Unafiki,majungu ya madiwani Arusha yamchefua RC Mongela,akemea

NA MWANDISHI WETU

MKUU wa Mkoa wa Arusha, John Mongela amewataka madiwani wa Jiji la Arusha kuacha kutumika vibaya kisiasa na kwa kupandikizwa unafiki na majungu na mtu mmoja na kuacha kufanya kazi za maendeleo kwa ajili ya wananchi.

Mongela ameyasema hayo leo wakati akizungumza na madiwani wa Jiji la Arusha pamoja na wakuu wa idara wa jiji hilo katika kikao cha kujadili hoja za Mkaguzi Mkuu wa Serikali CAG.

RC Mongela amesema,jiji hilo lina kila aina ya vyanzo vya mapato ambavyo madiwani hao wangevitumia vyema wangeweza kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 50 kila mwaka wa fedha, lakini imekuwa tofauti na badala yake wamekuwa ni watu wa kutengenezeana majanga.

"Jiji la Arusha mnakusanya shilingi Bilioni 20.3 na hazitoshi hata kuwaendeleza nyie wenyewe, lakini mnapata ruzuku ya shilingi Bilioni 66, sasa hayo hamyaoni mmebaki kukalia majungu, kunafikiana na kushikiwa akili na baadhi yenu mnasahau kazi za wananchi wenu,"amesema Mongela.
"Nilisema Jiji likusanye shilingi Bilioni 43, lakini nilivyo safiri nikarudi nilikuta wamechakachua hadi Bilioni 33 ili waweze kutupiga hizo zingine, uwezo wa kukusanya hadi shilingi Bilioni 50 kwa mwaka uwezo upo cha ajabu mnashikiwa akili.

"Mjitafakari sana, maana milioni 200 mnataka kuuana maana nasikia kila mahali mnapiga tu sio mizani wala wapi, mkibadilika mtakusanya mapato mengi zaidi na itakuwa ni rahisi kwenu nyie kupanga fedha hizo zikaendeleze maeneo yapi ya kata zetu na wananchi waweze kunifuika,"amesisitiza Mongela.

Aidha, RC Mongela ameeleza wamezuia vibali vya kusafiri kwa madiwani hao kwa kipindi hiki cha sasa hadi miaka yao itakapokwisha ili waweze kufanya kazi za wananchi na halmashauri hiyo kuwa sawa kuondokana na harufu zote za ufisadi.

"Kwa sasa hatuwezi kupitisha kibali chochote cha kusafiri hadi miaka mitano hii iishe, mtazunguka humu ndani hadi mtachakaa.Kuna wakati ninaamua kuwaacha makusudi maana ninaamini nyie wote ni watu wazima kama mtakaa kwa kuburuzwa na mtu anatoka huko nyumbani kwake anakuja kuwashikia akili,"amesema RC Mongela.
"Juzi alinifata Mbunge, kuomba lile eneo la Kaloleni tuwajengee wamachinga nadhani Mbunge bado hajanielewa wala na mimi sijamuelewa kabisa maana hatuwezi kuweka machinga kila eneo kwa sasa, tujenge masoko ya maana na yenye hadhi na ndipo baadae tuwahamishe taratibu,"amesema.

Mongela alieleza kuwa, katika suala la maendeleo na ikishafika hatua kuna maslahi ya taifa hakuna tena kubembelezana maana kinacho takiwa ni maendeleo na kuwaonya watakao jifanya vinara na wakikukutwa hakuna atakaye wasaidia wote watamkimbia.

Mbali na kuwa mkali Mongela juu ya kukerwa na madudu yanayoendelea katika halmashauri hiyo ya Jiji la Arusha alimtahadharisha Kaimu Mkurugenzi wa Jiji hilo Agney Chitukulo kuwa makini na madiwani hao maana hawatabiriki na wanaweza kumtengenezea fitna wakati wowote.

"Nikuombe Mkurugenzi utusaidie katika safu ya utendaji, maana katika eneo jingine bovu ni kwa watendaji ili kuweza kufanya majukumu yao kwa weledi na kwa manufaa ya nchi na uwe makini sana na hawa madiwani hawachelewi kukuwekea maneno na kukutafutia balaa,"amesema Mongela.

Aidha, Mongela aliwataka madiwani hao kubadilika na kuacha majungu ili kuweza kukidhi hadhi ya watanzania na kukidhi hadhi ya Jiji na kuwa na maendeleo na kumtaka Meya wa Jiji hilo Maximilian Iraqe kuwa weka pamoja madiwani hao ili ifikie hatua ya kuwa pamoja kama madiwani.

"Miezi mitatu iliyopita mlianzisha ajenda ya kutoa Meya kisa mambo yenu ya ajabu ya kuchongeana na ndiyo maana nilisikiliza nikawa nasubilia nione mwisho wake maana kama ni uchaguzi ningepanga mimi ila pia ningefikilia namna nyingine ili kukata mzizi wa fitna na umbea wenu.

"Mstahiki meya na madiwani niwaombe tu muwe kitu kimoja mkubaliane na kwenye vikao vyenu muwe na maamuzi ya pamoja mkiendelea na haya mambo yenu kwa mamlaka niliyonayo na kulinda amani nitafungia vikao vyenu maana havina faida kwa wananchi na kama mkiendelea kutafutiana matatizo,"amesema Mongela. 

Pia RC Mongela hakuishia hapo aliwaonya vikali madiwani hao juu ya mgogoro wa eneo la Bondeni City ambalo wamekuwa vigeugeu kila kukicha na kuwataka kuacha tabia hiyo mara moja maana kwa kuzidi kuwa vigeugeU mradi huo wa ujenzi wa eneo la Bondeni City Unaweza kufa.

"Juzi mmekuja na jambo la Bondeni City isimame ili muanze kuchunguza upotevu wa hekari kadhaa na alivyokuja Waziri wa Ardhi nikatoa tamko langu mbele ya waziri na mbunge wenu kwamba mimi nimekuta suala la Bondeni City,"amesema Mongela.

Pia Mongela alieleza kwamba zimeshafika timu zaidi ya nne na jiji wakasaini mkataba wa kwanza na baadae wakaja kusaini mkataba wa pili na kutaka kulipwa asilimia 10 ya fedha na baada ya muda tena wakataka wagawane ardhi na akawambia wamesaini MOU na hadi Benki ya Dunia imeweka eneo hilo kwa ajili ya ujenzi wa stendi ya mabasi.

"Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, ameirudisha Arusha ile ya zamani hapa sasa tuna tarajia kupata watu maarufu kuja kufanya mkutano mkubwa wa CAF na tumepanga tuwaombe watujengee viwanja vya mpira kule Bondeni City, nyie bado hamjafikiria chochote juu ya hilo matokeo yake ni migogoro tu.

"Niwatake msilishwe matango pori badala yake kila mmoja aje na hoja ya maendeleo ya kata yake ila mkiendelea kulishwa maneno na kujifanya mnajua mtajikuta miaka hii mitano imekata na hauna cha kusema kwa wananchi.Kwa namna madiwani mnavyolipeleka hili suala la Bondeni City huo mradi unaweza kufa maana wafadhili hawawezi kupeleka fedha sehemu zenye migogoro na ndiyo maana nawaeleza ukweli msipojitafakari kwa kina ujenzi wa hiyo stendi mtauuwa wenyewe na wananchi watakosa stendi kwa maendeleo yao,"amesisitiza 

Aidha, Mkuu wa Mkoa huyo alitoa wito wa jumla kwa madiwani wote kuacha magenge uchwara ambayo hayatawavusha na maisha hayo hayana mwenyewe wakumbuke ubinadamu na maslahi ya taifa kwa ujumla wake.

"Niwaombe madiwani wote kuweni kitu kimoja na muongee lugha moja na hiyo itawasaidia sana niwaombe tu acheni mambo yasiyo na tija kwa jamii wala kusaidia jamii kaeni chini muwe na maamuzi kama viongozi na msitengenezeane matatizo. 

"Imefika hata sasa naangaika na mambo ya wilaya zingine wanaojielewa na kufanya maendeleo kwa wananchi siku nyie mkiacha majungu na maneno maneno mtakuja kuwakuta wenzenu wamepiga hatua zaidi ya maendeleo,"amesema RC Mongela. (Arusha Press Club)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news