MWAUWASA yasaini mkataba wa Euro milioni mbili

NA MOHAMED SAIF 

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) imesaini mkataba wa Euro Milioni Mbili na Kampuni ya SEURECA Consulting Engineering ya Ufaransa itakayoshirikiana na Kampuni ya NETWAS ya Tanzania kufanya upembuzi yakinifu, usanifu na usimamizi wa ujenzi wa mradi wa miundombinu ya kupeleka maji maeneo ya Kusini mwa Jiji la Mwanza.
Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele (kulia) akisaini mkataba. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi MWAUWASA, Poas Kilangi.

Akizungumza wakati wa kusaini mkataba Jijini Mwanza hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele alisema mkataba huo ni hatua za awali za utekelezaji wa mradi wa kufikisha huduma ya maji kwenye maeneo ya Wilaya za Nyamagana, Misungwi na Magu. 

Kwa upande wa Wilaya ya Nyamagana Mhandisi Msenyele alitaja maeneo yatakayonufaika kuwa ni Buhongwa, Nyamazobe, Sahwa, Lwanhima, Fumagila, na Kishiri wakati kwa upande wa Wilaya ya Misungwi maeneo ya Usagara, Nyashishi, Nyang’homango, Kigogo Ferry, Bujingwa na Fella yatanufaika na kwa upande wa Wilaya ya Magu ni Kisesa, Bujora, Isangijo, Kanyama, Igekemaja na Ihayabuyaga. 
Mkurugenzi wa Kampuni ya NETWAS, Griphin Symphorian (kulia) akisaini mkataba. Kushoto ni Mhandisi Mshauri wa Kampuni ya SEURECA Afrika Mashariki, Christophe Lacarin. 
Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele (wa pili kushoto) akibadilishana mkataba na Mhandisi Mshauri wa Kampuni ya SEURECA Afrika Mashariki, Christophe Lacarin mara baada ya kusaini. 

Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele (wa pili kushoto) na Mhandisi Mshauri wa Kampuni ya SEURECA Afrika Mashariki, Christophe Lacarin mara baada ya kusaini mkataba.

Aidha, alifafanua kwamba mkataba huo umegawanyika katika sehemu mbili ya kwanza ikiwa ni kufanya upembuzi yakinifu, tathmini ya athari za mazingira na kijamii na usanifu na sehemu ya pili ni kumsimamia mkandarasi atakayetekeleza mradi huo. 

Mhandisi Msenyele amebainisha kuwa uhitaji wa huduma ya maji kwenye maeneo hayo ni mkubwa na kwamba wananchi wa maeneo hayo wanayo matarajio makubwa na mradi huo hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya maeneo hadi hivi sasa hayana mtandao wa majisafi. 

“Kuna uhitaji mkubwa wa huduma ya maji kwenye maeneo haya; ni matumaini yangu kwamba kutokana na uzoefu wenu mtafanya kazi kwa mujibu wa mkataba, wananchi wanahitaji maji, hawataki kutusikia tukizungumzia habari za michakato,” alisisitiza Mhandisi Msenyele. 
Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele (katikati) akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa kufanya upembuzi yakinifu, usanifu na usimamizi wa ujenzi wa mradi wa miundombinu ya kupeleka maji maeneo ya kusini mwa Jiji la Mwanza.

Amezihakikishia kuzipa ushirikiano wa karibu kampuni hizo na alizielekeza kuanza shughuli zake mara moja ili mapema mwaka 2023 shughuli za ujenzi wa mradi zianze ambazo alisema zitahusisha ujenzi wa vituo vinne vya kusukuma maji, ujenzi wa matenki manne ya ujazo tofauti ya kuhifadhia maji, uchimbaji wa mitaro na ulazaji wa bomba za kusambazia maji zenye urefu wa takriban kilomita 400. 

Kwa upande wake Mhandisi Mshauri wa SEURECA Afrika Mashariki, Christophe Lacarin ameihakikishia Serikali kuwa watakamilisha shughuli za mradi kwa wakati na kwa ubora mkubwa kulingana na uzoefu wa muda mrefu walionao kwenye shughuli za usanifu na usimamizi wa miradi. 

“Tunauhitaji huu mradi, tunaimani kwa ubora wa kazi zetu mradi huu utatuletea miradi mingine mingi na tumetekeleza miradi mingi maeneo mbalimbali duniani ambayo inaendelea kututengenezea mazingira ya kupata kazi,” alisema Lacarin. 

Naye Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi MWAUWASA, Poas Kilangi alisema mkataba huo ni wa miezi 44 na utekelezaji wake unapaswa kuanza ndani ya siku 28 kutoka siku ya utiaji saini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news