Serikali yamaliza mgogoro wa Kanisa la EAGT

NA MWANDISHI WETU

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies Of God Tanzania (EAGT), Dkt.Abel Mwakipesile amesema, mgogoro uliodumu kwa takribani miaka sita umekwisha mara baada ya uongozi wa Msajili wa Jumuiya kutoa maelezo ya kuumaliza mgogoro huo kufuatia Serikali kufanya uchunguzi wa kina na kubaini kuwa tuhuma zote juu ya Viongozi Wakuu wa Kanisa la EAGT hazina msingi wowote na wala viongozi hao hawahusiki kabisa na tuhuma hizo walizokuwa wakituhumiwa nazo.
Ameyasema hayo Julai 16, 2022 alipokutana na waandishi wa habari katika ofisi za kanisa hilo jijini Dodoma na kueleza kuwa tayari Serikali imeshalifanyia kazi na kubaini kutokuwepo kwa uhalali wa tuhuma zilizokuwa zikiwakabili viongozi hao.

Akielezea chanzo cha mgogoro huo, Dkt.Mwakipesile alimtaja aliyekuwa Makamu Askofu Mkuu wa kanisa la EAGT, Askofu John Stephene Mahene ndiye aliyepelekea kuzuka kwa mgogoro huo kwa kupinga kuondolewa madarakani kwa sababu alikiuka miongozo ya imani ya kanisa hilo ambapo alidai kuondolewa kwa sababu za kuhoji ubadhirifu wa fedha na mali za kanisa uliofanywa na viongozi wa kanisa.

“Tumewaita leo kueleza mustakabali mzima wa mgogoro huo ambapo kutokana na maamuzi ya uongozi wa Msajili wa Jumuiya ulitoa barua yenye kumbukumbu Na.SA. 7183/PARTVI/50 ya tarehe 30Juni, 2022, barua ambayo ina maelezo ya kina sana jinsi Serikali ilivyofanya Uchunguzi wa kutosha na mwishowe ikabaini kwamba tuhuma zote walizotuhumiwa Viongozi Wakuu wa Kanisa la EAGT hazina msingi na wala Viongozi hao Wakuu hawahusiki kabisa na tuhuma zote,”alisisitiza Askofu Mwakipesile.

Aliongezea kuwa mara baada ya vyombo vya Serikali kufanya uchunguzi wake na kujiridhisha kwa kina hali hiyo ikiwa yeye ni Askofu imempa ujasiri kutangaza rasmi kumalizika kwa mgogoro huo pamoja na kutambua uongozi halali wa Kanisa la EAGT.

Askofu Dkt.Mwakipesile amesisitiza kuwa hatua hiyo imelisafisha Kanisa kufuatia mawazo potofu yaliyokuwa yanaenezwa kuwa kuna mgawanyiko uliopelekea kuwa na EAGT mbili.

“Maamuzi haya ya Serikali, kikao cha Baraza la Waangalizi wa Kanisa letu zuri la EAGT kilichokaa tarehe 12/07/2022 ambacho ndicho kikao chenye kauli ya mwisho ya kukata mashauri mbalimbali kuhusiana na Wachungaji. Toleo la 2011 Ibara ya XI- 4 kifungu kidogo (f) kilimshukuru Mungu sana pamoja na Serikali yetu kwa kutenda haki,”alieleza Mwakipesile.
Sambamba na hilo kikao hicho kilitoa maelekezo kwa kuwapa miezi mitatu kuanzia tarehe ya barua hiyo kwa Mchungaji yeyote atakayetaka kurejea baada ya mgogoro kumalizika, atapokelewa na ngazi husika kwa sharti la kuandika barua kwa Uongozi husika kwamba ametambua kosa lake na sasa anaomba msamaha na kwamba yuko tayari kutumika chini ya Uongozi halali wa Kanisa la EAGT. Mwisho wa kupokelewa ni tarehe 20 Octoba 2022; na baada ya tarehe hiyo mlango utakuwa umefungwa.

“Kwa wale ambao watataka kuondoka EAGT, Baraza la Waangalizi limetamka kwamba lazima waheshimu Katiba yetu ya EAGT ya toleo la 2011 Ibara ya IX ambayo inasema, “Mtumishi aachapo utumishi wake EAGT ataondoka pekee pasipo washirika wala mali za kanisa,”alisisitiza.

Aliongezea kuwa, Kanisa la EAGT litaendelea kudumisha amani ya nchi yetu kama ambavyo limekuwa likifanya siku zote.

“Kanisa la EAGT litaendelea kudumisha amani na utulivu katika kutekeleza majukumu yake kwa busara pamoja na hekima itokayo juu kwa maongozi ya Roho Mtakatifu kwani ndiyo msingi wa kanisa letu, huku tukihubiri habari njema ya watu kuacha dhambi na kumgeukia Kristo kusimamia utakatifu kwa bidii, Mungu awabariki,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Askofu Dkt.Mwakipesile ametoa wito kwa kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika tarehe 23 Agosti, 2022 ili kuisaidia Serikali katika mipango mbalimbali ya maendeleo kwa kujua idadi kamili ya watu wake.

Post a Comment

0 Comments