TULITAWALIWA KWA SABABU YA SAYANSI NA TEKNOLOJIA-WAZIRI MKENDA

NA MATHIAS CANAL-WEST

KATIKA kutekeleza kwa vitendo ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025 na mpango mkakati wa serikali kupitia bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia mwaka 2022/2023 imedhamiria kuwekeza zaidi kwenye Sayansi na Teknolojia ikiwa ni pamoja na eneo muhimu la utafiti na elimu tiba.
Serikali imeeleza kwa uwazi dhamira yake ya kuhakikisha kuwa wanafunzi wanavutiwa na masomo ya Sayansi na Teknolojia ambapo imepanga kuwapatia udhamini wa masomo kwa ngazi ya chuo kikuu kwa wanafunzi watakaofaulu vizuri matokeo ya kidato cha sita katika masomo ya Sayansi na Elimu Tiba.

Pia katika kuhamasisha uandishi katika majarida mbalimbali nchini serikali imepanga kutoa Shilingi milioni hamsini kama motisha kwa wahadhiri kutoka chuo chochote cha serikali ama binafsi watakaoweza kuchapisha andiko kwenye majarida ya juu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof. Adolf Mkenda ameyasema hayo hivi karibuni Jijini Dar es laam wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari nchini juu ya mwelekeo wa Wizara, Vipaumbele na maeneo ya kimkakati katika utekelezaji kwa Mwaka wa fedha 2022/23.

Amesema kuwa ili nchi iweze kuendelea inahitaji zaidi sekta ya Sayansi, Teknolojia na Tiba kwani ndio msingi na moyo wa uchumi kwa taifa.

Amesema kuwa mambo mengine yatafuata na yanapaswa kuendelea lakini ni wajibu wa serikali na wadau wa elimu kuhakikisha kuwa Sayansi, Teknolojia na Elimu Tiba vinapewa kipaumbele maradufu.
“Tulitawaliwa kwa Sababu ya Sayansi na Teknolojia, Tulitumia Mishale na Mikuki wakaja na Bunduki, Tulitumia ngalawa baharini wenyewe wanakuja na Mamerikebu makubwa ni wazi tulitawaliwa kwa sababu hatukuwa na Sayansi na Teknolojia,”amesema Waziri Mkenda.

Waziri Mkenda amesema, pamoja na mambo mengine katika utoaji wa mikopo ya elimu ya juu, serikali imeweka kipaumbele zaidi kwenye utoaji wa mikopo kwa wanafunzi waliosoma masomo ya Sayansi, Uhandisi na Tiba.
Kuhusu michango ya chakula shuleni, Prof Mkenda amesema kuwa ni kweli kuna muongozo wa Lishe lakini zipo kaya zisizoweza kulipia kabisa kutokana na uduni wa maisha hivyo serikali inaliangalia na kulifanyia kazi jambo hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news