Rais Samia azindua mradi wa maji wa Shongo-Mbalizi

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amezindua mradi wa maji wa Shongo-Mbalizi uliopo mkoani Mbeya ambao utahudumia zaidi ya wakazi 80,000 katika eneo hilo.
Uzinduzi huo ameufanya leo Agosti 5, 2022 wakati wa siku ya kwanza ya ziara yake  ya siku tatu mkoani Mbeya.

Mheshimiwa Rais Samia akiwa mkoani humo atazindua miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa huo ikiwamo ya maji, afya, elimu na kilimo. 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji,Mhandisi Anthony Sanga amesema, mradi huo utakuwa na uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 8 hadi12 kwa siku.

“Mradi huu utaongeza upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Mbeya kutoka asilimia 44 zilizokuwepo kabla ya mradi huo hadi kufikia asilimia 65 za sasa baada ya mradi huo kukamilika,”amesema Mhandisi Sanga.

Kwa uapnde wake, Rais Samia amewataka wananchi wa Mbalizi kuutunza mradi huo ili maji yaendelee kupatikana. 

Aidha, amewataka watendaji wa taasisi za maji kuhakikisha maji yanapatikana kwa sababu serikali inatoa fedha nyingi kwenye miradi ya maji.

“Maji haya yamepatikana kwenye chanzo pale, ni matumaini yangu kwamba mtalinda kile chanzo. Ulinzi siyo jukumu letu, ni jukumu lenu wananchi. Mkiona watu wanaharibu chanzo kile, wawajibisheni kwa sheria mlizojiwekea.

“Niwaombe sana watendaji wa taasisi za maji, maji yasikosekane. Serikali inaweka fedha nyingi sana kuhakikisha maji yanapatikana. Kama maji yatakatika, toweni tangazo kwamba maji yatakatika pengine kwa sababu ya matengenezo,” amesema Rais Samia.

Pia amewataka wananchi kuendelea kufanya kazi ya uzalishaji kwa sababu serikali inakusanya mapato yake kutoka katika shughuli zao na fedha hizo ndiyo zinatumika kutekeleza miradi ya maendeleo.

“Wananchi tuendeleze uzalishaji, mapato ya serikali yanatokana na uzalishaji wenu. Sisi serikali tunakusanya kodi na tozo kutokana na shughuli mnazozifanya. Na kodi hizo ndiyo zinaleta maji, barabara, umeme, afya na elimu,”amesema Mheshimiwa Rais Samia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news