Rais Dkt.Mwinyi afungua mkutano wa Kimataifa wa bima, asisitiza umuhimu wake

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, malengo ya nchi na jumuiya mbalimbali katika kuleta mageuzi ya kiuchumi, yanapaswa kwenda sambamba na upangaji na utekelezaji wa mipango ya kuimarisha huduma za bima, kwa misingi kuwa wawekezaji huzingatia sana jambo hilo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi akifuatana na Kamishna wa Mamlaka ya Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Baghayo Abdalla Saqware (kulia) alipowasili Hoteli ya Madinat Al Bahr leo kufungua Mkutano wa 44 wa Umoja wa Mashirika ya Bima, Ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Dkt.Mwinyi amesema hayo katika mkutano mkuu wa 44 wa Umoja wa Wana Bima katika Ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika (OESAI), uliofanyikia katika Hoteli ya Madinat Al Bahr Mbweni Mkoa Mjini Magharibi.

Amesema, uwepo wa huduma bora za bima na zenye uhakika katika nchi wanachama wa OESAI ni miongoni mwa mambo ya msingi yanayozingatiwa na wawekezaji pale wanapofanya maamuzi ya kuwekeza katika miradi ya maendeleo.

Amesema, kauli mbiu ya mkutano huo isemayo “Kuimarisha Sekta ya Bima kwa Maendeleo yajayo’ inaendana na azma ya nchi nyingi barani Afrika zinazopitia katika mageuzi makubwa ya kiuchumi, kupanua wigo katika sekta za uzalishaji pamoja na kuendeleza sekta mpya ambazo hazikuwepo kabla.

Alisema, kuna umuhimu mkubwa wa kuimarisha sekta ya bima ili kuweka kinga kwa ajili ya mitaji mikubwa wakati huu huduma za uchimbaji madini barani Afrika zikiimarika, uchimbaji wa mafuta na gesi, uendelezaji wa viwanda pamoja na kupanda kwa kiwango cha ubunifu katika Sayansi na Teknolojia.
“Nchi nyingi za Visiwa hivi sasa zimeweka mkazo katika kuendeleza uchumi wa buluu ambao umeweka mkazo shughuli zinazohusu matumizi bora za rasilimali za bahari, huku nchi nyingine zikiwa zinakuza sekta za usafirishaji, kilimo, uvuvi pamoja na ufugaji,”amesema.

Amesema, Zanzibar ikiwa nchi ya Visiwa imeweka mkazo katika kuimarisha uchumi wa Buluu katika mwelekeo wake wa kiuchumi, ambapo zamani ilitegemea zaidi sekta ya kilimo, husuan cha zao la Karafuu, na kubainisha mahitaji ya huduma za Bima ambazo zinapswa kubadilika ili kuendana na mabadiliko hayo.

Aidha, alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejikita kuwekeza katika sekta ya Nishati ya Mafuta na Gesi, ujenzi wa miundombinu ya uzalishaji pamoja na Viwanja vya Ndege, Bandari na Barabara, hivyo akabainisha umuhimu wa Mashirika ya Bima kuunga mkono hatua hiyo ili kutoa Kinga kwa wawekezaji na wadau.

Katika hatua nyingine,Dkt. Mwinyi alisema, juhudi za kuleta mageuzi ya kiuchumi Barani Afrika zinakumbana na changamoto nyingi,ikiwemo ukosefu wa mitaji, hususan rasilimali fedha.

Alisema hivi sasa kumekuwepo ugumu na ushindani mkubwa wa kupata mitaji kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo inayolengwa kutekelezwa.

Alitumia fursa hiyo kuyahimiza mashirika na taasisi za bima barani Afrika kuwa na utayari na ubunifu wa kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo katika nchi zao badala ya kukaa na kusubiri kutoa huduma za bima pekee.
Alisema katika nchi zilizoendelea Mashirika ya Bima, mifuko ya Hifadhi ya Jamii na taasisi nyingine za fedha zimekuwa na mchango mkubwa katika upatikanaji wa fedha na mitaji ili kutekeleza miradi kradi ya maendeleo pamoja na kukuza ajira.

Alizishauri taasisi za fedha kuondokana na utaratibu wa kubaki na fedha wakati mahitaji ya fedha hizo yapo na makubwa, na hivyo akazitaka kujifunza katika taasisi za nchi zilizoendelea ili kuona kwa namna gani fedha zinaweza kutumika kwa miradi ya maendeleo.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuyahimiza mashirika ya bima umuhimu wa kuendelea na juhudi za kutanua huduma zake na kuyafikia makundi mbalimbali ya wajasiriamali, wakulima, wavuvi pamoja na wafugaji walioko vijijini.

Vile vile alisisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa jamii ili kuwa na kinga za bima, ikiwa ni hatua ya kuongeza idadi ya watu wanaotumia huduma hizo.

Akigusia utekelezaji wa malengo ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), Dkt.Mwinyi alisema mkazo mkubwa umewekwa ili kukuza biashara na shughuli za Ujasiriamali Barani Afrika.
Alisema, ufanisi na mzunguko wa wafanyabiashara, bidhaa, huduma na mahitaji kati ya nchi na nchi Barani Afrika, unahitaji kuwepo kwa huduma za Bima zilizo imara kwa kiwango cha Kikanda na Kimataifa.

Naye, Waziri wa Fedha na Uchumi Zanzibar, Sada Mkuya Salum alisema katika mkutano huo utakaodumu kwa muda wa siku mbili washiriki watapata fursa ya kuchanganua mafanikio na matatizo yanayoikabili sekta ya bima katika kanda hiyo.

Aidha, Kamishna wa Mamlaka ya Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Baghayo Abdalla Saqware alisema sekta ya bima ina umuhimu mkubwa katika kustawisha uchumi wa Taifa kwa kuongeza ukwasi wa rasilimali fedha.

Alisema, sekta hiyo hutoa kinga kwa wananchi pale majanga mbali mbali yanajitokeza na kuathiri mali, afya na maisha ya watu na hivyo kuwa chachu katika kuondoa umasikini.
Alieleza kuwa, Soko la huduma za Bima linalenga kuongeza uzalishaji kupitia sekta za kilimo, Uvuvi, pamoja na mifugo na akachukua fursa hiyo kuwakaribisha Wawekezaji mbali mbali.

Aliwahakikishia wawekezaji hao kuwa Mamlaka ya Bima nchini ina dhamira ya dhati ya kuwa na Soko la usawa na ushindani, lenye mashirikiano na kufanya kazi kwa weledi na umahiri na kuweka mazingatio makubwa katika kuleta tija.

Mkutano wa 44 wa OESAI utakaodumu kwa muda wa siku mbili, uanwashirikisha washiriki wapatao 350 kutoka mashirika ya Mataifa 30 Duniani, ikiwemo Tanzania, Angola, Botwasana, Eritrea, Eswatini, Ethipoia, UAE, Mozambique, Rwanda pamoja na India.

Mataifa mengine ni Morocco, Namibia, Urusi, Saudi Arabia, Syschelles, Zimbabwe, Zambia, Mauritius, Uganda, Uingereza, Afrika Kusini, Kenya na Bahrain, ambapo pamoja na mambo mengine utajikita katika kujadili namna huduma za bima zinazovyoweza kuwa imara na endelevu pamoja na Utunzaji wa mazingira.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news