KWA HII SIKU YA SENSA, ASIWEPO WA KUKOSA

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)

IMBEBAKI siku moja kabla ya Watanzania kushiriki katika Sensa ya Watu na Makazi. Sensa ni zoezi la kitaifa linalofanyika kila baada ya miaka 10 ambapo Sensa ya mwisho kufanyika nchini ni ile ya mwaka 2012.
Hivyo Sensa ya mwaka huu ambayo itafanyika kesho Agosti 23, 2022 itakuwa ni sensa ya sita kufanyika nchini baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012.

Mshairi wa kisasa, Bw.Lwaga Mwambande anasema kuwa, Sensa ina nafasi kubwa katika maisha yetu ya kila siku na hata mipango ya Serikali ikiwemo ile ya wadau wa maendeleo, kwa kuwapa takwimu muhimu za idadi ya watu, kulingana na sifa za idadi ya watu, kijamii na kiuchumi.

Hali ya makazi na huduma za kaya ili kuweza kuandaa mwongozo wa namna ya kuweza kupanga mipango ya maendeleo endelevu na namna bora ya kugawa huduma kwa uwiano sahihi, hivyo anasisitiza kuwa, karani wa sensa anapofika nyumbani kila mmoja analo jukumu la kutoa taarifa sahihi,jifunze jambo kupitia shairi hapa chini;

1:Agosti shina tatu, imekwishatufikia,
Sensa makazi na watu, siku imeshatimia,
Tusikose hiyo katu, kotekote Tanzania,
Kwa hii siku ya sensa, asiwepo wa kukosa.

2:Twazihitaji takwimu, mipango kupangilia,
Idadi yetu muhimu, ile iliyotimia,
Kuhesabiwa ni zamu, sote tulo Tanzania,
Kwa hii siku ya sensa, asiwepo wa kukosa.

3:Tumetangaziwa sana, siku hii metimia,
Sensa ni muhimu sana, tusije kupuuzia,
Ikifanywa vema sana, mbele tutafurahia,
Kwa hii siku ya sensa, asiwepo wa kukosa.

4:Serikali imeona, kazi kutupunguzia,
Mapumziko twaona, kusiwe kusingizia,
Tusijivuruga tena, sensa ni kusubiria,
Kwa hii siku ya sensa, asiwepo wa kukosa.

5:Mimi nishajiandaa, karani nasubiria,
Majibu nimeyavaa, tayari kuwapatia,
Sana wasijekukaa, majibu kusubiria,
Kwa hii siku ya sensa, asiwepo wa kukosa.

6:Wenye shughuli za kwetu, sensa ni kusubiria,
Baadaye twende zetu, tukihesabiwa pia,
Huo uzalendo wetu, na afya kwa Tanzania,
Kwa hii siku ya sensa, asiwepo wa kukosa.

7:Rais wetu Samia, Sensa kasisitizia,
Makamu Rais pia, hili amekumbushia,
Sote tumewasikia, nyumbani twende tulia,
Kwa hii siku ya Sensa, asiwepo wa kukosa.

8:Rais wa Zanzibar, wengi tumemsikia,
Na tumepata habari, Waziri Mkuu pia,
Wito huo ni mzuri, takwimu kujipatia,
Kwa hii siku ya Sensa, asiwepo wa kukosa.

9:Serikali kwa jumla, wanatusisitizia,
Na dini hawajalala, umuhimu watwambia,
Kutoshiriki msala, tusijekujipatia,
Kwa hii siku ya Sensa, asiwepo wa kukosa.

10:Makarani wa tayari, nyumbani kutufikia,
Tuwasubirisubiri, yetu tukijifanyia,
Wakija toa habari, ziweze kuwafikia,
Kwa hii siku ya Sensa, asiwepo wa kukosa.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

0 Comments