BILA YA SUPU YA PWEZA:Nguvu wapi wapoteza, balehe wakitimiza, Watafiti wajibikeni haraka

NA LWAGA MWANBANDE

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameagiza kufanyika utafiti wa kwa nini vijana balehe wana matizo ya lishe ili kuepuka kuwa na Taifa goigoi.

“Watoto balehe hebu tufanye utafiti, tunakosea wapi, kwa nini tunakuwa na lishe ndogo. Kwa nini kunakuwa na hizo gaps. Kwa nini tunakuwa na watoto wazuri kiafya, Je? Ni masuala ya mitindo? Nataka sijui slim, nataka sijui niwe kilo ngapi, nataka sijui mbavu ikae vipi kuna nini hasa kwa nini wawe hivi.

“Watafiti fanyeni tafiti, tuna tatizo, kwa sababu halisemwi ni siri linawaumiza zaidi vijana wetu, mara haya ninayoyataja, mara vumbi la Kongo, mara kitu gani, lakini tatizo kubwa liko kwenye lishe. Sasa watafiti fanyeni tafiti vijana wetu waweze kuzaa watoto wenye afya. Tutafika mahali hatujui mume nani, mke nani. Kwa hiyo twendeni tukasimamie hilo.

"Wavulana mnaonekana mmevaa suti, lakini kuna vigenge vya udongo la Kongo chungu mzima, Amos (Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makala) unanitazama huko ndio kunasifika kwa chipsi;

Mheshimiwa Rais Samia ameyasema hayo leo Septemba 30, 2022 wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa usimamiaji shughuli za lishe jijini Dodoma huku akisisitiza hilo jamii yote inapaswa kufanyia kazi, kwani wakiacha hilo liendelee Taifa litakuwa na watu goigoi. Ungana na mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande uweze kupata maarifa kupitia shairi hapa chini;


1:Hatari supu ya pweza, vijana inawalaza,
Kile wanachokoleza, nini lishe yawakwaza?
Jamii kuidumaza, wazalisha ni vilaza,
Ni masuala ya lishe, yapatiwe ufumbuzi.

2:Lishe nguvu yaongeza, na uzazi kukoleza,
Lishe duni yapunguza, vijana yawalegeza,
Kutaka supu ya pweza, waweze kujiongeza,
Ni masuala ya lishe, yapatiwe ufumbuzi.

3:Hebu chunguza chunguza, vijana na ukilaza,
Si akili za kuwaza, kizazi kukiongeza,
Kuzaa kubwa gereza, yawa shida kutokeza,
Ni masuala ya lishe, yapatiwe ufumbuzi.

4:Rais ameagiza, watafiti kuchunguza,
Nguvu wapi wapoteza, balehe wakitimiza,
Ni lishe wanapunguza, au kitu chawakwaza?
Ni masuala ya lishe, yapatiwe ufumbuzi.

5:Chini chini wajiliza, ndoa ukizichunguza,
Mambo chumbani yakwaza, siyo ya kutosheleza,
Wengine yawakimbiza, nguvu kuzitafutiza,
Ni masuala ya lishe, yapatiwe ufumbuzi.

6:Kesho ndiyo twaiwaza, vipi nchi tutajaza,
Vijana tunawawaza, nguvu zikijipunguza,
Hata lini huyu pweza, ataweza ziongeza?
Ni masuala ya lishe, yapatiwe ufumbuzi.

7:Nguvu kitaka ongeza, vyakula tunaviweza,tul
Tunavuna twavijaza, hivyo tukivimaliza,
Nguvu nyingi taongeza, tendo la ndoa kuweza,
Ni masuala ya lishe, yapatiwe ufumbuzi.

8:Kujenga nguvu twaweza, dona mwilini kijaza,
Protini kuongeza, madini tunajijaza,
Uzazi kuuongeza, hapo vijana waweza,
Ni masuala ya lishe, yapatiwe ufumbuzi.

9:Mafuta ninayawaza, na chumvi naichunguza,
Twakaanga vya kuoza, mwili vinaulegeza,
Vijana wavikimbiza, nguvu zao wazitenza,
Ni masuala ya lishe, yapatiwe ufumbuzi.

10:Rais ameagiza, hili jambo kuchunguza,
Vijana kazi kuweza, bila ya supu ya pweza,
Uzazi tutaongeza, tusije kujimaliza,
Ni masuala ya lishe, yapatiwe ufumbuzi.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news