Serikali yatoa wiki moja ujenzi Bandari kavu ya Kwala

NA MWANDISHI WETU 

NAIBU Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete, ametoa wiki moja kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kukamilisha taratibu za ndani na kumlipa Mkandarasi wa Kampuni Estim Construction anayejenga barabara ya kiwango cha zege (km 15), kutoka Kwala hadi Vigwaza ili ikamilike kwa wakati. Zinazohusiana, soma Rais wa Burundi atembelea Bandari Kavu ya Kwala
Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa barabara ya Kwala hadi Ruvu (km 15.5), kwa kiwango cha zege, mkoani Pwani. (PICHA NA WUU). 

Naibu Waziri Mwakibete ametoa kauli hiyo baada ya kutembelea Bandari Kavu ya Kwala Mkoani Pwani na kushuhudia uchelewaji wa ujenzi wa barabara hiyo kutokana na malipo. 

“Urasimu wa kutoa fedha ni miongoni mwa sababu za kuchelewa kwa mradi huu hivyo nawapa siku saba kamilisheni taratibu zote zinazotakiwa na mumlipe mkandarasi huyu na Serikali inatarajia kupokea barabara hii mwishoni mwa mwaka,”amesisitiza Naibu Waziri Mwakibete. Zinazohusiana, soma Mwinjilisti Temba aibua hoja Bandari Kavu ya Kwala (Vigwaza)

Ameitaka TPA kuhakikisha wanakamilisha taratibu za manunuzi kwa ajili ya kumaliza ujenzi wa kumaliza eneo la Bandari Kavu kwani limechukua muda mrefu hali inayosababisha upungufu wa ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam na kutofikiwa kwa lengo la kupunguza msongamano. 

Kwa upande wake Meneja Miliki wa TPA Bw, Alexander Ndibalema amemhakikishia Naibu Waziri Mwakibete kuwa maelekezo yake yatafanyiwa kazi kwa haraka. 

Meneja Ndibalema amesema TPA imeshaunda kamati ya kupitia zabuni zilizoombwa na ndani ya muda mfupi zoezi hilo litahitimishwa na mradi huo kuendelea kutekelezwa. 
Mhandisi Mkazi kutoka Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Jacob Mambo akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete, kuhusu ujenzi wa barabara ya Kwala hadi Ruvu (km 15.5), ambayo ni sehemu ya mradi wa Ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala. Zinazohusiana, soma Mwinjilisti Temba ataja mambo matatu kuhusu Bandari Kavu Kwala

Naye Mhandisi Mkazi wa mradi huo kutoka Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Jacob Mambo, amemhakikishia Naibu Waziri Mwakibete kuwa ujenzi umefikia zaidi ya asilimia 60 na asilimia zilizobaki zitakamilika ndani ya miezi mitatu. 

Mradi wa ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala unagharimu zaidi ya shilingi bilioni 80 ambazo zinahusisha ujenzi wa Barabara ya kutoka Kwala hadi Ruvu KM 15.5, uendelezaji wa eneo la hekta 5, reli kilomita 1.3 na ujenzi wa uzio wa eneo hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news