LESENI ZIWE HALALI:Kuepuka watoaji na watumiaji wa huduma za kifedha zisizo halali

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)

MATAIFA mbalimbali duniani kupitia Benki Kuu yamekuwa na utaratibu maalumu wa kusimamia huduma za kifedha ili ziweze kutolewa kwa ufasaha,bila ulaghai au kuingia katika mikono ya watoaji na watumiaji wa huduma zisizo halali (black market).

Kwa upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imekuwa ikilisimamia hilo kuhakikisha kila mmoja aliyepewa leseni ya kutoa huduma za kifedha anakidhi vigezo na anawajibika kulingana na miongozo ya Serikali. Dhamira ikiwa ni kila mwananchi au mpokea huduma anapata huduma ambayo ni sahihi na kwa wakati.

Ndiyo maana, BoT imetoa uwanda mpana wa huduma za kifedha kuanzia mijini hadi vijijini iwe huduma za mikopo, kubadilisha fedha za kigeni ambazo zinatolewa na kupatikana katika benki na taasisi za fedha nchini kote, maduka pamoja na maduka ya fedha za kigeni ya Shirika la Posta Tanzania (TPC).

Mara kwa mara Benki Kuu ya Tanzania huwa inapenda kuutahadharisha umma kutotumia huduma zisizo rasmi za ubadilishaji wa fedha za kigeni kutokana na hatari mbalimbali, ikiwemo kuibiwa au kupewa fedha bandia.

Aidha, utumiaji wa huduma zisizo rasmi ni kinyume cha sheria za nchi. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watoaji na watumiaji wa huduma zisizo halali.

Mshairi wa kisasa, Bw.Lwaga Mwambande leo anapenda kukushirikisha jambo kuhusu huduma za kifedha huku msisitizo ukiwa ni huduma za hakika na leseni ziwe halali, endelea;

 

1:Hizi huduma za fedha, hebu kuwa mwangalifu,
Kama unakopa fedha, uhakikishe wasifu,
Hiyo taasisi fedha, leseni yake si mfu,
Leseni iwe halali, huduma za uhakika.

2:Kuna benki taasisi, ambazo zinasadifu,
Hizo zinayo nafasi, ndiyo twakutaarifu,
Kwa sababu ni halisi, na wala siyo hafifu,
Kwa huduma za hakika, leseni ziwe halali.

3:Unabadilisha pesa, yapo halali maduka,
Ukiwa na hizo pesa, benki zinawajibika,
Hakikisha hizo pesa, mashine zinatumika,
Kwa huduma za hakika, leseni ziwe halali.

4:Pesa unapobadili, za ndani na za kigeni,
Hiyo huduma halali, yapatikana nchini,
Hakiki kila mahali, risiti i mkononi,
Kwa huduma za hakika, leseni ziwe halali.

5:Biashara ya kutuma, hata kupokea pesa,
Ili iwe ni salama, na kuaminika hasa,
Zipo taasisi njema, zenye usajili hasa,
Kwa huduma za hakika, leseni ziwe halali.

6:Benki Kuu Tanzania, ndiyo hutoa leseni,
Taasisi kutumia, kwa kuhudumu nchini,
Na wewe hakiki pia, siingie msambweni,
Kwa huduma za hakika, leseni ziwe halali.

7:Kama unatuma pesa, au kupokea pesa,
Hizi simu za kisasa, mkononi imenasa,
Usijefanya makosa, ukaipoteza pesa,
Kwa huduma za hakika, leseni ziwe halali.

8:Vema ujue vizuri, jinsi ya kutuma pesa,
Tena pia uhariri, gharama kutuma pesa,
Kama vigumu subiri, ili usijekunasa,
Kwa huduma za hakika, leseni ziwe halali.

lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

Previous Post Next Post

International news