HILO NI JAMBO GUMU

NA ADELADIUS MAKWEGA

WAKATI fulani, pahala fulani, nilialikwa katika sherehe fulani, kama mwakilishi wa serikali fulani ambapo kulikuwa na mahafali ya shule fulani, inayomilikiwa na taasisi moja ya dini fulani huku shule hii ikifanya vizuri sana katika matokeo ya ngazi fulani.

Nilifika hapo kwanza palikuwa na kikao cha wazazi fulani, wenye watoto hapo hapo katika shule fulani. Kabla ya mahafali hayo hayaanza mjadali wa ajenda fulani ulifanyika.

Mojawapo ya ajenda fulani ilikuwa kuhusu tabia ya baadhi ya wazazi wa kiume kuwa na mahusiano yaliyovuka mipaka na binti zao wa kuwazaa.

“Baba anapotembea na binti yake anahatarisha hata kuimarika kwa familia yake, ndoa yake na tabia hii inaweza kusababisha mabinti wenye tabia hiyo kuwafundisha tabia mbaya mabinti wenzao hata hapa shuleni, tumebaini jambo hili lipo.”

Kiongozi huyu wa shule alisema kwa uchungu mno, huku ukumbi ukiwa kimya mithili ya hakimu anayesoma hukumu mahakamani.
Mimi nilikuwa nimekaa katika kiti changu kimya, nimetulia tuli nikiufuatilia mjadala huo kwa umakini mkubwa, kando ya kiti changu alikuwepo mama mmoja ambaye katika utambulishwa alitambulisha kama Martha Mangu akiwa mke wa Inspekta Jenerali wa Polisi (IJP) wakati huo.

Mwanakwetu hauwezi kukaa jirani na mke wa mkubwa kama huyu kama wewe ni mtu mdogo. Kumbuka mada hiyo inaendelea chini ya uongozi wa mwenyekiti wa Bodi ya Shule. Fahamu kuwa eneo hili llikuwa mkoa wa mbali Dar es Salaam na mke IJP anapokuwepo Jeshi la Polisi la linajua kuwa mke wa mkubwa wao yupo eneo hilo na kwa shughuli fulani.

Hapo hata ukizungumza neno na lolote na mama huyu lazima litajulikana, maana hauwezi juu walikando na mama huyu wanakufutilia-eh MWANAKWETU anasema nini? Mama huyu alipotambulisha tu nikachukua simu yangu nakuingia Google ili kuusoma wasifu wa Afande Mangu, nilibaini kuwa afande Mangu aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai. DCI yeye ndiye anaelekeza jambo hili lifanyike hivi au vile, hapo kuna jinai au hapa hakuna jinai. Huyu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai siyo mtu wa mchezo mchezo.

Msomaji wangu tambua kuwa mke wa mwalimu anakuwa na tabia za kiualimu, mke wa tabibu hivyo hivyo sasa hata mke wa afande na yeye ni hivyo. Sasa hali inakuwaje kwa mke wa DCI na mke wa IJP?

Kwa hakika na yeye siyo mtu wa mchezo mchezo, msomaji wangu kumbuka ajenda husika inaendelea. Kimoyo moyo nikasema hawa wazazi wenye tabia mbaya chamoto watakiona, maana Mama Mangu atalipeleka kama lilivyo kwa mumewe.

Mandhari ya tukio hilo ilipambwa na askari kadhaa wenye sare na mitutu begani kadhaa huku akilini mwangu nikitambua kuwa askari kanzu wapo.

Wakati ninateta na Mama Mangu, nikaisikia sauti kutoka katika spika kando ikinikaribisha kuzungumza na ukumbi huu uliojaa wazazi. Makofi yakawa yanasikika kwaaa, kwaaaa…kwa kando ndugu zangu wanahabari kadhaa wakiwa tayari kusikia ninasema nini juu ajenda hii?.

Nikausalimu umma huu na wao kuipokea salaam hiyo, nikawaomba wanahabari kuwa nawaombeni kwa hisani yenu, haya mtakayoyasema msiyanukuu.

Nikauliza watoto walioingia katika kadhia hii si mnawatambua? Jibu lilikuwa ndiyo, nikasema kwa kuwa jibu ni ndiyo waiteni wazazi wote wawili baba na mama, muwaeleze juu ya tabia hii mbaya inayofanywa na mzazi mwenzake, wajulisheni hata viongozi wao wa kiroho na serikali pahala walipo.

Washauriwe kama mazingira bado ni hatarishi mama wa binti husika achague sehemu husika binti yake akae sehemu salama katika kipindi hicho.(Kama vile bibi , shangazi au mama wadogo).

Tukio hili liliwakuta wengine kwa baba zao wa kuwazaa na wengine wazazi wa kambo. Niliwaambia kuwa wazazi hao walipe karo na huduma nyingine ili watoto wavuke salama katika kipindi hiki kigumu.

Tulikubaliana katika kikao hicho baadhi ya mabinti hao taasisi hii ya dini iliamua wabaki wakiishi shuleni kwa muda wote.

Huku vyombo vya serikali maeneno husika vikichukua hatua kali. Nilipomaliza kusema hayo niliwauliza wazazi au mnataka tumjulishe IJP sasa hivi ili alikamilishe zoezi hili? Ukumbini ilikuwa kimyaaaa, nilitoka katika marufaa na nikarudi katika kiti changu kilichokuwa jirani na Martha Mangu na kuketi.

Maazimio ya jambo hilo yote tuliyoweka yalifanyiwa kazi vizuri sana kwa ushirikiano wa wazazi wakiwemo wote, viongozi wa shule na mwanakwetu.

Lakini la kusikitisha mara baada ya mwezi mmoja IJP Mangu alichaguliwa kuwa Balozi, wa Tanzania nchini Rwanda na mama Martha Mangu sikukutana naye tena ninaambiwa wako Rwanda.

Mwanakwetu tambua anapochaguliwa mtu mpya katika nafasi yoyote ile kama mlikuwa mnalifanya jambo la manufaa ya umma na yule aliyeondoka, wewe ulibaki katika jambo hilo unatakiwa kwanza kuutafuta muda wa kumfuata umueleza jambo hilo kiongozi mpya, ukishaupa muda huo ufunge safari, alafu na hiyo nafasi yenyewe upewe, ukishapewa nafasi kiongozi mpya aliafiki jambo hilo, akishaliafiki ndipo lifanyike na lifanyike katika ubora ule ule nadhani HILO NI JAMBO GUMU.

Nimeumwa sikio kuwa mabinti wale wengine sasa wanamalizia shahada zao za utabibu huku wakiwasiliana kwa karibu na mkuu wa shule ile.

Popote alipo Balozi Afande Ernest Mangu nakusalimu sana na salaam hizi fikisha kwa mama Martha Mangu kwa maana nakumbuka mahafali yale, ya shule ile na ajenda ya wakati ule.

makwadeladius@gmail.com
0717649257
(Kutoka Kitabu cha Simulizi za Wakuda- adeladius makwega Mei 2017).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news