Rais Samia atoa maagizo kwa DCI Kingai

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Samia Suluhu Hassan amemuagiza Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Nchini (DCI) Ramadhan Kingai kuhakikisha unafanyika upelelezi na kuwa na ushahidi wa kutosha kabla ya kumuweka mtuhumiwa mahabusu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan akiagana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Camilius Wambura pamoja na Makamanda wengine wa Jeshi hilo mara baada ya kufungua Kikao Kazi cha Makamanda hao kilichofanyika kwenye Chuo cha Polisi (CCP) Mkoani Kilimanjaro tarehe 30 Agosti, 2022.(Picha na Ikulu).

Rais Samia ametoa agizo hilo leo wakati akifungua Kikao Kazi cha Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi Makao Makuu, Makamanda wa Polisi wa Mikoa/Vikosi katika Shule ya Polisi Tanzania (TPS) iliyoko wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro.

Aidha, Rais Samia amesema kesi za watuhumiwa 1,840 zimefutwa na kuachiwa huru kwa kukosekana ushahidi ambapo kuwakamata watuhumiwa hao kumeipa gharama Serikali na familia za watuhumiwa.

Rais Samia amelitaka Jeshi la Polisi kukabiliana na changamoto za kiutawala na kiufundi, kuangalia upya mitaala ya mafunzo pamoja na kufanya mageuzi makubwa ya kimuundo na kimfumo inayoendana na mabadiliko ili kukabiliana na changamoto za sasa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu (IGP) Omari Mahita mara baada ya kufungua Kikao Kazi Cha Maafisa Wakuu Waandamizi wa Makao Makuu ya Polisi na Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi kilichofanyika katika Chuo cha Polisi (CCP) Mkoani Kilimanjaro tarehe 30 Agosti, 2022.

Rais Samia amesema upungufu wa mafunzo unachangia mmomonyoko wa maadili ndani ya Jeshi la Polisi hivyo Serikali imetenga shilingi bilioni 11 kwa ajili ya mafunzo ya askari polisi.

Vile vile Rais Samia amesema Serikali itaendelea kufanya uwezeshaji wa kifedha ili Jeshi hilo lifanye marekebisho ya kiutendaji katika mafunzo ya TEHAMA kuanzia ngazi za wilaya hadi mkoa.

Rais Samia pia amelitaka Jeshi la Polisi kuacha matumizi mabaya ya fedha hususan zile za bajeti zinazopelekwa kwao na kutaka kuwa na uhusiano mzuri kati yake na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na viongozi wengine katika picha ya pamoja na Maafisa Wakuu Waandamizi wa Makao Makuu ya Polisi na Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi mara baada ya kufungua Kikao Kazi cha Makamanda hao kilichofanyika kwenye Chuo cha Polisi (CCP) Mkoani Kilimanjaro tarehe 30 Agosti, 2022.

Kwa upande mwingine, amelitaka Jeshi hilo kudhibiti matumizi ya fedha za Mifuko ya ndani ya askari polisi, fedha zitokanazo na tozo na faini pamoja na zile za Mikataba mbalimbali inayosainiwa na Jeshi hilo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan akiagana na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu mara baada ya kufungua Kikao Kazi cha Makamanda hao kilichofanyika kwenye Chuo cha Polisi (CCP) Mkoani Kilimanjaro tarehe 30 Agosti, 2022.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news