Mjane wa Augustino Lyatonga Mrema aanza kupokea watoto wa nje

NA DIRAMAKINI

MJANE wa aliyekuwa Mwenyekiti wa TLP, hayati Augustino Lyatonga Mrema, Doreen Mrema amesema kuwa hadi sasa ameshapokea watoto wa hayati Mrema watatu ambao walikuwa hawajatambulika kwenye familia.
Bi.Doreen ameahidi ataendelea kuwapokea na kuwalea kama mama yao na yupo tayari kuendelea kuwapokea endapo tu ni kweli watakuwa ni watoto wa Mzee Mrema

Amesema hayo wakati akizungumza na vyombo vya habari Mjini Moshi mkoani Kilimanjaro ambapo pia ametoa shukrani kwa viongozi wa Serikali, vyama vya siasa na watu binafsi kwa kuwa nao kipindi chote cha msiba.

"Alinieleza nisiogope na niwapokee na niombe radhi kwenu, niwakumbatie na niwalee kama mama yao kama ambavyo yeye angewalea na ninamshukuru Mungu nimeendela kuwapokea watoto ambao walikuwa bado hawajatambulika kwenye familia na sasa nimeshapokea zaidi ya watoto watatu.

"Mimi kama mama nitaendelea kuwapokea na kuwakumbatia kama ambavyo mume wangu mpenzi alivyoniasa siku mbili kabla ya kifo chake,"amesema Doreen Mrema.

Aidha, amewahakikisa Watanzania kuwa ataendelea kumuenzi mume wake mpenzi, Mrema na kuishi vile alivyomuasa na muda sahihi wa kuzungumza ukifika ataeleza ukweli juu ya maneno yanayoongelewa katika mitandao ya kijamii.

"Muda sahihi ukifika nitasema ukweli wote,yapo maneno mengi yanayoongelewa na watu na mengine yameandikwa kwenye vyombo vya habari na mtandaoni,ila muda ukifika nitasema,siogopi na Mzee Mrema alisema nisiogope hata wakati hayupo,"amesema.

Post a Comment

0 Comments