'Watumishi vuteni subira'

NA DIRAMAKINI

SERIKALI imesema Jumanne Julai 26, 2022 itakutana na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) ili kuwasikiliza na kutoa ufafanuzi kuhusu nyongeza ya mishahara katika mishahara ya Julai, mwaka huu.
Hayo yamebainishwa leo Julai 24, 2022 na Msemaji Mkuu wa Serikali,Bw. Gerson Msigwa kupitia ukurasa wa Twitter wa Msemaji Mkuu wa Serikali.

“Ndugu wafanyakazi, Jumanne tarehe 26 Julai, 2022 Serikali itakutana na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) ili kuwasikiliza na kutoa ufafanuzi kuhusu nyongeza ya mishahara katika mishahara ya Julai, 2022,” amesema Msigwa.

Mei 14 mwaka huu Rais Samia Suluhu Hassan aliridhia mapendekezo ya kuongeza mishahara ikiwemo kima cha chini kwa watumishi wa umma kwa asilimia 23.3 ambayo yangeaza katika mshahara wa mwezi Julai.

Katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus ilisema mapendekezo hayo ni mwendelezo wa kikao cha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alichokifanya mkoani Dodoma na kupokea taarifa kutoka kwa wataalamu kuhusu ongezeko la mishahara.

Taarifa hiyo ilisema Serikali imepanga kutumia kiasi cha shilingi trilioni 9.7 katika mwaka wa fedha 2022/23 kwa ajili ya kugharamia malipo ya mishahara ya watumishi wote katika Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, taasisi na wakala za Serikali.

Post a Comment

0 Comments