Rais Dkt.Mwinyi azindua mafunzo ya walimu wa Sayansi, Hisabati na Kiingereza huku akidokeza jambo

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa, Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari wa kuwajengea uwezo wa masomo ya Sayansi, Hisabati na Kiingereza walimu unakwenda sambamba na mikakati ya Serikali ya kuhakikisha inatoa elimu bora inayoendana na mahitaji ya sasa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika hafla ya Uzinduzi wa Muongozo wa Mafunzo ya Sayansi kwa Skuli za Sekondari Zanzibar, uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B” Unguja. (Picha na Ikulu).

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Agosti 3, 2022 katika uzinduzi wa mafunzo ya Walimu wa Sayansi, Hisabati na Kiingereza pamoja na makabidhiano ya Moduli na Miongozo ya Mafunzo, hafla iliyofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, iliyopo Uwanja wa Ndege jijini Zanzibar.

Katika hotuba yake, Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, Elimu ya Sayansi na Hisabati ina mchango mkubwa katika kufikia malengo hayo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akisalimiana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mhe.Lela Mohamed Mussa na Naibu wake Mhe.Ali Gulam Hussein pamoja na viongozi wengine alipowasili katika hafla ya Uzinduzi wa muongozo wa mafunzo ya Sayansi kwa Skuli za Sekondari katika Ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar,mafunzo hayo yataendeshwa na Shirika la KOICA .

Pia amesema kwamba, ni dhahiri kuwa katika kufikia malengo hayo, ni lazima mikakati imara ya kuinua ufaulu wa masomo ya Sayansi na Hisabati sambamba na uwezo katika lugha ya Kiingereza kwa wanafunzi uimarishwe.

Ameongeza kuwa, katia kipindi cha miaka mitano iliyopita kuanzia mwaka 2017 hadi 2021, matokeo ya wanafunzi katika mitihani ya Taifa ya kumaliza elimu ya Sekondari hayakuwa yakiridhisha.

Amesema kwamba, kwa wastani asilimia 33 ya wanafunzi kila mwaka wanakosa vyeti na wengi wao ni wale wanaosoma masomo ya sayansi ambapo ufaulu mdogo wa wanafunzi hasa katika masomo ya Sayansi na Hisabati unachangiwa kwa kiasi kikubwa na uhaba wa walimu wenye sifa, uhaba wa maabara na uhaba wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwa vitendo.

Hivyo, Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na washirika mbalimbali wa maendeleo ili kuhakikisha changamoto zinazoathiri ufaulu wa masomo ya Sayansi zinapatiwa ufumbuzi kwa kuwajengea walimu uwezo zaidi wa ufundishaji wa masomo hayo na pia, kujenga maabara za Sayansi na kuzipatia vifaa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi (wa pili kulia) akimsikiliza Meneja mwandamizi wa Goodneighbors Nd.John Massenza akitoa maelezo wakati alipotembelea maonesho ya Vitabu mbali mbali vya kufundishia katika hafla ya Uzinduzi wa muongozo wa mafunzo ya Sayansi kwa Skuli za Sekondari nje Ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar,ambapo Shirika la Koika litaendesha mafunzo hayo.

“Nafurahi kusikia kwamba tulianza kuwapatia mafunzo walimu 600 wanaosomesha Sekondari Kidato cha Kwanza na cha Pili kwa masomo ya Sayansi, Hisabati na Kiingereza kupitia Mradi wa ZISP ambao Serikali inautekeleza kwa ushirikiano na Benki ya Dunia na leo tena kwa kushirikiana na KOICA tutawapatia mafunzo walimu wa Skuli za Sekondari wa Kidato cha Tatu na cha Nne wanaosomesha masomo ya Sayansi,Hisabati na Kiingereza Unguja na Pemba,”amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Mwinyi.

Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, mkakati wa Serikali ni kuhakikisha skuli zote mpya zinakuwa na maabara za Sayansi, maabara za Kompyuta na maktaba za kisasa pamoja na kuzipatia vifaa.
Wanafunzi wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi (kushoto) akizungumza wakati wa Uzinduzi wa muongozo wa mafunzo ya Sayansi kwa Skuli za Sekondari yatakayoendesha na Shirika la Koika hafla iliyofanyika leo katika Ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar.

Amesema kuwa, hayo ni miongoni mwa mageuzi makubwa ya elimu ambayo Serikali inaendelea kuyafanyia kazi ambapo kupitia mageuzi hayo Serikali itaimarisha matumzi ya teknolojia katika skuli zote ili kurahisisha ufundishaji na kujifunza kwa walimu na wanafunzi hasa katika ngazi ya Elimu ya Msingi na Sekondari.

Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, matumizi ya teknolojia yatawasaidia sana wanafunzi kuweza kujifunza popote walipo na si lazima kuwepo darasani kwani itakumbukwa wakati wa Janga la UVIKO-19, pale ambapo Skuli zilifungwa kwa takriban miezi mitatu na bado wanafunzi waliendelea kusoma.
Viongozi mbali mbali wakiwa katika hafla ya Uzinduzi wa muongozo wa mafunzo ya Sayansi kwa Skuli za Sekondari yatakayoendesha na Shirika la Koika hafla iliyofanyika leo katika Ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar,mgeni rasmi akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani).

Amesisitiza kwamba Serikali kupitia mageuzi ya elimu itaimarisha mafunzo ya Amali na Ufundi kwa kuhakikisha kila wilaya ina vyuo vya aina hiyo kwa ajili ya watoto ili waweze kupata ujuzi wa ufundi utakaowawezesha kujiajiri wenyewe na kujipatia kipato kwa ajili ya kuimarisha maisha yao.

Rais Dkt.Mwinyi ametoa wito kwa walimu wote wa shule za Serikali, walengwa wa mafunzo hayo wanaofundisha masomo ya Hisabati, Sayansi na Kiingereza kushiriki kikamilifu katika kuyapokea mafunzo hayo na kwenda kuyafanyia kazi wakati wanapofundisha wanafunzi wao madarasani.

Sambamba na hayo, Rais Dkt.Mwinyi alilishukuru Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Korea (KOICA), Good Neighbors na washirika wenzao wa maendeleo katika kutekeleza na kufanikisha mradi huo muhimu wa mafunzo ya walimu aliyoyazindua.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akipokea Vitabu vya muongozo wa mafunzo ya Sayansi,Hesabati na Kiingereza kutoka kwa Balozi wa Korea Kusini Nchini Tanzania Mhe.Sun Fyo Kim baada ya Uzinduzi wa muongozo wa mafunzo hayo uliofanyika leo katika Ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar.

“Nawashukuru sana Serikali ya Korea ya Kusini, KOICA na Taasisi ya Good Neighbors kwa msaada wao huo mkubwa katika sekta ya elimu,”alisema Rais Dkt.Mwinyi.

Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Leila Mohammed Mussa alitoa pongeza kwa KOICA kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya elimu.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiagana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe.Lela Mohamed Mussa mara baada ya Uzinduzi wa muongozo wa mafunzo ya Sayansi kwa Skuli za Sekondari yatakayoendesha na Shirika la Koika hafla iliyofanyika leo katika Ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar.

Alieleza kwamba mbali ya msaada wao huo wa mafunzo kwa walimu wa Sayansi wa Sekondari pia, KOICA imesaidia katika ujenzi wa maabara kumi za kisasa ya Sayansi Unguja na Pemba.

Ameeleza juhudi za Serikali katika kuimarisha sekta ya elimu ambapo imetenga jumla ya shilingi Bilioni 63 kwa ajili ya miradi ya elimu zinazotokana na fedha za ahuweni ya UVIKO-19.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiangalia Ngoma ya Msewe katika viwanja vya Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Unguja. alipowasili katika viwanja vya Hoteli hiyo,kwa ajili ya Uzinduzi wa Muongozo wa Mafunzo ya Sayansi kwa Walimu wa Skuli za Sekondari Zanzibar, na (kushoto kwa Rais) Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe.Idrisa Mustafa Kitwana na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said na (kulia kwa Rais) Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Mohammed Mussa.

Balozi wa Korea ya Kusini, Sun Pyo Kim kwa upande wake alimuhakikishia Rais Dkt.Mwinyi kwamba Serikali ya Korea ya Kusini itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika miradi yake mbalimbali ya maendeleo ikiwemo sekta ya elimu.

Balozi Kim alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa juhudi zake za kuiimarisha sekta ya elimu.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Meneja Mwandamizi wa Good Neighbors Tanzania John Messenza akitowa maelezo ya Vitabu vya muongozo wa Elimu ya Sayansi, wakati akitembelea maonesho hayo ya nyenzo za kufundishia masomo ya Sayansi, Hisabati na Kiingereza katika viwanja vya Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Unguja Wilaya ya Magharibi “B” Unguja na (kulia kwa Rais) Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Mohammed Mussa na (kushoto kwa Rais) Balozi wa Korea ya Kusini Nchini Tanzania Mhe.Sun Pyo Kim na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Ali Abdulgulam Hussein.

Mapema Mkurugenzi Mkaazi wa KOICA, Kyucheol Eo pamoja na Mkurugenzi Mkaazi wa Good Neghbors kwa nyakati tofauti walieleza hatua wanazozichukua katika kuiunga mkono Zanzibar kwenye sekta ya elimu huku wakiahidi kuendeleza misaada yao ili kuhakikisha masomo ya Sayansi, Hisabati na Kiingereza mafunzo yake yanatolewa kwa ufanisi mkubwa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B” Unguja, wakati ukipigwa wimbo wa Taifa wa Zanzibar, Tanzania na wa Afrika Mashariki, kabla ya kuaza kwa Uzinduzi wa Muongozo wa Mafunzo ya Elimu ya Sanyasi Zanzibar, na (kulia kwa Rais) Balozi wa Korea ya Kusini Nchini Tanzania Mhe. Sun Pyo Kim,Mkurugenzi Mkaazi wa KOICA Tanzania Bw. Kyucheol Eo na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said na (kushoto kwa Rais) Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Mohammed Mussa na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe. Idrisa Mustafa Kitwana.
Wageni waalikwa katika hafla ya Uzinduzi wa Muongozo wa Mafunzo ya Elimu ya Sayansi kwa Skuli za Sekondari Zanzibar, wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi.(hayupo pichani) akihutubia na kizindua Muongozo huo, uzinduzi huo uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B” Unguja. Baadhi ya Watendaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi.(hayupo pichani) akihutubia na kuzindua Muongozo wa Mafunzo ya Sayansi kwa Skuli za Sekondari Zanzibar, uzinduzi huo uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B” Unguja.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika hafla ya Uzinduzi wa Muongozo wa Mafunzo ya Sayansi kwa Skuli za Sekondari Zanzibar, uzinduzi huo uliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B” Unguja leo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akikabidhiwa Vitabu vya Muongozo wa Mafunzo ya Sayansi, Hesabati na Kingereza na Balozi wa Korea ya Kusini Nchini Tanzania Mhe. Sun Pyo Kim (kulia kwa Rais) na Mkurugenzi Mkaazi wa KOICA Tanzania Bw.Kyucheol Eo na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said na (kushoto kwa Rais) Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Mohammed Mussa, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe.Idrisa Mustafa Kitwana na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Ali Abdulgulam Hussein.(Picha na Ikulu).

Wakati huo huo, Rais Dkt.Mwinyi alikabidhiwa vitabu vya miongozo ya mafunzo na moduli kwa walimu pamoja na Kamati za Skuli ambapo mapema mara baada ya kufika hotelini hapo alitembelea mabanda maalum yaliyowekwa nyenzo za kufundishia na kupata maelezo juu ya namna za kufundishia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news