Serikali yatenga Bilioni 11.3/- kuweka lami na viwanda vidogo Njombe Mji

NA OR-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe.Innocent Bashungwa amesema,Serikali imetenga shilingi bilioni 11.3 kwa ajili ya kuweka lami, viwanda vidogo vidogo kwa ajili ya kusaga nafaka na kujenga karakana za wajasiriamali katika Halmashauri ya Mji wa Njombe mkoani Njombe.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akitembelea Soko Kuu la Njombe Mjini mara baada ya kulizindua rasmi soko hilo leo Agosti 10, 2022.Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa Innocent Bashungwa.

Mheshimiwa Bashungwa ameyasema hayo leo Agosti 10, 2022 wakati wa mkutano wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan na wananchi wa Mkoa wa Njombe uliofanyika kwenye uwanja wa Sabasaba mkoani humo.

Amesema, kupitia mradi wa TACTICS, Mhe.Rais aliwaelekeza kutenga shilingi Bilioni 11.3 kwa ajili ya kupendezesha Mji wa Njombe.

"Hivyo fedha hizo zitajengwa barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 6.2, kujenga viwanda vidogo kwa ajili ya kusaga nafaka na kujenga karakana za wajasiriamali.

"Niwahikilishie wananchi wa Njombe tu kuwa kazi hiyo itafanyika kikamilifu na mji huu utabadilika na kupendeza zaidi,"amesema Waziri Bashungwa.

Akiwa mkoani Njombe leo Rais Samia Suluhu Hassan amezindua Soko Kuu la Kisasa la Njombe Mji ambalo lina ukubwa wa mita za mraba 9,186, sakafu (floors) tatu.

Pia soko hilo lina mifumo na sehemu mbalimbali yakiwemo maduka 162, meza za biashara 407, vyoo 47, migahawa miwili, stoo sita, vizimba vya kuku 27, machinjio ya wanyama wadogo, sehemu za huduma za kibenki mbili, ofisi za utawala mbili, mfumo wa maji safi na maji taka na kisima kirefu cha maji.

Aidha, soko hilo lina uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 680 na limegharimu shilingi bilioni 10.2 hadi kukamilika kwake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news