Vijana tuendelee kumuunga mkono Rais Samia asema Kenani Kihongosi, aanika mafanikio

NA DIRAMAKINI

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Kenani Kihongosi amewataka vijana kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Ameyasema hayo alipokuwa anahutubia katika Mahafali ya UVCCM Seneti ya Dar es Salaam leo Julai 3, 2022. 

"Wajibu wetu mkubwa vijana ni kusimama na Serikali, kusimama na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kusimamia na Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan,matunda ya miradi hii ya kimkakati wanufaika wakubwa ni sisi vijana na watoto wetu kwa miaka mingi baadae,"amesema.
Kihongosi amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika Taifa letu ya kuhakikisha vijana wanapata ajira pamoja na kuendeleza miradi mikubwa ya kimakakati.
"Tunampongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyenkiti wetu wa Chama Cha Mapinduzi, ninyi wenyewe ni mashahidi miaka sita nyuma hapakua na ajira kwenye utumishi wa umma, lakini yeye ndani ya mwaka mmoja Mheshimiwa Rais ametoa ajira zaidi ya elfu 79, watumishi wa umma tunampongeza sana.
"Mhe. Rais Samia, ameendelea kufanya kazi kubwa, miradi ya kimkakati inaendelea ujenzi wa bwawa la kufua Umeme la Mwalimu Nyerere linalogharimu zaidi ya trilioni 6 ambalo litazalisha umeme Megawatt 2115, ujenzi umefikiaikia asilimia 62 kutoka asilimia 41 alipoupokea Mhe.Rais Samia.

"Tunao mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) hadi kufikia Aprili 2022, ujenzi wa Reli kipande cha Dar es Salaam-Morogoro (km 300) umefikia asilimia 96.54 na kipande cha Morogoro-Makutupora (km 422) umefikia asilimia 85.02 na tumeona treni ya majaribio ipo katika majaribio Kazi Inaendelea,"amesema Kihongosi. 

Pia Katibu Mkuu ameeleza kuwa, vijana wana kila sababu ya kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufuta ada kuanzia shule za msingi hadi sekondari, kwani kufutwa kwa ada kunaenda kuleta nafuu kubwa kwa familia nyingi Tanzania na kuhakikisha vijana wote wanapata elimu bora.
"Wengi tunajua adha ya kitu kinaitwa ada.Tunampongeza Mhe.Rais Samia kwa kufuta ada ya kidato cha Tano na cha Sita, jambo hili ni kubwa linakwenda kuwasaidia Watanzania walio wengi kupata elimu bora,"amesema.

Pia Katibu Mkuu UVCCM Taifa amewataka vijana kuhamasisha kuhusu Sensa na kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kuhesabiwa kwani Sensa ni msingi wa maendeleo katika Taifa.

"Vijana twendeni tukahamasishe Sensa na tukawaambie Sensa ndio msingi wa Maendeleo katika nchi yetu, bila kujua idadi ya watu Serikali haiwezi kufanya maendeleo yanayotakiwa, niwaombe sana tumuunge mkono Mhe Rais Samia na Serikali yetu kuhakikisha tunakuwa mabalozi wema wa kuhamasisha Sensa,"amesema Kihongosi.

Kuhusu kilimo, Katibu Mkuu ameeleza ni kwa kiasi gani Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anajua umuhimu wa kilimo katika Taifa letu, kwani uwekezaji wa fedha nyingi katika kilimo inaonesha maono yake makubwa aliyoyabeba kwa watanzania. 

"Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan,katika Sekta ya Kilimo ameongeza bajeti kutoka Bilioni 294 hadi Bilioni 900 haijawahi kutokea katika historia ya Taifa hili akitambua kuwa kilimo ndio uti wa mgongo wa Taifa letu, tumejionea maafisa ugani nchini nzima wamepewa vifaa mbalimbali ili kuiboresha Sekta ya Kilimo,"amesema.
Kihongosi amesema, kuna watu walidhani mambo yatakwama, lakini wamekwama wao maana kazi inaendelea na hakuna mradi hata mmoja uliosimama tangu Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani. 

"Kuna watu walidhani kuna mambo yatasimama, hatimae wamesimama wao Mama anaendelea kuupiga mwingi, wajibu wetu vijana ni kumuunga mkono Mhe.Rais Samia na kumsemea na kumwambia Mama Ulipo Tupo Kama Vijana,"amesema Kihongosi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news