TANZIA:Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Ilala jijini Dar es Salaam,Benjamin Jackson Mwakasonda afariki


Mahakama ya Tanzania inasikitika kutangaza kifo cha Mtumishi wake aliyekuwa Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Ilala jijini Dar es Salaam, Mhe. Benjamin Jackson Mwakasonda (pichani) kilichotokea leo tarehe 26 Agosti, 2022.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt, marehemu Mwakasonda amekutwa na umauti katika hospitali ya Kairuki jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.

Marehemu Mwakasonda aliwahi kufanya kazi Mahakama ya Mwanzo Songea, Mahakama ya Mwanzo Namabengo mkoani Ruvuma na Mahakama ya Mwanzo Kariakoo-Dar es Salaam.

Mpaka anafikwa na umauti, marehemu Mwakasonda alikuwa akihudumu katika Mahakama ya Mwanzo Ilala, pia alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Ubungo (UFA). Aidha; marehemu aliwahi kuwa Katibu wa Timu ya 'Mahakama Sports' kuanzia 2010 hadi 2013.

Mhe. Sarwatt amesema kuwa taratibu za mazishi zinafanyika nyumbani kwa marehemu Sinza-Darajani, taarifa zaidi zitatolewa mara baada ya kukamilika kwa maandalizi hayo.

Mahakama ya Tanzania inaungana na ndugu, jamaa na marafiki kuomboleza katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wetu.

BWANA AMETOA NA BWANA AMETWAA, JINA LAKE LIHIMIDIWE.

Post a Comment

0 Comments