Rais Samia atoa salamu za rambirambi kutokana na vifo vya watu 19 katika ajali

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homera kufuatia vifo vya watu 19 vilivyotokea katika ajali ya gari.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais-Ikulu, Bi.Zuhura Yunus ikielezea kuwa, ajali hiyo imetokea Agosti 16, 2022 saa mbili asubuhi katika eneo la Shamwengo Kata ya Inyala tarafa ya Tembela Wilaya ya Mbeya Vijijini mkoani Mbeya.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Ulrich Matei, waliopoteza maisha ni watu 19 (wanawake sita, wanaume 12 na mtoto mmoja) na majeruhi ni 25.

SACP Matei amesema, ajali hiyo imehusisha lori lililokuwa likitoka Mbeya kwenda Dar es Salaam, lenye namba za usajili T387 DSJ na tela namba T 918 DFE mali ya Kampuni ya Everest French Limited.

Lori hilo lililokuwa imebeba kontena la mchanga ililigonga kwa nyuma basi la abiria la Kampuni ya Super Rojas iliyokuwa ikitoka Mbeya kwenda Njombe.

Aidha, basi hilo nalo lililigonga kwa nyuma gari ndogo aina ya Benz yenye namba ya usajili T 836 DRE ambalo nalo liligonga Lori lililokuwa limebeba kontena lenye namba ya usajili T342 CHG na tela namba CGS kwa nyuma.

"Rais Samia anawapa pole majeruhi wa ajali hiyo pamoja na wafiwa wote pia anaungana na familia hizo katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu wote mahali pema. Amina,"imeeleza taarifa hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news