Rais Dkt.Mwinyi:Serikali itaendelea kuwekeza katika elimu, tumedhamiria kupata matokeo bora

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa, dhamira ya Serikali ya Awamu ya Nane ni kuona kwamba kiwango cha ufaulu wa wanafunzi wa skuli za Zanzibar unazidi kuimarika kila mwaka katika mitihani yao ya Taifa.
Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi akimkabidhi zawadi ya fedha mwanafunzi bora nafasi kumi Kitaifa Wanawake Tanzania wa Skuli ya Zanzibar Commercial Kidato cha Sita, Nasra Ali Omar, wakati wa hafla ya Chakula Maalum na kuzawadiwa zawadi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi, wanafunzi Bora waliofanya vizuri mitihani yao ya Taifa, katika viwanja vya Ikulu jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Agosti 3, 2022 katika hafla ya chakula alichowaandalia wanafunzi waliofaulu vyema zaidi katika mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne mwaka 2021 na Kidato cha Sita mwaka 2022, hafla iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu jijini Zanzibar.Amesema kuwa, Serikali itaendelea kuwekeza katika sekta ya elimu kwenye ujenzi wa miundombinu ya taasisi za elimu, kuzipatia vitendea kazi vikiwemo vifaa vya kusomea na kusomeshea na kutoa mafunzo kwa walimu ili wapate mbinu bora za kufundishia.

Rais Dkt.Mwinyi aliwaahidi kuwapatia kompyuta mpakato wanafunzi wote wa Kitado cha Sita na Kidato cha Nne waliopata daraja la kwanza wa Unguja na Pemba.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi zawadi ya kompyuta mpakato mwanafunzi Nasra Ali Omar wa Skuli ya Zanzibar Commercial ambaye ametokea kuwa kati ya wanafunzi 10 bora Kitaifa Wanawake kwa Tahasusi ya ECA, na kushoto kwa Rais ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Mohammed Mussa, hafla hiyo ilifanyika leo katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Pia, Rais Dkt.Mwinyi amewaeleza wanafunzi waliofaulu kidato cha sita kwamba wote watapata mikopo ya Elimu ya Juu na kusisitiza kwamba Serikali itahakikisha inaiwekea mazingira mazuri bodi hiyo huku akiwaleza kwamba wana fursa ya kutumia bodi zote mbili za mikopo ikiwemo ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Dkt.Mwinyi amesisitiza haja kwa Wizara ya Elimu kufanya mashindano baina ya Skuli na Skuli, Mikoa na Mikoa pamoja na Wilaya kwa Wilaya kwani ushindani unaleta matokeo mazuri.

Katika kuzithamini juhudi za wanafunzi hao Rais Dkt.Mwinyi ametoa nafasi za udhamini wa masomo “Scholaship” kwa wanafunzi 30 waliofanya vizuri katika mitihani yao ili kuendelea na masomo katika vyuo mbali mbali.
Wanafunzi wa Kidato cha Sita na Nne Skuli za Sekondari Unguja wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) wakati wa hafla ya chakula maalum cha mchana na kuzawadia zawadi kwa kufaulu vizuri mitihani yao ya Taifa, hafla hiyo ilimefanyika katika viwanja vya Ikulu jijini Zanzibar leo.(Picha na Ikulu).

Pia ametoa pongezi kwa skuli binafsi ambazo nazo zimekwua zikifanya vizuri na kuweza kuisaida Serikali katika kupunguza mzigo wa wanafunzi katika skuli zilizopo za serikali.

Sambamba na hayo, aliahidi mafunzo na maslahi kwa walimu na kuahidi kwamba Serikali anayoiongoza itahakikisha inayazingatia.

Naye Waziri wa Elimu Leila Mohamed Mussa alieleza mikakati iliyowekwa na wizara hiyo katika kuimarisha sekta ya elimu huku akiwasihi wanafunzi waliopata daraja la kwanza wa kidato cha nne na sita kujitambua na kuthamini jambo hilo walilofanyiwa na Rais.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ,Ali Abdulgulam ameeleza kwamba, mafanikio hayo yote yametokana na ushirikiano wa pamoja kati ya uongozi wa wizara hiyo, watendaji,walimu pamoja na wazazi.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ali Khamis Juma akitoa takwimu za uafaulu wa wanafunzi alisema mtihani ya kidato cha nne ulifanyika mwezi Novemba 2021 na matokeo yake yalitoka Januari 2022 ambao jumla ya wanafunzi 15,569 walifanya mtihani huo na wanafunzi 4,403 wamefanikiwa kuendelea namasomo ya kidato cha tano Julai 2022.

Alisema kuwa, ufaulu wao ni kati ya daraja la kwanza hadi la tatu na ni sawa na asilimia 28.3, kati ya wanafunzi hao,wanafunzi 445 walipata daraja la kwanza ambapo ni sawa na asilimia 2.8 tu, ambao 308 ni miongoni mwao ambao wamefika Ikulu ya Mnazimmoja leo.

Pia amesema mtihani wa kidato cha sita ulifanyika Mei 2022 na matokeo yake yalitokea mwezi Julai 2022 ambapo jumla ya wanafunzi 3,683 walifanya mitihani na wanafunzi 3,644 waliofaulu kuendelea na masomo kwa ngazi ya elimu ya juu katika vyuo vya ndani na nje kwa fani zote ambazo Serikali itawekea kipaumbele kulingana na mahitaji yake.

Amesema kuwa, kati ya wanafunzi hao, wanafunzi 693 walipata daraja la kwanza, ambapo 542 ndio waliofika katika hafla hiyo ya chakula na zawadi Ikulu Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiwa na Mkewe Mama Mariam Mwinyi wakiwa katika picha ya pamoja na Wanafunzi Bora wa Kidato cha Sita kulia kwa Mama Mariam Mwinyi) ni mwanafunzi Nasra Ali Omar Skuli ya Zanzibar Commercial, mwanafunzi Marco Andra Masabula (Lumumba) na kushoto kwa Rais ni Idrisa Ali Shaban (Skuli ya Zanzibar Commercial), Nahya Said Ahmed (Skuli ya Zanzibar Commercial ) na Firdaaus Salum Seif (FEZA). (Picha na Ikulu).

Amesema, takwimu za ufaulu kwa kidato cha nne zimekuwa za kutia moyo mwaka hadi mwaka kwa vile kuna ishara zilizowazi za kuimarika na hivyo kuifanya Zanzibar nayo kuwa ni mshindani halisi kwenye matokeo ya mitihani katika mikoa ya hapa nchini.

Katibu Mkuu huyo amesema kuwa, wizara inafanya jitihada za makusudi kuona kuwa matokeo ya mitihani ya kidato cha 4 na 6 yanakuwa mazuri na yenye kupendeza ambapo kuanzia mwaka huu, Wizara hiyo inakusudia kuongeza ufaulu angalau kwa wastani wa asilimia tano kwa kila mwaka.

“Matokeo yote haya ni mazuri sana na mara ya kwanza kutokea tangu Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964, matokeo haya yamekuja chini ya uongozi wako mahiri wa Serikali ya Awamu ya Nane, ni dhahiri kuwa mafanikio yanahakisi ile slogan yako ya uchaguzi kuwa ‘Yajayo yanafurahisha, yajayo ni neema tupu,"alisema.

Rais Dkt.Mwinyi pia alitoa zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri zaidi wakiwemo wanafunzi watatu waliopata kompyuta mpakato akiwemo mwanafunzi bora katika Tahasusi ya ECA (Economic,Commerce na Account) Nasra Ali Omar ambaye pia anaingia katika kundi la wanawake 10 bora Tanzania.

Post a Comment

0 Comments