Waziri Dkt.Ndumbaro:Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali zingatieni maslahi mapana ya nchi

PRISCA ULOMI NA SARA MWAKYUSA-OWMS

SERIKALI imeitaka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) izingatie maslahi mapana ya nchi katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku ya kusimamia, kuratibu na kuendesha mashauri ya madai na usuluhishi kwa niaba ya Serikali na taasisi zake ili kuhakikisha kuwa inatetea maslahi ya Serikali na wananchi ndani na nje ya nchi
Baadhi ya Wakurugenzi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakimsikiliza Waziri wa Katiba na Sheria Dkt Damasi Ndumbaro (aliyeketi mbele meza kuu) wakati wa kikao cha kujadili utekelezaji wa majukumu ya Ofisi hiyo kilichofanyika jijini Dar es Salaam

Hayo yameelezwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) wakati wa kikao kazi baina yake na Menejimenti ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali iliyoongozwa na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Nalija Luhende kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwa na majadiliano na taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo ili kujadili utekelezaji wa majukumu ambapo kikao hicho kilifanyika jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damasi Ndumbaro (Mb) akizungumza na Menejimenti ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (hawapo pichani) wakati wa kikao chake cha kujadili utekelezaji wa majukumu ya Ofisi hiyo kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Dkt. Ndumbaro alisema kuwa ni muhimu Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ihakikishe inaiwakilisha vema Serikali na taasisi zake kwenye mashauri ya madai na usuluhishi ili kuhakikisha kuwa Serikali inapata inachostahili kwa maslahi mapana ya taifa na wananchi wake kwa ujumla ili kulinda hadhi ya Serikali

“Wizara hii imeshikilia haki ya wananchi; amani na utulivu wa nchi; na uwekezaji nchini; hivyo ni muhimu kuhakikisha wananchi wanapata haki yao kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi zilizopo; nchi inavutia wawekezaji kwa kuwahakikisha amani na utulivu; pamoja na kuwa na miongozo stahiki inayohusu mikataba katika uwekezaji ili kulinda maslahi mapana ya taifa,” amefafanua Dkt. Ndumbaro. Menejimenti ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damasi Ndumbaro (hayupo pichani) wakati wa kikao cha kujadili utekelezaji wa majukumu ya Ofisi hiyo kilichofanyika jijini Dar es Salaam

Pia, ameongeza kuwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali inaendesha mashauri ya madai na usuluhushi kwa maslahi mapana ya taifa la Tanzania hivyo ni muhimu kwa watumishi kutekeleza majukumu kwa kuweka uzalendo mbele; kuzingatia taaluma; maadili ya kazi; weledi na uzoefu kwenye maeneo ya migogoro, usuluhishi, na majadiliano ikiwa ni pamoja na kushirikisha wadau ili kuhakikisha kuwa Serikali inashinda na kunufaika na uwepo wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya Ofisi hiyo kwa niaba ya Menejimenti, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Nalija Luhende amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Ofisi hiyo mwaka 2018 hadi mwezi Juni mwaka 2022; Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imeendesha jumla ya mashauri 5,905 ambapo kati ya hayo mashauri 5,768 ni ya madai na mashauri 137 ni ya usuluhishi.

Dkt. Luhende ameongeza kuwa ili kufikia azma ya kupanua wigo wa utendaji wa Ofisi hiyo na kuongeza ukaribu katika kuhudumia wananchi, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ina Ofisi 17 ambazo zimefunguliwa kwenye mikoa yote yenye masjala za Mahakama Kuu ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na kwenye mikoa ya Dodoma; Mtwara; Iringa; Ruvuma; Tanga; Kilimanjaro; Arusha; Kigoma; Mara; Mwanza; Kagera; Shinyanga; Tabora; Rukwa; Mbeya; na Morogoro.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damasi Ndumbaro (Mb) (aliyesimama mbele katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Menejimenti ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali baada ya kikao kazi na Ofisi hiyo kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Dkt.Ndumbaro yuko Dar es Salaam kwenye ziara ya kikazi ambapo ataonana na kuzungumza na taasisi za Wizara hiyo ikiwemo Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali; Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali; Ofisi ya Mwendesha Mashtaka; Tume ya Haki za Binadamu; Wakala wa Vizazi na Vifo; na Taasisi ya Msaada wa Kisheria ili kujadili utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizo kwa Serikali kwa niaba ya wananchi

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news