TMDA yaonya matumizi ya dawa za kutolea mimba, kuongeza nguvu za kiume

NA DIRAMAKINI

WANANCHI wametakiwa kuacha kutumia mara moja dawa kiholela za kutolewa mimba na za kuongeza nguvu za kiume bila kufuata ushauri wa daktari ili kuepuka madhara mbalimbali ikiwemo kupoteza maisha.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA),Adam Fimbo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho Biashara ya Kimataifa ya 46 yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julias Nyerere jijini Dar es salaam 

Amesema, matumizi ya dawa hizo kiholela yanaweza kumsababishia mtu madhara mbalimbali ikiwemo kupoteza maisha.

"Utumiaji holela wa dawa ikiwemo hizi za kutoa mimba na kuongeza nguvu za kiume zimekuwa zikitumika ndivyo sivyo, ni muhimu mtu kabla ya kuanza kutumia kupata ushauri wa wataalamu juu ya namna sahihi na bora ya kuweza kutumia dawa,"amesema.

Amebainisha kuwa, TMDA imekuwa ikipata ripoti mbalimbali kuwa watu wamekuwa wanapoteza maisha wanapotumia dawa hizo za viagra.

"Tunatoa wito kwa jamii kama mtu akitaka kutumia dawa hizi ni muhimu apate ushauri kwa mtaalamu wa afya kwanza," amesema Fimbo

Aidha, amesema matumizi ya viagra nchini yamekuwa ni makubwa hivyo kwa sasa wanafanya utafiti kuangalia matumizi hayo yapo kwa kiwango gani ili kuweza kutoa elimu zaidi kwa wale wanaotumia isivyotakiwa.

Pia amesema dawa za kutoa mimba maarufu kama P2 nazo wameziwekea mkakati kwa lengo la kudhibiti uholela wa utumiaji wake ambapo imeonekana watoto wa shule wengi wanapenda kuzitumia kutolea mimba.

“Tumeweka mkakati wa kuhakikisha tunatoa elimu kwa watoto wetu wa kike na wanawake kuacha kutumia dawa hizi kiholela kwa sababu zinasababisha vifo visivyotarajiwa na kuelimisha jamii matumizi sahihi ya kutumia,” amesema.

Akizungumzia kuhusu udhibiti wa dawa bandia Fimbo amesema wameweka mifumo ya ukaguzi katika maeneo mbalimbali.

Amesema kuwa, dawa yeyote inayoingia nchini lazima ikaguliwe ili kuhakikiwa kama zipo amazo hazijasajiliwa na kuweza kuziongoa katika soko.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news