Rais Samia aiagiza TARURA kutoa orodha ya Makandarasi waliowahi kuharibu kazi

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameitaka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kutoa orodha ya makandarasi waliowahi kuharibu ujenzi wa miundombinu ili wasipewe kazi nchini.

Pia Mheshimiwa Rais Samia ameonya tabia ya kuwepo kwa madalali wanaotoa zabuni kwa watu wasio na uwezo wala sifa nchini.

Mheshimiwa Rais Samia ametoa agizo hilo leo Agosti 14, 2022 jijini Dodoma wakati wa hafla ya utiaji saini Mikataba Kati ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na Makandarasi watakaotekeleza kazi za Ujenzi,Ukarabati na Matengenezo ya Miundombinu ya Barabara kwa Mwaka wa Fedha 2022/23 ambapo leo imesainiwa mikataba 10 kati ya 960.

”Ninaagiza mikataba yote 960 iende kwa wakandarasi wenyewe hasa wa ndani na kujiepusha na madalali ambao wamekuwa wakifanya kazi chini ya kiwango na kwa kuchelewa na wakandarasi wababaishaji hawatakuwa na nafasi.”amesema Rais Samia

Pia amewataka wakandarasi wazawa kubadilika na kujenga barabara za kudumu na zenye kutumia teknolojia japo kwa miaka 10 badala ya mazoea ya ujenzi wa barabara za msimu zinazoisababishia Serikali gharama za mara kwa mara.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Samia ameielekeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango kupitia vifungu vya kisheria kuhusu teknolojia ya ujenzi wa barabara na madaraja nchini ili kuongeza tija na thamani ya fedha katika miradi ya barabara nchini.

“Huko nyuma kila mwaka mabilioni yalikuwa yanatolewa kurekebisha barabara, mvua zikija zinabomoa. Hata hivyo, Kuna teknolojia mbadala tuzitumie hasa maeneo ya vijijini ili barabara zikijengwa kuwe na nafasi ya angalau miaka saba ndio tufanye matengenezo,”amesema Mheshimiwa Rais Samia.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amesema katika mwaka wa fedha 2022/23 ujenzi wa barabara kwa iwango cha lami utakuwa na urefu wa kilomita 422, kiwango cha changarawe urefu wa kilomita 11,074, madaraja 269 na matengenezo kwa barabara yatakayofanyika ni ya urefu wa kilomita 21,595.

Amesema, bajeti ya ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara vijijini na mijini imeongezeka kutoka shilingi bilioni 272.56 mwaka 2020/21 hadi shilingi bilioni 722 katika mwaka wa fedha 2021/22 sawa na ongezeko la asilimia 185.

”Mwaka wa fedha 2022/23 ni mwaka wa pili wa utekelezaji wa Mpango Mkakati ambapo TARURA imetengewa bajeti ya jumla ya shilingi bilioni 838.16 ambapo kati ya hizo Shilingi bilioni 776.63 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 61.53 ni fedha za nje,”amesema Mheshimiwa Bashungwa.

Pia amesema, Ofisi ya Rais-TAMISEMI ilitoa maelekezo kwa TARURA kuanza taratibu za manunuzi mapema ili kazi ziweze kuanza kabla ya kipindi cha mvua ambapo tayari TARURA ilitangaza zabuni 1,085 zenye thamani ya shilingi bilioni 378.56, sawa na asilimia 60 ya fedha zilizopangwa kutekeleza miradi ya barabara za vijijini na mijini, kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TARURA , Mhandisi Victor Seff amesema kuanzia mwaka 2021/22 hadi 2026/27 lengo ni kuongeza mtandao wa barabara za lami kwa kilomita 1,450.75 kutoka kilomita 2,404.90 zilizopo sasa hadi kufikia kilomita 3,855.65.

Aidha, changarawe kilomita 73,241.57 kutoka kilomita 29,116.57 hadi kufikia kilomita 102,358.14 na madaraja 3,808 kutoka 2,812 hadi kufikia madaraja 6,620.

Mhandisi Seff amebainisha kuwa, fedha zitakazotumika kwenye mpango huo zinakadiriwa kuwa zaidi ya shilingi trilioni 4.2 za Kitanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news