Wadau wa habari waliipinga sheria hii siku moja baada ya kupitishwa-Mjumbe TEF

NA MWANDISHI WETU

KATIBU mstaafu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ambaye kwa sasa ni mjumbe wa jukwaa hilo, Bw.Neville Meena amesema kuwa, Sheria ya Vyombo vya Habari ya Mwaka 2016 ilikataliwa siku ya kwanza baada ya kusainiwa na kuanza kutumika kama mwongozo kwa vyombo vya habari nchini.
Meena ameyasema hayo leo Agosti 17, 2022 wakati akizungumza na Kituo cha Radio cha Nyemo jijini Dodoma.

“Sheria ya Habari ya Mwaka 2016 ilipingwa na wadau wa habari siku moja baada ya kupitishwa ili kutumika. Si kwamba, hakukuwa na vitu muhimu kwa wanahabari, wadau waliona imebeba mitego na madhara mengi kwa wanahabari na vyombo vya habari,’’amesema Meena.

Amesema, kutokana na yaliyomo kwenye sheria hiyo, wadau wa habari waliamini vyombo vya habari vitazidi kusinyaa.

‘‘Wadau wa habari wakiwemo UTPC, TAMWA, MISA-TAN, LHRC, TLS, Twawezaa, Sikika, THRDC na wengine, walikaa pamoja na kuangalia madhara yanayoweza kutokea kutokana na sheria hiyo.

‘‘Tunashukuru hatua zilipofika kwa sasa. Rais (Samia Suluhu Hassan) amekuwa na utashi wa kufanya mabadiliko lakini hata waziri aliyepo sasa (Nape Nnauye), mwelekeo wake ni huo,’’amesema Meena.

Amesema, baada ya serikali kuona umuhimu wa kupitia sheria hizo, iliandaa maboresho na kupeleka kwa wadau kupitia.

Pia amesema kwamba, baada ya wadau kupata mapendekezo hayo, waliyapitia na kuongeza pia kupunguza huku wakipitia zaidi vifungu vingine vya sheria vilivyoonekana kuwa hatari kwa wanahabari kutekeleza majukumu yao.

‘‘Hata yale mapendekezo yaliyoletwa na serikali, nayo tuliyaangalia na kuyapitia kisha kukubalina na baadhi na kisha mengine kutokubaliana nayo.
‘‘Kimsingi kuna baadhi ya vipengele ni vigumu kutelekezwa kama sheria ilivyompa madaraka mtu mmoja kufungia chombo cha habari. Hii ni hatari sana,” amesema Meena.

Ametaja eneo lingine lenye ukakasi kuwa ni matangazo ya serikali kuratibiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo.

‘‘Sasa hapa ni kuwa, kama Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo haelewani nawe ama chombo chako, huwezi kupata matangazo. Tukumbuke uchumi wa vyombo vya habari ni matangazo,” amesema Meena.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news