Tanzania,Zambia kuendelea kushirikiana katika kukuza biashara

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Zambia zimekubaliana kuendelea kushirikiana katika kuibua fursa za biashara na kutatua mara moja changamoto zilizopo na zitakazojitokeza katika uwekezaji na biashara ili kukuza biashara na uwekezaji baina ya nchi hizo mbili.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Chipoka Mulenga walipokutana na kujadiliana kuhusu masuala ya uwezeshaji, biashara na kukuza uchumi baina ya Tanzania na Zambia katika kikao kilichofanyika Agosti 3, 2022, Jijini Dar es Salaam.

Mawaziri hao walikutana kufuatia maagizo yaliyotolewa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Hakainde Hichilema, Rais wa Jamhuri ya Zambia katika kikao chao kilichofanyika Ikulu Dar es Salaam tarehe 2 Agosti 2022 ambapo waliagiza Mawaziri wa Biashara kukutana mara moja kujadili masuala ya biashara baina ya Tanzania na Zambia.

Dkt.Kijaji ameeleza kuwa miongoni mwa changamoto zinazofanyiwa kazi ni pamoja na ucheleweshaji wa kuruhusiwa magari ya Tanzania katika mpaka wa Tunduma Nakonde, Wafanyabiashara wadogo wakinyanganywa pasi zao za kusafiria, na Madereva Watanzania kuibiwa mizigo.
Kwa upande wake Waziri wa Biashara na Viwanda wa Zambia amesema wanafanyia kazi changamoto zilizowasilishwa huku akisisitiza lengo ni kuimarisha biashara ndani ya Afrika.

Katika kikao hicho, Mawaziri walikubaliana kufanya kikao cha pamoja ambacho kitajadili kwa kina masuala ya kibiashara na changamoto zilizopo baina ya Tanzania na Zambia. Waziri wa Zambia aliahidi ndani ya wiki mbili kuwasilisha mapendekezo ya tarehe za kikao hicho na ilikubalika kitanguliwe na kikao cha Sekta Binafsi.
Aidha, Mawaziri hao walisisitiza kuendeleza ushirikiano ambao umekuwepo tangu enzi za Mhe. Mwalimu Julius Nyerere Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Keneth Kaunda, Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Zambia na sio kwa kushindana.

Vilevile, Mawaziri hao walikubaliana kuendeleza dhamira nzuri ya Waheshimiwa Marais wa nchi zote mbili ya kuondoa vikwazo na kuwezesha biashara na uwekezaji ili kukuza uchumi na hatimaye ajira kwa wananchi wa pande zote mbili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news