Rais Dkt.Mwinyi:Pia Sensa ina mchango mkubwa katika Uchumi wa Buluu nchini

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Sensa ya Watu na Makazi 2022 ina mchango mkubwa katika kuimarisha shughuli mbalimbali za sekta ya Uchumi wa Buluu hapa nchini.
Dkt.Mwinyi amesema hayo nyumbani kwake Ikulu ndogo Migombani jijini Zanzibar, baada ya kukamilisha zoezi la kuhesabiwa katika Sensa ya Watu na Makazi leo Agosti 23,2022.

Amesema, kupitia sensa, Serikali itaweza kutambua idadi ya watu na shughuli wanazofanya katika Sekta ya Uchumi wa Buluu hatua itakayosaidia mipango ya Serikali katika uimarishaji wa sekta hizo.

Akiambatana na mkewe Mama Mariamu Mwinyi, Rais Dkt.Mwinyi ametoa wito kwa wananchi wote Unguja na Pemba kushiriki kikamilifu katika zoezi la kuhesabiwa, akibainisha faida kubwa itakayopatikana ya kuliwezesha Taifa kupanga mipango yake ya maendeleo.

Amesema, takwimu zitakazopatikana kupitia sensa hiyo zitaisaidia Serikali kupanga mipango ya maendeleo kwa kipindi cha miaka kumi pamoja na kujua mahitaji katika sekta zote, ikiwemo huduma mbalimbali za kijamii, kama vile maji, elimu, afya na nyinginezo.

Akiongoza kaya yake wakati wa kuhesabiwa, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi aliwatoa hofu wananchi kwa kusema zoezi hilo ni rahisi na lisilotumia muda mwingi.

“Maswali yana lengo la kujua idadi ya watu na shughuli zao, ni zoezi rahisi, halitumii muda mrefu, maswali yake rahisi, hakuna sababu ya kuwa na hofu,"amesema.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiwa na mkewe, Mama Mariam Mwinyi wakimsikiliza Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Zanzibar, Balozi Mohammed Hamza, kabla ya kuaza kwa zoezi lililofanyika katika Makazi ya Rais Ikulu ndogo Migombani Wilaya ya Mjini Unguja leo Agosti 23,2022, na kushoto kwa Rais ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mhe. Idrisa Kitwana Mustafa.(Picha na Ikulu).

Mapema, Kamisaa wa Sensa na Makaazi 2022 Zanzibar, Balozi Mohamed Hamza alisema ana matumaini makubwa kuwa zoezi hilo litakamilika vyema, huku akibainisha taarifa za awali za wananchi kulipokea vizuri zoezi hilo.

Aidha, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa alieleza matarajio yake ya zoezi hilo kupata ufanisi kwa kuzingatia kuwa linafanyika katika mazingira ya amani na usalama pamoja na kuwapongeza watendaji kwa maandalizi bora na kuwa na mipango mizuri.

Naye Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Salum Kassim Ali amesema, mchakato wa kuhesabu watu katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo kwenye mahoteli, hospitalini,bandarini, maeneo ya visiwa na dago na maeneo mengine umefanyika kikamilifu kwa watendaji na makarani wa Sensa kufika na kufanikisha na kutekeleza kwa ufanisi majukumu yao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news