Mwanga Hakika Bank Limited yawakutanisha wanahisa wake

NA MWANDISHI WETU

BENKI ya Mwanga Hakika imefanya mkutano mkuu wa pili na wanahisa wake (Annual General Meeting) huku wakielezwa benki hiyo ilipotoka, ilipo na pia inapokwenda.
Mkutano huo umefanyika Agosti 27, 2022 katika Ukumbi wa Baobab Retreat Hall wilayani Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro ukiwa pia na lengo la kutimiza sheria ya nchi, inayotaka kila kampuni kufanya mkutano mkuu na wanahisa wao kila mwaka.

Mbali na hayo,mkutano huo ulikuwa na lengo la kuimarisha uhusiano uliopo baina ya wanahisa hao na benki hiyo, ili kuwataarifu wanahisa hao kuhusu benki hiyo ilipotoka, ilipo na pia inapokwenda ili kuweza kupata taarifa kamili na ili wanahisa hao waweze kutathmini maendeleo ya benki hiyo na kubaini changamoto ili ziweze kutatuliwa.

Sambamba na kutoa ushauri juu ya masuala ya kimaendeleo yatakayoikuza benki hiyo na kuwa imara zaidi.

Mkutano huu ni mkutano wa pili na wanahisa wa Benki ya Mwanga Hakika, ambapo mkutano wa kwanza ulifanyika mwaka 2021 na kuhudhuriwa na wanahisa mbalimbali, kwa lengo la kuimarisha uhusiano wao na wanahisa wa benki hiyo.

Pia mikutano hii ina chachu ya kukutanisha wanahisa kwa pamoja na kudumisha umoja na mshikamano wao.

Mbali na hayo, benki ya Mwanga Hakika imefanya mkutano huo wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro kwa sababu benki hiyo chimbuko lake ni Mwanga ambapo ilianzishwa mwaka 2000, ikiwa inaitwa Mwanga Community Bank (Benki ya Wananchi Mwanga) na baadhi ya wanahisa waliohudhuria mkutano huo ni waasisi, kwani walikuwepo tangu benki hiyo ilipokuwa changa.

Na kama wasemavyo Waswahili “Mcheza Kwao Hutuzwa”. Benki ya Mwanga Hakika inatambua hilo na kuenzi msemo huo.

Mkutano huo uliohudhuriwa na wanahisa zaidi ya 300, wakiwemo waasisi na viongozi mbalimbali wa benki hiyo nao ni,Mhandisi Ridhiwani Mringo ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Mwanga Hakika, pia Mhe.Cleopa Msuya (aliyekuwa Makamu wa Rais, Waziri Mkuu mstaafu, Mwanahisa wa Benki ya Mwanga Hakika, na mshauri wa benki hiyo).
Wengine ni Mhandisi John K Msemo (Mkurugenzi), CPA (T) Zukra Ally (Mjumbe wa bodi), Bw. Christopher Mageka (Mkaguzi wa nje wa mahesabu), Mwakilishi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Bw. Leodgara A. Haule na wengine wengi.

Kabla ya mkutano huo kulikuwa na semina na wanahisa, ambapo waliweza kutoa maoni, pongezi na kutaka ufafanuzi juu ya maendeleo ya benki hiyo miaka ijayo.

Pia Mjumbe wa bodi, CPA (T) Zukra Ally, alitoa elimu ya uwekezaji kwa njia ya hisa, na alieleza kuhusu gawio la wanahisa, ununuaji na uuzaji wa hisa, na kueleza baadhi ya sheria zinazoongoza benki hiyo.

“Sheria ya Mapato (2004) inadhibiti masuala ya teknolojia na TEHAMA sababu mabenki yanakuwa na mtandao mkubwa ila kupitia sheria hizi kunakuwa na siri baina ya mabenki na watu wao.

“Katika ulimwengu wa leo, kampuni zenye hisa ndio chombo madhubuti cha kuwekeza biashara,mradi tu kuwepo na uimara wa bodi,menejimenti ya wenye taaluma ya biashara husika kama ifanyavyo Benki ya Mwanga Hakika, hivyo msisite kuweka hisa zenu,’’amesema CPA (T) Zukra Ally.

Mmoja kati ya wanahisa hao, Bw.Josephat Shirima alisema kuwa, “Nipende kupongeza uongozi wote wa Benki ya Mwanga Hakika kwa tukio hili linaonyesha kuwa mnatambua mchango wetu, ningeomba pia kama kuna uwezekano tawi mojawapo liwe ni kwa jina la Mhe. Cleopa Msuya, ili kuonyesha kwamba tunatambua mchango wake kwenye benki hii,kwani amepigana vema tangu benki hii ilipokuwa benki ya wananchi hadi leo”.

Kwenye mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Mwanga Hakika,Mhandisi Ridhiwani Mringo, alieleza mapato na matumizi kwa mwaka ulioishia 31 Disemba 2021, utekelezaji wa mpango wa biashara kwa mwaka mmoja uliopita, na kuteua wajumbe wa bodi kwa mwaka 2021/2022.

Mbali na hayo,kwenye mkutano huo yalijadiliwa mapendekezo kutoka kwa wanahisa, na mwanahisa mmoja aliipongeza benki na alipendekeza benki kuongeza mawakala wa kutosha, pia kuongeza matangazo, ili benki ijulikane vizuri.
Pia, Mhe.Cleopa Msuya, Waziri Mkuu mstaafu, alitoa historia fupi ya jinsi walivyoanzisha Mwanga Community Bank (Benki ya Wananchi Mwanga) na kusema kuwa, “Tulipoanzisha benki hii tulikuwa na lengo la kuwa benki ya jamii, na nipende kumpongeza Mwenyekiti wa Bodi pamoja na bodi yake kwa kazi kubwa walioifanya na naomba muendelee na kazi nzuri ambayo mmeianzisha, vilevile nipende kuwaomba wanahisa wote kutafakari jinsi benki hii inavyowasaidia kimaendeleo.

“Nipende kuomba benki hii iendelee na mchakato wa kuwa benki kubwa ya biashara, na isisahau kuhudumia wateja wadogo wadogo ambao ndio walikuwa lengo kuu la kuanzishwa wka benki hizi za kijamii,”amesema.

Mwakilishi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw.Leodgar A. Haule, aliipongeza benki kwa kufanya vizuri kwa kipindi cha muda mfupi na aliipongeza kwa mtaji ambao umepata hadi kufikia hatua ya kuwa benki ya biashara.

“Nipende kuwapongeza wote,hasa uongozi wa Benki ya Mwanga Hakika pamoja na wanahisa wote kwa juhudi mzifanyazo kuhakikisha benki hiyo inapata maendeleo zaidi, pia niiombe benki hii iendelee kufanya kazi kwa bidii na kufuata sheria mbalimbali zilizopo,"amesema.

Aidha, alisema kuwa, Benki Kuu, itaendelea kusimamia na kutoa ushauri kwa benki kama msimamizi mkuu wa mabenki nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news