ya Ithibati ni miongoni mwa baadhi ya maeneo yatakayojadiliwa kwenye mchakato mzima wa kupitia upya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari namba 12 ya mwaka 2016 ambayo ndio imeunda bodi hiyo.
Msigwa ameyasema hayo leo Julai 13, 2022 kando ya mkutano wa wadau wa maendeleo uliofanyika New Africa Hotel (Four Points by Sheraton Dar es Salaam) jijini Dar es Salaam ambapo umefunguliwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye.

"Bodi ya Ithibati nayo ni baadhi ya maeneo yatakayojadiliwa kwenye mchakato mzima na kupitia upya Sheria ya Huduma za Habari Namba 12 ya mwaka 2016 ambayo inaunda hiyo bodi ya ithibati. 

"Lakini ninachotaka kusema Serikali imeonesha dhamira ya kwamba sasa tunataka kwenda kupitia upya sheria na taratibu zote ambazo zimewekwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari namba 12 ya mwaka 2016 pamoja na sheria nyingine zitaangaliwa katika mchakato huo,"amesema Msigwa.

Awali, wahariri wa vyombo vya habari nchini, wameeleza kwamba, uundwaji wa Bodi ya Ithibati ya Habari huru utaweka mazingira ya usawa kati ya Serikali na vyombo vya habari nchini.

Wameeleza kuwa, iwapo bodi hiyo ya kitaaluma haitaingizwa mkono wa Serikali katika uundwaji wake, Serikali itapata sehemu ya kwenda kupeleka malalamiko yake pale itakapokwazwa na habari au mwanahabari.

Kauli hiyo ilikuja kufuatia maoni ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Dkt.Eliezer Feleshi aliyoyatoa Mei 13, 2022 alipokutana na wadau wa habari ofisini kwake bungeni, jijini Dodoma.

Mei 31, 2021, aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa (kabla tasnia ya Habari kuhamishiwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Tasnia ya Habari) alisema Serikali inaendelea na taratibu za kuanzisha bodi ya ithibati itayokuwa na jukumu la kutoa ithibati na vitambulisho kwa wanahabari wenye sifa.

Bashungwa, ambaye sasa ni Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (OR-TAMISEMI), alitoa kauli hiyo wakati akiwasilisha makadiro ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Wakizungumza Julai 12 jijini Dar es Salaam katika mkutano wa wadau wa habari, wahariri hao wamesema kuundwa kwa chombo hicho, kutakuwa mwarobaini wa malalamiko ya muda mrefu kutoka kwenye vyumba vya habari mbalimbali nchini. 

Neville Meena, Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) amesema, iwapo Serikali itaamua kuunda Bodi ya Ithibati ya Habari, basi bodi hiyo itakosa uhuru wa kufanya uamuzi pale malalamiko yatakapoihusu yenyewe (Serikali).

Amesema, ili kukwepa hilo na kutenda haki kwa vyombo vyote vya habari nchini, hakuna budi kwa Bodi ya Ithibati ya Habari kuundwa na kusimamiwa na wanataaluma wenyewe ambao ndio wanahabari.

“Bodi ya Ithibati ya Habari ikisimamiwa na Serikali, itakosa uhuru wa kuamua, hivyo inapaswa kuundwa na wanataaluma na kazi yake ni ya kitaaluma. Serikali ikiwa na malalamiko nayo inakwenda kulalamika kwenye bodi na wala haipaswi kutoa maelekezo,” ameeleza Meena.

Kwa upande wake, Mhariri wa Gazeti la Raia Mwema, Joseph Kulangwa alionyesha wasiwasi iwapo serikali itasimamia uundwaji wa bodi hiyo akisema, “serikali itataka wanaowaandika vizuri tu, ndio wahalalishwe kufanya kazi hiyo.”

Alisema, tasnia mbalimbali nchini zimeunda na kusimamia bodi zao wenyewe bila maelekezo ama kuingiliwa na Serikali, amehoji sababu za Serikali kupendekeza kuunda bodi hiyo badala ya kuwaacha wanataaluma wa habari kuunda na kusimamia bodi hiyo.

Naye Jimmy Charles, Mhariri wa Jarida la Tz & Beyond pia Panaroma alisema, iwapo Serikali itaunda bodi hiyo, itajihakikishia uhuru wa habari kutuama mikononi mwake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news