Rais Dkt.Mwinyi ateua viongozi mbalimbali leo

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Agosti 3, 2022 na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar, Mhandisi Zena A.Said.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amemteua Masoud Hussein Iddi kuwa Katibu Mkuu katika Ofisi ya Rais-Ikulu.

Ndugu Iddi, kabla ya uteuzi alikuwa Mkurugenzi Ofisi ya Rais, huku Moh'd Ali Abdalla akiteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mjini Magharibi.

Kabla ya uteuzi huu wa Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi, Moh'd alikuwa Katibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora.

Vile vile, Mheshimiwa Rais Dkt. Mwinyi amemteua Radhia Haroub kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kusini Unguja.Kabla ya uteuzi huo, Radhia alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mjini Magharibi.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amemteua Dkt.Ali Khatib Bakari kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kaskazini Pemba. Kabla ya uteuzi huo, Dkt.Ali alikuwa Mkuu wa Divisheni ya Utafiti wa Udongo na Mimea katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Zanzibar (ZARI), Pemba. Aidha, Ali Mohamed Mwinyi aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kaskazini Pemba atapangiwa kazi nyingine.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, pia Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amemteua Bakari Haji Bakari kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Biashara la Taifa la Zanzibar (ZSTC). Kabla ya uteuzi huo, Bakari alikuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara Zanzibar.

Aidha, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amemteua Rajab Yussuf Khamis Mkasaba kuwa Mkuu wa Wilaya ya Unguja Kusini. Kabla ya uteuzi huo, Rajab alikuwa Mwandishi wa Habari wa Rais.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uteuzi huo umeanza leo Agosti 3, 2022 ambapo Katibu Mkuu na Mkuu wa Wilaya wataapishwa Ijumaa ya Agosti 5, 2022 Ikulu jijini Zanzibar kuanzia saa 3:00 asubuhi.

Wakati huo huo, taarifa hiyo imefafanua kuwa, Mheshimiwa Rais pia atawaapisha Mheshimiwa Juma Makungu Juma, Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi na Rashid Ali Salim, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda ambao uteuzi wao ulifanyika Juni 30, 2022.

Sambamba na Dkt.Maua Abeid Daftari, Kamishna wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambaye uteuzi wake ulifanyika Julai 8, 2022.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news