Wakili Marenga ataja faida za sheria rafiki kwa vyombo vya habari

NA DIRAMAKINI

MAKAMU Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA-TAN), Wakili msomi wa kujitegemea James Marenga amesema,sheria rafiki kwa vyombo vya habari ni miongoni mwa nguzo muhimu ambayo itawawezesha wadau wote wa habari wakiwemo waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa kujiamini bila kukinzana na sheria kwa manufa ya Serikali na umma nchini.
Wakili Marenga ameyasema hayo Julai 20,2022 katika semina ya siku moja iliyoratibiwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kwa waandishi wa habari za mtandaoni iliyofanyika katika Hoteli ya Sapphire jijini Dar es Salaam.

Kupitia semina hiyo, Wakili huyo aliwapitisha wanahabari katika vifungu mbalimbali vya Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 vikiwemo vile ambavyo vinaonekana kuwa chanya kwa ustawi bora wa jamii na Taifa.

Sambamba na vifungu ambavyo wadau wanaona kuna haja ya Serikali kuvifanyia maboresho au kuvifuta kabisa kwa kuwa, vina changamoto ili kuiwezesha tasnia ya habari na wanahabari kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Amesema, kwa ujumla wake sheria hiyo imeweka baadhi ya maneno ambayo yanaweza kutumiwa vibaya na mahakama huku tafsiri ya maneno hayo ikiwa imefichwa.

Wakili Marenga ametaja baadhi ya maneno yenye mitego katika sheria hiyo kuwa ni pamoja na, ‘kwa namna nyingine’ ama ‘kusudio na kinyume cha sheria.’

“Neno kama ‘kwa namna nyingine ama kusudio na kinyume cha sheria,’ ni maneno hatari yanayotumika hasa kuharamisha jambo ambalo sio kosa kisheria. Maneno haya unaweza kuyaona kuwa ya kawaida, lakini ni hatari sana,” amesema Wakili Marenga.
Wakili Marenga amesema, kwenye sheria hiyo kuna adhabu zilizowekwa kwa makosa ambayo hayapo wazi kinyume na Ibara ya 13 (6)(C) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia amesema, sheria hiyo kupitia Kifungu 7 (i)(g) imevuruga uhuru wa faragha ambapo taarifa binafsi za mtu zinaweza kuchukuliwa na polisi kinyume na Ibara ya 16(i) ya Katiba ya Tanzania.

“Sheria hii katika Kifungu cha 50(2)(b) kinaondoa haki ya mtu kukata rufaa kinyume na Ibara ya 13(6)(a) ya Katiba, lakini pia Kifungu cha 38(2)(b) cha sheria hii kinaruhusu usikilizwaji wa shauri mahakamani hata bila muhusika kuwepo. 

“Hukumu ikitolewa, ndio unatafutwa na kufungwa bila kujua kesi yako ilipelekwa mahakamani lini, na kwa kosa gani. Ndio maana tunasema sheria hii inatakiwa kupitiwa upya,”amesema Wakili Marenga.
Wakili Marenga amesema, sheria hiyo inayohusu makosa yanayohusiana na mifumo ya kompyuta na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) iliwasilishwa Machi, 2015 bungeni kwa hati ya dharura na ilipitisha na Bunge tarehe Mosi Aprili, 2015 na kuidhiniswa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili 25, 2015. "Ni sheria ambazo zilikwenda kwa mfumo wa hati ya dharura tunasema certificate of agency,"amesema.

Sheria imetibu

Amesema, sheria hiyo licha ya mapungufu iliyo nayo inatibu mambo mbalimbali kwa ustawi bora wa jamii hususani kwa upande wa maadili, hivyo wadau wanaamini ikifanyiwa maboresho au vifungu vyenye mikinzano kufutwa huenda ikwa miongoni mwa sheria bora nchini

Maeneo chanya;-

-Kusimamia utoaji na ukusanyaji wa maudhui katika mtandao,

-Kudhibiti picha za ngono (wakubwa/watoto),

-Utoaji wa taarifa za uongo,

-Ujumbe unaotumwa bila ridhaa,

-Matusi ya kibaguzi,

-Unyanyasaji kupitia mtandao kula njjama ya kutenda kosa,

- Ukiukwaji wa haki bunifu;

Wakili Marenga amesema kuwa, miongoni mwa vifungu muhimu kwa ustawi bora wa jamii na Taifa katika sheria hiyo ni 39-49 ambavyo vinazungumzia kuhusu usimamizi wa maudhui ya mitandao.

"Sheria imekuja kutibu baadhi ya hayo mambo, sheria hii jambo muhimu ambalo inafanya ni kusimamia ukusanyaji wa maudhui katika mtandao. Hii ni sehemu muhimu sana ya sheria,ndio sababu ina control maudhui kuhusu nini kirushwe na nini kisirushwe na mambo mengine yanayohusina na Usalama wa Taifa.

"Kudhibiti na kupiga marufuku picha za ngono ambayo yamekuwa yakifanyika sana bila watu kujua kifungu cha 13-14 cha sheria hiyo ukisoma kinazungumzia hayo mambo na kuna watu ambao sheria hii tayari imewatafuna.

"Kwani sheria inasema hata kama ni wewe umerusha au umerushiwa sheria imeweka makatazo kwa sababu sheria imekuja na taratibu za wewe kuweka password (nywila) kwenye simu yako na kadhalika.

"Sheria haina excuses ya aina yoyote kwamba mimi sikuwa na taarifa au mtu mwingine nilimwachia simu yangu na hiyo simu yangu ndio ilionekana imerusha hivyo vitu, na hii inawagusa sana kinamama wamekuwa wakiaminiana kwenye haya masuala, lakini matokeo yake ni mabaya.

"Kudhibiti utoaji wa taarifa za uongo na hii ndio imekuwa vilevile sababu ya Serikali kuja na hii sheria moja kwa moja, kwa haraka. Ni kweli kwamba watu walipata taarifa za uongo, na taarifa za uongo zinatokana na nini? yawezekana mtu anayezitoa sio professional, hajui kama anachotoa ni uongo au ni ukweli.

"Tukio kwa mfano limetokea mahali fulani ninyi waandishi wa habari mmefundishwa matukio haya kwa mfano ajali mtu anayetakiwa kusema ni msemaji wa Polisi wa eneo husika, lakini ilikuwa kwamba watu wakipata taarifa kama zile wanazirusha na kutoa taarifa ambazo haziaminiki na sio sahihi.

"Lakini matukio ya mauaji maeneo fulani fulani watu wengine walikuwa wakitoa taarifa na kuwataja hata watu wa matukio hayo yawezekana hata mtu aliyefanya hilo tukio sio yule unayemsema wewe na kesi ya mauaji ni kesi sensitive sana, lakini kama umesharusha kwenye mtandao mara moja watu wana tendecy ya kuamini taarifa ya awali.

"Halafu yule mtu anaweza kudhurika, kuna watu wanaamini watu wanaorusha kwenye mitandao ni waandishi wa habari na ndugu zangu waandishi wa habari wanaaminika ni kweli ukirusha content kama hiyo...ni kweli kabisa hii sheria inasaidia kudhibiti utoaji wa taarifa za uongo soma kifungu cha 14 na 16 vya sheria vinasaidia katika eneo hilo.
"Lakini vilevile sheria hii inasaidia kudhibiti jumbe zinazotumwa bila ridhaa ya mpokeaji siku hizi tunaona jumbe zinaingia...zingine zinaelekeza mambo fulani fulani...na wewe baadaye unazirusha.

"Sheria hii inasema kupokea ni jambo moja na kushea ni jambo jingine ukiipokea na kuishea unaingia kwenye hatia kama mtu aliyekutumia, meseji ambazo hazifai ni za kuangalia sana unaweza ukapuuzia, lakini tatizo linapokukumba ni kubwa na pia kudhibiti matusi ya kibaguzi,"amesema Wakili Maranga wakati akiainisha baadhi ya maeneo chanya katika sheria hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news