Rais Dkt.Mwinyi akagua ujenzi barabara ya Kijangwani-Birikau, atoa pongezi maalumu

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza Taasisi ya Milele kwa juhudi zake za kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Kijangwani hadi Birikau yenye urefu wa kilomita 4.3 inayojengwa kwa kiwango cha lami.

Katika maelezo yake Rais Dkt. Mwinyi alieleza kuwa, asasi zisizo za Kiserikali ziko nyingi lakini Taasisi ya Milele imekuwa na mchango mkubwa katika kuiunga mkono Serikali.

Amesema kuwa, taasisi hiyo imekuwa ikisaidia katika ujenzi wa skuli, nyumba, misikiti pamoja na miradi kadhaa ya maendeleo.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa, tayari ukamilishaji wa ujenzi wa barabara hiyo fedha zake zimeshatengwa kwenye bajeti ya mwaka huu.
Sambamba na hayo, Rais Dkt. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwapongeza wananchi wa maeneo hayo kwa hatua waliyoichukua ya kutotaka kulipwa fidia ya vipando vyao vilivyoathirika wakati wa ujenzi wa barabara hiyo.

Naye Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dkt. Khalid Salum Mohammed aliwaeleza wananchi kwamba katika mambo yaliyopangwa kufanywa kiswani Pemba ni pamoja na kujenga jengo jipya la abiria pamoja na njia ya kurukia na kutulia ndege na kuweza kutua ndege kubwa.

Aliongeza kuwa, Bandari ya Mkoani nayo itajengwa ili iweze kupokea meli za makontena hatua ambayo itapunguza gharama kwa wananchi pamoja na ujenzi wa barabara ya Chake Wete na Mkoani hadi Chake.
Afisa Mdhamini wa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi, Ibrahim Saleh Juma alitumia fursa hiyo kuipongeza Taasisi ya Ifraji Zanzibar Foundation pamoja na Milele kwa pamoja kwa wazo lao la kusaidia ujenzi wa barabara hiyo ambayo ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wanaishi katika maeneo hayo.

Mapema Rais Dkt. Mwinyi alikagua shughuli za wajasiriamali pamoja na kuwakabidhi wajasriamali bodaboda.

Katika maelezo yake Rais Dkt. Mwinyi alieleza hatua tano zilizochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha wajasiriamali wanasaidiwa ikiwa ni pamoja na kuwasaidia katika kuwapatia mtaji, soko, elimu, kuwajengea mazingira mazuri ya kufanya shughuli zao pamoja na zana za kufanyia kazi.

Rais Dkt. Mwinyi pia, aliweka jiwe la msingi katika Hospitali ya Wilaya ya Chake huko Ole ambako alieleza jinsi alivyoridhika na hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa hospitali hiyo.
Pia, Rais Dkt. Mwinyi alieleza haja kwa watendaji wa sekta ya umma kufanya kazi kwa bidii katika kutoa huduma bora kwa wananchi kwani tayari Serikali imeshawaongezea maslahi yao.

Sambamba na hayo, Rais Dkt. Mwinyi aliweka jiwe la msingi la skuli ya Sekondari Pujini na kueleza jinsi Serikali ilivyodhamiria kujenga skuli za ghorofa kama hizo ili kupunguza changamoto ya uhaba wa madarasa.

Alieleza azma ya serikali ya kujenga na kuzifanyia ukarabati skuli zote za zamani ili ziweze kukidhi kusaidia katika kuondoa changamoto katika sekta hiyo ya elimu.

Wakati huo huo, Rais Dkt. Mwinyi alitembelea mabwawa ya kufugia samaki huko Kibaridi Pujini na kuwaeleza wafugaji wa samaki kwamba serikali itachukua juhudi za makusudi katika kuhakikisha wanapatiwa vifaranga.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi alieleza hatua zitakazochukiliwa katika kuhakikisha vikundi vyote vinapatiwa mitaji na kuiagiza wizara husika kuwawekea mazingira maalum wafugaji hao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news