Rais Dkt.Mwinyi:Serikali imeamua kuwajengea mazingira bora wajasiriamali

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kwamba Serikali imeamua kuwajengea mazingira bora wajasiriamali ili waondokane na kuuza bidhaa zao pembezoni mwa barabara.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi alipokuwa akizungumza na Wananchi katika Uwanja wa Mpira wa Paje,mara baada ya kugawa vifaa mbali mbali vya Uvuvi,Mwani pamoja na Zawadi mbali mbali ambapo anakamilisha kutimiza Ahadi zake alizozitoa pamoja na kukagua miradi ya maendeleo akiwa katika ziara ya Wilaya ya Kusini Unguja. (Picha na Ikulu).

Mheshimiwa Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo huko Mtule mara baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa kituo cha wajasiriamali ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kutembelea miradi ya maendeleo hapa nchini.

Katika maelezo yake, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kwamba wakati umefika kwa Wajasiamali kufanya shughuli zao katika mazingira mazuri na yenye kuvutia.

Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, hatua hiyo ni katika utekelezaji wa ahadi zake alizokuwa akiwaahidi wajasiriamali wakati wa kampeni za uchaguzi na kwa vile wananchi hao wamempa ridhaa ndio maana ameamua kutekeleza ahadi yake hiyo.

Aliongeza kuwa, Serikali anayoiongoza imeamua kwa makusudi kuwawekea mazingira mazuri wajasiriamali wa Unguja na Pemba ambapo kazi za ujenzi wa vituo hivyo kwa upande wa Mkoa huoa Serikali imeamua kuwapa kikosi cha Zimamoto ambao wamezifanya vizuri.

Hivyo, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kukipongeza kikosi cha Zimamoto kwa kazi nzuri iliyofanya katika ujenzi wa mradi huo na kueleza kwamba ni mradi unaovutio kuliko ile yote aliyokwisha kuitembelea ambapo aliitaka Mikoa mengine kuchukua mfano wa ujenzi huo ambao unavutia.

Mapema mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika hospitali ya Wilaya ya Kusini Unguja iliyopo Kitogani, Rais Dkt. Mwinyi aliahidi kwamba Serikali kitaendelea kuwapatia kazi wakandarasi wa ndani wenye uwezo kutokana na kufanya kazi vizuri.

Rais Dkt. Mwinyi alimpongeza Mkandarasi wa Hospitali hiyo Kampuni ya Quality Building Contractors ya Zanzibar kwa kufanya kazi nzuri na yenye ubora huku akieleza lengo la Serikali la kuwapa wakandarasi wazalendo ujenzi wa miradi hiyo ni kwa ajili ya kuhakikisha fedha za UVIKO-19 zinatumika vizuri na zinawahudumia vyema wananchi.

Alisema kwamba timu za Madaktari kutoka mataifa mbali mbali duniani zitakwenda kutoa huduma katika hospitali hizo za Wilaya kwa ajili ya kuongeza nguvu pale zitakapoanza kutoa huduma.

Aliongeza kwamba tayari Serikali imeshatenga ajira 5600 zikiwemo za sekta ya afya na elimu na kueleza kwamba sekta ya afya ni sekta iliyopewa kipaumbele kikubwa.

Alieleza kwamba si wagonjwa wote watakaopelekewa katika hospitali ya Mnazi Mmoja badala yake wagonjwa wengi watatibiwa katika hospitali hizo za Wilaya na zile za Mkoa zinazoendelea kujengwa katika Wilaya na Mikoa yote nchi nzima.

Akieleza kuhusu huduma za maji katika Mkoa huo, Rais Dk. Mwinyi aliwahakikishia wananchi kwamba juhudi za makusudi zitachukuliwa katika kuhakikisha Serikali inawafikishia wananchi huduma hiyo ipasavyo.

Aidha, alieleza hatua zitakazochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha inawalipa fidia wananchi waliokuwa na vipando vyao katika maeneo hayo yaliyojengwa miradi hiyo ya maendeleo.

Naye Waziri wa Afya Nassor Ahmed Mazrui alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa juhudi zake kubwa anazozichukua katika kuimarisha sekta ya afya na kuwahakikishia wananchi kwamba mambo makubwa zaidi yanakuja katika sekta hiyo huku akiwapongeza wakandarasi wazalendo kwa kazi nzuri wanazozifanya.

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi aliungana na waumini wa Kiislamu katika sala ya Ijumaa huko katika Msikiti wa Ijumaa Bwejuu ambapo katika salamu zake mara baada ya sala hiyo aliwasisitiza wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa ya watu na makaazi linalotarajiwa kufanyika nchi nzima mwezi ujao.

Aliwaeleza waumini hao kwamba iwapo watahisabiwa Serikali itapata idadi ya watu na kuweza kupanga vyema mipango yake ya maendeleo.

Sambamba na hayo aliwanasihi waumini hao kuendelea kumuombea dua ili aweze kutekeleza vyema shughuli zake zikiwemo ahadi alizoziahidi kwa wananchi.

Mapema asubuhi, Rais Dk. Mwinyi alipokea taarifa ya utekelezaji ya Mkoa huo wa Kusini Unguja iliyowasilishwa na Mkuu wa Mkoa huo Rashid Hadid Rashid huko katika ofisi za Mkoa huo Tunguu, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusinin Unguja.

Katika taarifa hiyo, Mkuu wa Mkoa huo alieleza mafanikio, changamoto zilizokuwepo pamoja na hatua zinazochukuliwa katika kuzipatia ufumbuzi huku akieleza juhudi zilizochukuliwa na uongozi wa Mkoa huo katika kusimamia miradi ya maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news