Wajitoa ufahamu kwa kupora vitendea kazi vya Sensa 2022

NA DIRAMAKINI

BAADHI ya watu wasiokuwa na nia njema wameamua kujitoa ufahamu na kufanya hujuma kwa kupora vitendea kazi vya umma ambavyo vinatumika kufanikisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ambalo limeanza rasmi Agosti 23, mwaka huu.

Hujuma hiyo imefanyika mkoani Arusha na Katavi kwa makarani wawili kuporwa vifaa vyao vya kukusanyia taarifa maarufu kama vishikwambi.

Wizi wa vishikwambi hivyo, huenda usiwe na faida kwa mtu yeyote ambaye ameamua kuvichukua kwa kuwa, licha ya kutekeleza jukumu hilo muhimu kwa Taifa vimeunganishwa na mfumo maalumu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambayo itakwamisha mipango yao ya kuvitumia mitaani.

Tukio la kwanza limetokea jijini Arusha ambapo karani aliyetambuliwa kwa jina la Saraphia Kiwango ameporwa kishikwambi chake alipokuwa akielekea kuanza kuhesabu makundi maalum katika Kata ya Unga Limited jijini humo.

Diwani wa Kata ya Unga Limited, Mahmoud Said amesema alipokea taarifa usiku wa kuamkia Agosti 23, kuwa kuna karani ameibiwa kishikwambi na mumewe kujeruhiwa kichwani na bodaboda wawili.

"Jana usiku hawa makarani wa sensa waliitwa kwa mtendaji wakati wanakwenda huko ndiyo wakakutana na vibaka waliokuwa kwenye bodaboda wakamjeruhi mumewe na kumpora kishikwambi kisha kutoweka kusikojulikana," amesema Diwani Said.

Naye Mtendaji wa kata hiyo, Sophia Laizer amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwa karani huyo baada ya kuibiwa kishkwambi hicho na kuwa alivamiwa na vijana hao akiwa njiani kuelekea kuhesabu makundi maalum.

"Ni kweli tukio hilo lilitokea jana usiku lakini ameshapewa kishkwambi kingine na anaendelea na kazi," amesema Laizer.

Mratibu wa Sensa Wilaya ya Arusha, Maneno Maziku amekiri kutokea kwa tukio hilo ila kila kitu kipo sawa na aliyejeruhiwa anaendelea vizuri na maeneo mengine zoezi linaenda vizuri.

"Ni kweli aliporwa kishikwambi na mume wake kujeruhiwa kichwani, lakini ameshapewa kishikwambi kingine anaendelea na kazi, lakini pia majeruhi hali yake inaendelea vizuri,"amesema,

Wakati huo huo, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Said Mtanda amesema hali ni shwari katika maeneo mengine na kuwa watakaotaka kuvuruga sensa watashughulikiwa.

"Hali ni shwari ila jana usiku kuna karani mmoja wahuni walitaka kumshambulia kwa sababu tuliweka mgambo na polisi walidhibitiwa," amesema.

Mbali na hayo, katika Kata ya Majimoto Halmashauri ya Mpimbwe mkoani Katavi, karani aliyetajwa kwa jina la Kenani Kasekwa amevamiwa na mtu asiyejulikana na kumwibia kishikwambi na fedha taslimu shilingi 760,000.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Catherine Mashala alisema,“Mwizi aliingia chumbani akaiba vitu hivyo na vingine, inavyoonekana alipuliza dawa ili walale usingizi fofo akapata mwanya wa kuiba pia redio aina ya subwoofer na simu,”amesema.

Amesema baada ya kutokea tukio hilo karani huyo alitoa taarifa kituo cha Polisi Majimoto na polisi walifanya msako kisha kumkamata mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa.

Katika hatua nyingine, Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi 2022, Anne Makinda amewataka wananchi ambao hawatafikiwa na makarani wa Sensa kutokuwa na wasiwasi kwa kuwa shughuli hiyo itaendelea kwa siku saba nchini.

Makinda amesema hayo jijini Dodoma baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suhuhu Hassan kuhesabiwa kwenye Ikulu ya Chamwino.

“Tumeanza leo, tutaendelea mpaka siku saba, makarani wakifanikiwa kwa leo watafanya kwa asilimia 15 tu.Tunaomba wananchi wasilalamike kama hawatafikiwa na makarani leo. Sio lazima ufikiwe leo, ni siku saba. Tunaomba utulivu uwepo,"amesema Makinda.

Pia amewataka wananchi kuwa watulivu wakiandaa taarifa zao muhimu zikiwemo za NIDA na mawasiliano ili kama karani hataelewa taarifa hizo atafanya mawasiliano kwa muhusika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news