Rais Dkt.Mwinyi ajumuika na mamia ya wananchi, viongozi katika maziko ya kaka yake

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi leo amejumuika na viongozi wa kitaifa, vyama vya kisiasa pamoja na mamia ya wananchi katika maziko ya kaka yake, Hassan Ali Mwinyi yaliofanyika Mangapwani Mkoa Kaskazini Unguja.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi akijumuika na wananchi na viongozi mbalimbali wa Serikali na Vyama vya Siasa katika sala ya jeneza ya marehemu Hassan Ali Hassan Mwinyi, kaka yake iliyofanyika kijijini kwao Mangapwani Wilaya ya Kaskazini “B” Unguja leo. Kulia kwa Rais ni Rais mstaafu wa Tanzania Alhaj Ali Hassan Mwinyi,Mbunge wa Jimbo la Mahonda Mhe. Abdalla Hassan Mwinyi na Spika wa Baraza la Wawakilishi Alhaj Zuberi Ali Maulid.(Picha na Ikulu).

Marehemu Hassan Ali Mwinyi (66) alifariki dunia jana usiku katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja jijini Zanzibar alikokuwa amelazwa kwa kipindi kirefu.
Maandalizi ya maziko ya marehemu Hassan yalifanyika nyumbani kwake Chukwani Mkoa Mjini Magharibi, ambapo wananchi, ndugu na jamaa pamoja na majirani walipata fursa ya kumswalia na baadae mwili wake kusafirishwa hadi Mangapwani, ambako aliswaliwa tena na hatimaye kuzikwa kwenye Shamba la Familia.
Akitoa nasaha baada ya kukamilika kwa hafla ya dua na sala, Mjumbe wa Maulamaa Mkoa Kaskazini Unguja, Sheikh Khamis Abdulhamid aliwataka waislamu kumuombea maghfira marehemu huyo, huku akiitaka familia kuwa na moyo wa subira.

Naye Balozi wa Tanzania nchini Saud Arabia, Ali Mwadini akiwasilisha salamu kwa Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dkt.Mwinyi pamoja na wanafamilia, kwa niaba ya mabalozi hao, alimuombea maghfira kwa Mwenyezi Mungu marehemu huyo.
Aidha, akitoa salamu kwa niaba ya Kikosi Kazi Tanzania, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhad Mussa alitoa pole kwa familia ya marehemu pamoja na kumuombea marehemu maghfira kwa Mwenyezi Mungu.

Vile vile, akitoa shukrani kwa niaba ya familia ya marehemu, ndugu wa marehemu huyo Abdalla Ali Mwinyi aliwashukuru wananchi wote walioungana na familia katika msiba huo mzito wa ndugu yao.
Marehemu Hassan Ali Mwinyi (66) akiwa mtoto wa Pili wa Familia ya Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Alhaj Ali Hassan Mwinyi kutoka uzawa wa Mama Mtumwa Yussuf, ameacha mjane na watoto saba, wakati ambapo katika kipindi cha uhai wake aliwahi kuwa Mtumishi wa Umma na miongoni mwa nyadhifa alizoshika ni pamoja na Meneja wa Shirika la Meli Zanzibar.
Viongozi mbalimbali wa Kitaifa walishiriki maziko hayo akiwemo Rais mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Abeid Amani Karume, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, Waziri Mkuu mstaafu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Kayanza Pinda pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali ya SMZ,SMT na masheikh.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news