Meja Jenerali mstaafu Isamhuyo aiomba Serikali kufanya jambo kwa wakulima, wafugaji mkoani Mara

NA DIRAMAKINI

MEJA Jenerali mstaafu, Michael Isamhuyo ameiomba Serikali kutengeneza mazingira rafiki kwa wakulima na wafugaji mkoani Mara ili waweze kutumia fursa za kilimo na ufugaji zilizopo mkoani humo kuinua uchumi wa jamii,mkoa na taifa kwa ujumla.
Isamhuyo ameyasema hayo Agosti 8, 2022 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari shambani kwake kijijini Pida Wilaya ya Butiama ambapo amesema kuwa ili sekta hizo ziweze kuwa na tija upo umuhimu wa serikali kuingilia kati na kutatua changamoto zilizopo.

Amesema kuwa, licha ya sekta za kilimo na ufugaji kuwa na fursa nyingi za kiuchumi na kijamii, zipo changamoto nyingi ambazo bado zimekuwa ni kikwazo kwa wajasiriamali na wawekezaji kunufaika na fursa hizo.

Amezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na ukame, ukosefu wa mbegu bora, chakula cha mifugo pamoja na soko la mazao yao, changamoto ambazo amesema kuwa anaamini serikali ikiamua kuzifanyia kazi suluhisho litapatikana.

"Kilimo cha kutegemea mvua kimepitwa na wakati, mkoa wa Mara una vyanzo vingi vya maji serikali inatakiwa iangalie namna ya kujenga miundombinu ya umwagiliaji ili tutumie ardhi yetu yenye rutuba ambayo bado haijatumika ipasavyo ili kufanya mapinduzi kwenye mifugo na kilimo,"amesema.
Amesema kuwa, changamoto ya ukosefu wa masoko ya uhakika ya bidhaa zao pia inaweza kutatuliwa kwa ujenzi wa viwanda vidogo na vya kati hatua ambayo mbali na kuwapatia soko la uhakika, itasaidia kuwepo kwa mzunguko wa pesa na hivyo kuinua uchumi wa jamii kwa ujumla.

"Sio kwamba watu hawataki kufanya kilimo au ufugaji wa kisasa, lakini kumbuka kuwa ili ufanye mambo hayo unatakiwa kuwa na fedha sasa unawaza uwekeze pesa nyingi halafu hauna pa kupeleka mazao yako mfano mimi hapa kwa siku ninazalisha lita 80 za maziwa ambazo naishia kuuza tu hapa hapa kijijini,"amesema.

Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Kilimo na Viwanda ( TCCIA), Mkoa wa Mara, Boniface Ndengo amesema kuwa changamoto hizo ni miongoni wa sababu zilizopelekea chemba hiyo kuandaa Maonesho ya Biashara ya Kimataifa (Mara Business Expo) yanayotarajiwa kufanyika mjini Musoma kuanzia Septemba 2, mwaka huu.
 
Amesema kuwa, changamoto hizo zinahitaji ushrikiano wa pamoja kuzitatua ambapo ametoa wito kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Nchini (TADB) kuangalia namna ya kuwasiadia wawekezaji wadogo na wa kati mkoani Mara ili waweze kufanya shughuli zao kwa tija.

"Mkoa wa Mara ukiwezeshwa unaweza kutoa mchango mkubwa katika uchumi wa taifa hili kwasababu fursa zipo tena nyingi tu ambazo hazijatumika kwahiyo niiombe serikali itusadie,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news