Waziri Mkenda:NMB kutoa bilioni 200/- kwa wanafunzi elimu ya juu

NA MATHIAS CANAL-WEST

WANAFUNZI wamepata ahueni baada ya Benki ya NMB katika mwaka wa fedha 2022/2023 kutenga Bilioni 200 kwa ajili ya kutoa mikopo yenye riba nafuu ya asilimia 9 kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu.
Mikopo hiyo itatolewa kwa wazazi na walezi ambao ni waajiriwa wa serikali na sekta binafsi au wafananyakazi wanaotaka kujiendeleza.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo tarehe 11 Julai 2022 wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Bi Ruth Zaipuna ofisini kwake Jijini Dar es salaam.

Waziri Mkenda amesema kuwa mikopo hiyo itasaidia kupunguza idadi ya waajiriwa wanaowaombea watoto wao mikopo kwenye Bodi ya mikopo ya Elimu ya juu (HESLB) na hivyo kutoa fursa kwa waombaji wenye uhitaji zaidi.
“Naipongeza Benki ya NMB kuwa mstari wa mbele kuinua sekta ya elimu nchini kwa kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na pia kutoa ufadhili kwa watoto wanaotoka kwenye familia zenye uhitaji,”amesema Waziri Mkenda.

Ameongeza kuwa, Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan inaendelea kutafuta vyanzo mbalimbali vya kugharamia elimu ya juu ili kuendana na mahitaji yanayotokana na ongezeko kubwa la uhitaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Bi Ruth Zaipuna amesema kuwa, hivi karibuni Benki hiyo ilizindua “Nuru Yangu Scholaship and Mentorship Program” kwa ajili ya kusaidia elimu nchini kwa lengo la kukata mnyororo wa umasikini na kuendeleza kizazi kijacho cha viongozi kwa kutumia njia ya kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na Elimu ya Juu.
Amesisitiza kuwa kupitia programu hiyo wanafunzi watalipiwa kila kitu ikiwemo ada, fedha za kujikimu, fedha za mafunzo kwa vitendo,bima ya afya, na kompyuta mpakato.

Bi.Zaipuna amesema kuwa utoaji wa mikopo hiyo ya Bilioni 200 ni utekelezaji wa ahadi waliyoitoa ambayo waliahidi kuanza mchakato wa kutoa mikopo yenye riba nafuu ya asilimia 9.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news