Rais Samia azindua Mpango Utoaji Rizuku ya Mbolea, aagiza utekelezaji wake kuanza ifikapo Agosti 15, 2022

NA MWANDISHI WETU

RAIS wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi Mpango wa Utoaji wa Ruzuku ya Mbolea kwa wakulima na kuagiza utekelezaji wake uanze mapema ifikapo tarehe 15 Agosti, 2022 ili kutoa nafasi kwa wakulima kujiandaa kuanza msimu wa kilimo kwa mwaka 2022/2023.
Rais Samia Suluhu Hassan akimsikiliza Waziri wa Kilimo Hussein Bashe akimwomba Rais kuridhia bei za mbolea zilizowasilishwa kwake kwa kukata utepe ili kuwapa nafuu ya bei ya mbolea wakulima nchini wakati wa maadhimisho ya siku ya mkulima kitaifa yaliyofanyika katika viwanja vya Mwakangale Jijini Mbeya tarehe 8 Agosti, 2022.

Uzinduzi huo umefanywa leo tarehe 8 Agosti, 2022 ikiwa ni kilele cha maazimisho ya sherehe za wakulima maarufu kama nanenane yenye lengo la kutambua mchango wa Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi katika kuongeza uhakika wa upatikanaji wa chakula na lishe bora na kuongeza kipato kwa wananchi na nchi kwa ujumla.

Pamoja na uzinduzi huo Rais Samia amekiri kuona hari ya watumishi wa Wizara ya kilimo na taasisi zake kwenda kutekeleza kwa dhati mipango ya utoaji wa ruzuku na mipango mingine inayotekelezwa na kusimamiwa na wizara hiyo.
Rais Samia Suluhu Hassan akiwa amekata utepe ikiwa ni ishara ya kuzindua rasmi mpango wa ruzuku za mbolea zitakazoanza kutolewa kwa wakulima kuanzia tarehe 15 Agosti, 2022 wakati wa maadhimisho ya sikukuu ya wakulima nanenane yaliyofanyika katika viwanja vya Mwakangale Jijini Mbeya.

Akizungumzia ruzuku inayotolewa mwaka huu wa fedha, Rais Samia amesema Serikali haitajikita katika kutoa ruzuku za mbolea kwa miaka yote na kuwataka wakulima kutumia fursa hii ya ruzuku kuzalisha kibiashara ili kipatikane chakula cha kutosha pamoja na cha kuuza nje ya nchi ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na nchi.

Ameongeza kuwa uzalishaji huo utapelekea Serikali kuanzisha mfuko wa pembejeo utakaotumika wakati kunapotokea dharura na kusababisha kupanda kwa bei za pembejeo za kilimo kusiko kwa kawaida na mfuko huo kutumika kuwapunguzia wakulima hadha ya bei.
Baadhi ya wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) wakiwa kwenye jukwaa tayari kufuatia sherehe za maadhimisho ya sikukuu ya wakulima nanenane yaliyofanyika katika viwanja vya Mwakangale Jijini Mbeya leo tarehe 08 Agosti, 2022.

Pamoja na mpango wa Serikali wa kutoa ruzuku za mbolea, Rais Samia ameeleza mipango mahususi ya kuongeza uzalishaji wa ndani wa mbolea na kueleza uwepo wa kiwanda cha Itracom kinachojengwa mkoani Dodoma na kile cha Minjingu kilichoko wilaya ya Babati Mkoani Manyara kuwa vitapunguza adha ya upatikanaji na bei ya mbolea kwa wakulima.

Ameongeza kuwa, katika kuvijengea uwezo viwanda vya mbolea vya ndani, Serikali inamjengea uwezo mwekezaji wa kiwanda cha Minjingu ili awe na uwezo wa kupata mikopo itakayomsaidia kuendeleza kiwanda na hivyo kuongeza uzaliahaji wa mbolea kutoka kiwandani hapo.

Pamoja na hayo, Rais amezitaka Mamlaka za Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanasimamia zoezi la utoaji wa ruzuku ya mbolea na kuwataka kutoacha jukumu hilo kusimamiwa na Wizara ya Kilimo pekee.
Watumishi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) wakifuatilia ratiba inayoendelea wakiwa wameketi kwenye jukwaa ulipofanyika uzinduzi wa mpango wa ruzuku ya mbolea na Rais Samia Suluhu Hassan kabla ya kuhutubia watanzania waliokusanyika kwenye maadhimisho ya sikuu ya wakulima yaani nanenane yaliyofanyika katika viwanja vya Mwakangale Jijini Mbeya tarehe 8/08/2022.

Aidha, Rais Samia amezitaka Wizara ya kilimo pamoja na Wizara ya Fedha kuhakikisha zinatoa kwa wakati pesa za ruzuku ili wakulima wapate mbolea kwa wakati itakayowafanya kuzalisha kwa tija.

Akizungumzia zoezi la sensa ya watu na makazi Rais Samia ametoa wito kwa watanzania kujitokeza na kushiriki kikamilifu zoezi la kuhesabiwa na kueleza takimwu sahihi za idadi ya watu na makazi ndiyo chanzo cha mipango bora ya maendeleo kwa nchi yeyote.

Mwisho Rais ametoa wito kwa wakulima wote kujisajili na kubainisha kuwa mbeleni vitambulisho vitatolewa kwa wakulima ili kuwawezesha kupata huduma mbalimbali zinazohusiana na masuala ya kilimo.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo (katikati) , kulia kwake ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka Prof. Anthony Mshandete na viongozi mbalimbali wakiwa eneo ulipofanyika uzinduzi wa mpango wa ruzuku ya mbolea na Rais Samia Suluhu Hassan siku ya kilele cha maonesho ya wakulima Nanenane Jijini Mbeya tarehe 8 Agosti, 2022.

Kwa Upande wake Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amemshukuru Rais kwa kuridhia kushuka kwa bei za mbolea kwani kilikuwa kilio kikubwa kwa wakulima kwa msimu uliopita.

Akiwasilisha bei za mbolea kwa Rais Samia kabla ya uzinduzi alisema mbolea aina ya DAP wastani wa bei kabla ya ruzuku ni 131,676 na baada ya ruzuku itauzwa shilingi 70,000 na serikali itachangia kwa shilingi 61,676, mbolea ya UREA kabla ya ruzuku inauzwa kwa wastani wa 124,734 baada ya ruzuku mkulima atanunua kwa shilingi 70,000 ambapo serikali itachangia kiasi cha shilingi 54,734.

Mbolea nyingine zitakazonufaika na ruzuku ni CAN kabla ya ruzuku ni shilingi 108,156 baada ya ruzuku itauzwa shilingi 60,000, mbolea aina ya SA inauzwa shilingi 82,852 baada ya ruzuku itauzwa shilingi 50,000 na NPK's zinauzwa kwa wastani wa shilingi 122,695 baada ya ruzuku zitauzwa 70,000 na kiasi kinachozidi serikali itachangia hivyo kupunguza mzigo wa bei ya mbolea kwa mkulima.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, ameipongeza Serikali kwa kusimamia na kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi yenye lengo la kuleta mapinduzi kwenye sekta ya kilimo.

"Ilani ya uchaguzi 2020/2025 imebeba ajenda ya kilimo kama kipaumbele kikuu kuikuza sekta hii kukuza mchango wake ifikapo 2030,"Chongolo aliongeza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news