TPDC: Tunaendelea kuongeza upatikanaji wa gesi asilia nchini

NA DIRAMAKINI

SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC), limesema linaendelea kuongeza upatikanaji wa gesi asilia katika vyanzo mbalimbali ambavyo watafiti wapo kazini kutafuta nishati hiyo pamoja na mafuta.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba, Ofisa Uhusiano wa TPDC, Fransis Lupokela, amesema zipo taasisi mbili za serikali ambazo ni gereza la Mtwara na la Keko, shule nne pamoja na hoteli ya Serena zinatumia nishati hiyo ya gesi asilia.

“Shirika linaendelea kufanya tafiti mbalimbali za kuongeza upatikanaji wa gesi asilia majumbani na tayari Serikali imesharuhusu REA (Wakala wa Nishati Vijijini) kushirikiana na TPDC ili kuwezesha ujenzi wa miundombinu na upatikanaji wa nishati hiyo majumbani,”amesema. 

Amesema, ili kuhakikisha kwamba gesi asilia inafika maeneo ya mikoani tayari wamejipanga kusambaza kwa njia tatu ambazo zinaweza kufikisha gesi hiyo ikiwemo ya mabomba na usindikaji wa gesi katika maeneo husika.

Amesema kuwa, shirika hilo limefanikiwa kugundua gesi katika maeneo mbalimbali na linaendelea na shughuli za utafiti wa mafuta na gesi katika mkondo wa Juu, wa Kati na chini.

Lupokela amesema, katika mkondo wa juu shirika lina miradi ya kimkakati wa Eyasi ambao huko wanatafuta mafuta na gesi katika ziwa Eyasi, linalogusa mikoa ya Singida, Arusha, Tabora na Simiyu.

Amesema, kitalu hicho cha Eyasi, sofa zake za kijiolojia zinafanana na za kitalu cha Uganda na Kenya ambapo wamegundua mafuta hivyo hali hiyo inawapa hamasa kuwa watagundua mafuta na gesi katika maeneo hayo.

Amesema,katika Mradi wa Mnazi Bay Kaskazini (North) wanaendelea kufanya tafiti za kugundua gesi pamoja na mradi wa Songosongo (west) Magharibi.

Vilevile amesema, nchi mpaka sasa ina miundombinu mitatu ya gesi asilia ambayo ni Songas, Mkomazi National Park (MNP) ambao unaishia Mtwara na Miundombinu ya taifa ya gesi asilia ambao unamilikiwa na serikali kwa kiasi kikubwa.

“Zaidi ya asilimia asilimia 62 ya umeme unaozalishwa nchini ambao upo kwenye gridi ya taifa unazalishwa na gesi asilia, kwahiyo unaweza kuona kwamba kama gesi hii isingekuwepo hali ingekuaje, lakini imeiondolea mzigo serikali wa kutumia fedha za kigeni kuagiza mafuta nje ya nchi ili kuzalisha umeme,” amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news