Waziri Balozi Mulamula atoa wito kwa washirika wa maendeleo nchini

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula ametoa wito kwa washirika wa maendeleo nchini kuelekeza miradi na programu zao katika sehemu mbalimbali za nchi kulingana na mahitaji ya walengwa na vipaumbele vya taifa.
Mazungumzo baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Balozi wa Autria nchini Tanzania mwenye makazi yake jijini Nairobi, Kenya Mhe. Christian Fellner yakindelea.

Waziri Mulamula ametoa wito huo alipokuwa akifanya mazungumzo ya Balozi wa Austria nchini Tanzania Mhe. Christian Fellner mwenye makazi yake jijini Nairobi, Kenya. 

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika katika Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam, Waziri Mulamula ameeleza kuwa mara nyingi programu na miradi kutoka kwa washirikia wa maendeleo zinazolenga kuwawezesha wananchi katika shughuli za uzalishaji mali zimekuwa zikielekezwa upande mmoja wa nchi na kusahau maeneo mengine.

"Tanzania ni nchi kubwa na kila sehemu ya nchi ni muhimu na inamchango wake katika maendeleo ya Taifa letu kulingana na mazingira yanayowazunguka, hiyo ni vyema miradi na programu zinazoandaliwa na washirika wetu wa maendeleo zilenge kuwawezesha wananchi wa pande zote za nchi badala ya kuelekeza nguvu upande mmoja. Alipendekeza michango hiyo ielekezwe kupitia Serikali Kuu,"amesema Waziri Mulamula.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Balozi wa Autria nchini Tanzania Mhe. Christian Fellnermwenye makazi yake jijini Nairobi, Kenya yaliyofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Sambamba na hayo Waziri Mulamula amemshukuru Balozi Fellner kwa msaada wa vifaa tiba kutoka Serikali ya Austria wenye thamani ya Euro 50,000 uliokabidhiwa nchini jana tarehe 25 Julai 2022, na kupongeza mchango wa Serikali hiyo katika kuchangia maendeleo ya nchi kupitia programu mbalimbali wanazozifanya hapa nchini ikiwemo katika sekta ya afya, elimu, utalii, kilimo, usafirishaji na teknolojia.

Vilevile Waziri Mulamula amemweleza Balozi Fellner kuhusu utayari wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuendelea kushirikiana na Austria na hasa katika kipindi hiki ambacho Tanzania inaendelea kufungua na kuongeza maeneo ya ushirikiano na Dunia. Aliongeza kusema kuwa bado kuna fursa ya kuongeza maeneo ushirikiano hasa katika biashara, uwekezaji na utalii baina ya Tanzania na Austria.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (wa tatu kushoto) Balozi wa Autria nchini Tanzania Mhe. Christian Fellner (wa pili kushoto) Balozi Swaiba Mndeme Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na America (wa tatu kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na Maafisa kutoka Wizarani na Ubalozi wa Austria.

Kwa upande wake Balozi wa Austria nchini, Mhe. Christian Fellner ameeleza kuwa Austria itaendelea kushirikiana na Tanzania sambamba na kuongeza nguvu zaidi katika kusaidia sekta ya elimu, ikiwemo kuanzisha na kuendesha programu za kuwajengea uwezo Wanafunzi na Taasisi za Elimu wa kufanya utafiti wa masuala mbalimbali kwa maendeleo ya nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news