Simba SC yawagonga St.George kama walivyogongwa Yanga SC

NA GODFREY NNKO

SIKU mbili baada ya mabingwa wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, Yanga SC kukung'utwa mabao 2-0 na mabingwa wa Ligi Kuu nchini Uganda Vipers SC katika mchezo wa kirafiki kwenye kilele cha Siku ya Wananchi (Yanga Day) watani zao Simba SC wameshinda mabao 2-0 dhidi ya St.George ya Ethiopia katika kilele cha Simba Day.
Yanga SC ambao pia ni mabingwa wa Kombe la Shirikisho la ASFC walianza kufungwa bao la awali kipindi cha kwanza kabla ya kuruhusu bao la pili kipindi cha pili.

Kipigo hicho kizito kwa mashabiki wa Yanga kilikuwa cha pili kwenye tukio linalofanana na hilo kwani mwaka 2021 walifungwa bao 2-1 na Zanaco United ya Zambia.

Ni katika mtanange ambao ulipigwa katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Dar es Salaam jijini Dar es Salaam ambapo kwa Yanga SC mwitikio wa mashabiki haukuwa wa kuridhisha vilivyo, lakini walitengeneza fedha nyingi kutokana na kiwango cha viingilio kuwa vikubwa huku kwa upande wa Simba SC leo Agosti 8, 2022 mashabiki ndani ya dimba hilo wamefurika.

Kwa Simba SC leo nao ulikuwa ni mchezo maalumu kwenye kilele cha Wiki ya Simba ikiwa ni mchezo wa kwanza kwa Kocha Zoran Maki ambaye ni raia wa Serbia.

Mabao ya Simba yamefungwa na mzawa Kibu Dennis na Nelson Okwa ambaye aliingia kipindi cha pili akitokea benchi.

Kocha Maki amesema kuwa, wamefurahi kupata ushindi kwenye mchezo wa kirafiki na wanakwenda kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga SC unaoatarajiwa kuchezwa dimba hilo la Benjamin Mkapa,Agosti 13.

Awali, kwa Yanga SC katika mchezo huo kocha Nasreddine Nabi alianza na kikosi cha wachezaji ambao walikuwepo msimu uliopita kabla ya kipindi cha pili kufanya mabadiliko ambayo kwa kiasi kikubwa ubora ulipungua kulinganisha na namna ambavyo walicheza kipindi cha kwanza.

Bernard Morrison, Aziz Ki na Bigirimana ni miongoni mwa wachezaji wa Yanga ambao walitambulisha na walipata nafasi ya kucheza.

Wakati huo huo, Simba SC wanapata ushindi katika mchezo wa kirafiki ikiwa wamekamilisha uhamisho wa mshambuliaji wa Kimataifa wa Serbia aliyekuwa anakipiga katika klabu ya NK Domzale inayoshiriki Ligi Kuu nchini Slovaneia.

Mshambuliaji huyo anayefahamika kwa jina la Dejan Georgijevic mwenye umri wa miaka 28 anajiunga na Simba SC ambao ni miamba wa soka nchini na Afrika Mashariki na kati kwa kandarasi ya miaka miwili.
Georgijevic aliyewahi kukipigia Bosnia na Herzegovina, Hungary, Serbia na Kazakhstan pamoja na Nelson Okwa wa Rivers United ni kati ya nyota waliotambulishwa.

Pamoja na kucheza kama fowadi, lakini Dejan ambaye ni chaguo la Kocha Zoran Maki aliyemleta pia beki wa kati Mohamed Ouattara anamudu pia kucheza kama winga wa kulia na kushoto.

Aidha,kwenye eneo la ushambuliaji Simba SC sasa ina mtaji mkubwa wa nyota huyo wa Serbia, mwingine ni Pape Ousmane Sakho, Okwa, John Bocco, Clatous Chama, Kibu Denis na Peter Banda.

Licha ya ushindi huo, awali dimba la Benjamin Mkapa lilitawaliwa na burudani kabambe kutoka kwa wasanii mbalimbali akiwemo Zuchu, Tunda Man na wengine wengi ambao walitoa burudani zilizoibua shangwe dimbani hapo.

Post a Comment

0 Comments