Dkt.Ritta Kabati akoleza safari ya kurejesha tabasamu kwa watu wenye ulemavu Iringa

NA HUGHES DUGILO

MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa, Mhe. Dkt.Ritta Kabati amewaongoza mamia ya watu wenye ulemavu wa mkoa huo katika kongamano maalum lililolenga kupinga ukatili wa kijinsia pamoja na kutoa elimu ya sensa ili kuwajengea uelewa na kujitokeza kuhesabiwa katika zoezi la Sensa linalotarajiwa kufanyika Agosti 23, mwaka huu. 
Kongamano hilo lililohudhuriwa na mamia ya watu wenye ulemavu kutoka katika wilaya zote za mkoa wa Iringa lilianza kwa maandamano maalum yaliyoanzia katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo na kupokelewa na mgeni rasmi wa shughuli hiyo, Mkuu wa mkoa huo, Queen Sendiga katika Viwanja vya Garden vilivyopo Posta katikati ya Mji wa Iringa.

Akizungumza alipokuwa akitoa hotuba yake ya utangulizi alipokuwa akimkaribisha mgeni rasmi, Mhe.Kabati amesema kuwa, imekuwa ni ndoto na kiu yake ya muda mrefu pia imetokana na kushuhudia changamoto nyingi wanazokumbana nazo watu wa makundi maalum hususani wenye ulemavu, wazee, watoto, yatima na wanawake ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri a Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan za kupinga ukatili wa kijinsia. 
"Mheshimiwa mgeni rasmi kutokana na changamoto hizo nilianza kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha napunguza au kuondoa changamoto hizo kabisa. Baadhi ya hatua hizo ni pamoja na kupeleka maswali na hoja zinazohusu watu wenye ulemavu bungeni ili kutafuta ufumbuzi ikiwemo mabadiliko ya kisheria na sera mbalimbali kuendana na mazingira yao.

"Hatua nyingine niliamua kuanzisha kampeni maalum ya kusaidia vifaa saidizi ikiwemo fimbo, basikeli, mafuta na hata kuboresha miundombinu katika baadhi ya maeneo ili wasikutane na changamoto hiyo,"amesema Mhe. Kabati.
Aidha, ameongeza kuwa baada ya kuona hali ya uhitaji katika jamii ni kubwa, aliamua kuanzisha taasisi maalum ya kushughulikia changamoto zinazowakabili watu waliopo kwenye makundi maalum inayoitwa RITTA KABATI TRUST FUND, ambayo itajihusisha moja kwa moja kutafuta ufumbuzi wa changamoto za watu wenye mahitaji maalum kwa kuwafuata kwenye maeneo yao na kuwatambua ili kufanya uratibu wa kuwasaidia.

"Taasisi hii inalenga kukuza utu na heshima kwa watu wenye ulemavu na kutoa ushauri wa matibabu bila malipo kwa walemavu pamoja na kusaidia miradi na shughuli nyingine za kiuchumi zinazoendeshwa na watu wenye ulemavu," ameongeza Mhe.Kabati.
Aidha, amebainisha kuwa kazi nyingine ni kuanzisha na kudumisha vituo vya walemavu ili kusaidia jamii na kujihusisha katika michezo hususani ya watu wenye ulemavu kwa kuanzisha mashindano mbalimbali ya michezo na burudani katika Mkoa wa Iringa. 

Kazi nyingine ni pamoja na kusaidia programu na mipango inayolenga kuwaelimisha na kuwafahamisha wazazi na walezi wa watoto wenye ulemavu kuhusu changamoto mahususi zinazowakabili watoto wenye ulemavu na jinsi ya kuwatunza.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Queen Sendiga amempongeza Mbunge Kabati kwa hatua yake ya kusaidia watu wenye mahitaji maalum na kwamba kwa kufanya hivyo anaunga mkono jitihada za Serkali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kupiga vita unyanyasaji wa kijinsia na vitendo vya ukatili hasa kwa watoto na walemavu.

Sendiga amesema kuwa, takwimu zinaonesha kuwa mkoa huo unaongoza kwa ukatili wa kijinsia na kwamba jamii yote hususani wakazi wa mkoa huo wanapaswa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wadau mbalimbali katika kutokomeza vitendo hivyo kama anavyofanya Mbunge Kabati.

"Ni aibu sana na fedheha kwa mkoa wetu kuongoza katika vitendo vya ukatili wa kijinsia, tunapaswa kupiga vita kwa nguvu zetu zote na mtu akikutwa na hatia ya kuhusishwa na vitendo hivi anapaswa kuchukuliwa hatua kali hata kufungwa maisha," amsema Mkuu wa Mkoa huyo huku akionesha kukasirishwa na vitendo hivyo.

Katika hatua nyingine amezungumzia umuhimu wa watu wenye ulemavu kushiriki katika Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23, mwaka huu na kuhimiza kuhesabiwa kwa watu wenye ulemavu na kwamba zoezi hilo litaifanya Serikali kutambua idadi ya watu hao na hivyo kupata huduma kwa urahisi kutokana na mahitaji yao na maeneo walipo.
"Ndugu zangu naomba sana kuhamasisha wazazi na walezi kuhakikisha watu wote wenye ulemavu tulinao majumbani wanahesabiwa, usimfiche mtu mwenye ulemavu kwani kwa kufanya hivyo utaifanya Serikali kukosa idadi yao na hivyo kushindwa kuwafikia kuwapatia huduma zao wanazostahili,"amesisitiza RC Sendinga. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news